Kazi na masharti kwa Zico akiaminiwa kuinoa KCB
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya KCB imetangaza Jumatatu kuajiri naibu wa kocha wa Gor Mahia, Zedekiah “Zico” Otieno kuwa kocha wake mpya mkuu.
Mchezaji huyu wa zamani wa Gor Mahia, ambaye aliwahi kunoa mabingwa hao mara 18 wa Kenya msimu kadha, ameanza kazi Juni 10.
Kibarua alichopewa msimu 2019-2020 kikiwa kufikisha wanabenki hawa katika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.
Zico, ambaye alikuwa naibu wa Hassan Oktay katika msimu uliokamilika 2018-2019, amechukua mikoba ya ukocha kutoka kwa kocha mwingine wa zamani wa Gor, Frank Ouna.
“Tuko makini kuendelea kuimarisha kikosi chetu ili kuhakikisha tunafika mbali iwezekanavyo katika mashindano tunayoshiriki. Tunalenga kumaliza msimu ujao katika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu kwa hivyo tunalenga kutafuta ujuzi utakaotimiza azma hiyo,” amesema Rais wa klabu ya soka ya KCB, Paul Russo, ambaye pia ni mmoja wa Wakurugenzi wakuu katika benki hiyo.
KCB ilikamilisha msimu 2018-2019 katika nafasi ya 10 kwa alama 45 ikiwa ni ufanisi mkubwa kwa sababu ilikuwa imeingia Ligi Kuu.
Zico, 50, aliwahi kuwa kocha mkuu wa Posta Rangers.