Makala

AFYA: Njia mbalimbali za kuondoa sumu mwilini

June 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MARADHI mengi yanayowasumbua watu hivi leo yanatokana na sumu zilizopo katika miili.

Mabadiliko ya hali ya hewa na mtindo wa maisha huchangia kutengenezeka na kuingia kwa sumu nyingi ndani ya mwili wa binadamu.

Sumu hizi hutokana na vyakula, vinywaji na hata mazingira tunamoishi.

Zinaweza kuleta madhara makubwa mwilini kama vile kusababisha baadhi ya viungo kushindwa kufanya kazi na hata aina mbalimbali za saratani.

Kula vyakula vya asili

Baadhi ya watu husifu vyakula vya viwandani na vile vya kukaangwa kuwa ndivyo vyakula bora. Ili uweze kuondoa sumu mwilini mwako, ni vyema ukaepuka vyakula hivi kwani huwa vina viini vinavyojenga sumu mwilini. Fanya mazoea ya kula vyakula vya kuchemsha tena vya asili. Matunda na mbogamboga zisizo na dawa na kemikali za kisasa zitakufaa zaidi.

Kunywa maji mengi

Ni dhahiri kuwa miili yetu imejengwa kwa maji asilimia 70, hivyo kunywa vinywaji kama vile soda na juisi za viwandani kunaongeza sumu mwilini.

Ni muhimu kufahamu kuwa ufanyaji kazi wa viungo kama vile figo hutegemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa maji ya kutosha mwilini. Hivyo, maji yakikosekana ni dhahiri kuwa sumu nyingi sana hazitaondolewa mwilini.

Fanya mazoezi

Kufanya mazoezi kutawezesha viungo vyako vya mwili kufanya kazi jinsi ipasavyo. Ni dhahiri pia unapofanya mazoezi, utatokwa na jasho; na hii ni njia nzuri ya kutoa taka mwilini ikiwemo sumu zilizoingia katika mwili wako. Unaweza kufanya mazoezi ndani au hata nje kutegemea vile unavyopenda mwenyewe.

Punguza mafuta

Jizoeshe kupunguza ama kuepuka mafuta katika vyakula vile unavyokula kwani si aina zote za mafuta zinafaa kwenye mwili wako.

Kula mafuta haya ni kuongeza sumu mwilini mwako. Jitahidi kuepuka na kupunguza ulaji wa mafuta uwezavyo ili uweze kuondoa sumu mwilini mwako.

Kula vyakula vya nyuzinyuzi

Unatakiwa kufahamu kuwa vyakula vyenye nyuzinyuzi ni vizuri pia katika kusafisha mwili na kuondoa sumu. Ulaji wa vyakula hivi utakuwezesha kuondoa kiasi kikubwa cha sumu mwilini.

Tambua bidhaa unazozitumia

Watu wengi hununua na kutumia bidhaa bila kuzifahamu vyema. Inawezekana ni kutokana na ukosefu wa elimu au kuishi kwa mazoea. Elewa kila chakula au kinywaji unachotumia kina nini ndani yake. Je, malighafi yaliyotumika ni yapi?

Vinywaji vingine na vyakula vina viambata ambavyo ni sumu katika mwili wako. Kama sio lazima kutumia kitu, basi kiepuke.

Epuka matumizi holela ya plastiki

Vyombo vilivyotengenezwa kwa plastiki vimetokana na kemikali mbalimbali ambazo nyingine ni hatari kwa afya yako.

Matumizi ya vyombo vya chakula vilivyotengenezwa kwa plastiki yanaweza kusababisha kemikali kama vile Bisphenol A (BPA) pamoja na polymer kuingia mwilini mwako.

Hatari huzidi pale ambapo vyombo hivi hutumika kuwekea vyakula vya moto, kwani husababisha kemikali hizi kuyeyuka na kuingia kwa kiasi kikubwa mwilini.

Epuka matumizi ya pombe

Kama ilivyo kwa vyakula vya viwandani, pombe nyingi hutengenezwa kwa kutumia kemikali mbalimbali ambazo nyingine ni hatari kwa afya yako. Ili kuondoa na kupunguza kiasi cha sumu zinazoingia mwilini mwako jitahidi kuepuka matumizi ya pombe na kutumia vinywaji vingine kama vile maji.

Tumia dawa kwa uangalifu

Dawa zisipotumika vyema zinaweza kuwa sumu hatari mwilini mwako. Epuka kutumia dawa bila ushauri wa kitaalamu. Dalili za ugonjwa mmoja zinaweza kuwa pia ni dalili za ugonjwa mwingine, hivyo ni vyema kufanya vipimo kabla ya kuanza kutumia dawa.

Unaweza kutumia njia za asili kutibu magonjwa mbalimbali badala ya kukimbilia kutumia dawa za viwandani ambazo zinaweza kusababisha sumu kuingia mwilini mwako.