Michezo

Manchester United wasaka kizibo cha Pogba

June 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

MANCHESTER United wameanza mipango ya kutafuta kizibo cha kiungo Paul Pogba ambaye anatazamiwa kuyoyomea kambini mwa Real Madrid, Uhispania.

Licha ya baadhi ya vinara wa Man-United kushikilia kwamba huduma za Pogba si za kunadiwa hivi karibuni, kocha Ole Gunnar Solskjaer amekiri kuwa anafuatilia baadhi ya wachezaji ambao wana uwezo wa kujaza pengo la kiungo huyo mzaliwa wa Ufaransa.

Kufikia sasa, Pogba ambaye pia anahusishwa na uwezekano wa kurejea kambini mwa Juventus, Italia angali na mkataba wa miaka miwili kati yake na Manchester United.

Iwapo Real watamshawishi Pogba kutua uwanjani Santiago Bernabeu, Solskjaer amefichua kwamba nyota Christian Eriksen wa Tottenham Hotspur ni miongoni mwa wachezaji atakaowapendekezea Man-United kumtwaa.

Eriksen aliyehusishwa na uwezekano wa kutua Real, huenda sasa akalazimika kujiunga na Man-United baada ya Real waliokuwa wakiziwania huduma zake kumsajili fowadi Eden Hazard kutoka Chelsea.

Mbali na Eriksen ambaye amewataka Tottenham kumwachilia kufikia Agosti mwaka huu, Man-United wanazisaka pia huduma za viungo watatu, akiwemo Mbelgiji Youri Tielemans ambaye kwa sasa anavalia jezi za Leicester City kwa mkopo kutoka AS Monaco.

Hata hivyo, ni matumaini ya Solskjaer kwamba Pogba atasalia ugani Old Trafford kadri anavyojiandaa kusajili viungo wengine wa haiba kubwa watakaoshirikiana vilivyo na nyota huyo aliyewachochea Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2018.

Rakitic

Wachezaji wengine wanaomezewa mate na Man-United ni Ivan Rakitic wa Barcelona na Bruno Fernandes wa Sporting Lisbon, Ureno.

Wanapojizatiti kuziba pengo la Pogba, Man-United pia wanajitahidi kusaka kipa ambaye atachukua pahala pa mlinda-lango David de Gea anayehusishwa na uwezekano wa kuyoyomea kambini mwa PSG nchini Ufaransa.

Mbali na kipa wa AC Milan, Gianluigi Donnarumma, Man-United pia wanayakeshea maarifa ya Jordan Pickford wa Everton.

Donnarumma ni miongoni mwa makipa wazuri nchini Italia na amekosa mechi mbili pekee za Milan ligini tangu 2015. Ana kandarasi na Milan hadi 2024, ingawa mshahara wake unaoaminika kuwa Sh676.3 milioni kila mwaka, huenda ukawa mzigo kwa waajiri wake kumudu.

Tovuti ya Calciomercato inadai kwamba ombi la kati ya Sh7 bilioni na Sh8 bilioni huenda likatosha kushawishi Milan kuruhusu kipa huyo chipukizi kuondoka Italia. De Gea ambaye ni mzaliwa wa Uhispania, anataka Man-United iongeze mshahara wake kutoka Sh26 milioni kwa

wiki hadi Sh45 milioni, kiasi ambacho PSG iko tayari kumpa kipa huyo mwenye umri wa miaka 28.