Mnawaumiza Wakenya kushindia kuongeza bei ya mafuta, serikali yaambiwa
CHARLES WASONGA
SERIKALI imelaumiwa kwa bei za juu za mafuta nchini kutokana na kutoza bidhaa hizo kiwango cha juu cha ushuru.
Mamlaka ya Kudhibiti Sekta ya Kawi nchini (EPRA) Jumanne iliwaambia maseneta kwamba hali hiyo ndio inayochangia Wakenya kununua mafuta kwa bei za juu ikilinganishwa na wananchi katika mataifa jirani, haswa Tanzania.
Mamlaka hiyo, zamani ikijulikana kama Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC), iliongeza kuwa bei ya mafuta ghafi katika masomo ya kimataifa, kiwango cha mafuta ambacho Kenya hununua na gharama ya usambazaji mafuta pia huchangia ongezeko la bei ya mafuta aina ya petroli, dizeli na mafuta taa.
Mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Bw Pavel Oimeke, hata hivyo, aliwahakikishia maseneta kwamba asasi hiyo itahakikisha kuwa inashusha bei ya mafuta sambamba na kushuka kwa bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa.
“Lakini miongoni mwa sababu zote tulizotaja kama wasilisho letu kwa kamati hii, ushuru wa juu ndio wenye uzito mkubwa. Zaidi ya asilimia 50 ya bei ya mafuta katika masoko ya rejareja huwa ni aina nyingi za ushuru ambazo hutozwa na serikali,” akasema.
“Hii ndio maana kwa mfano mafuta aina ya petroli inauzwa sasa kwa Sh112 ilhali nchini Tanzania bidhaa hiyo inauzwa kwa Sh104.37, kwa lita moja,” akaongeza Bw Oimeke.
Mkurugenzi huyo mkuu aliongeza kuwa bei ya mafuta nchini Tanzania hukadiriwa kwa kuzingatia mafuta yaliyoagizwa kwa kipindi cha siku 60 ilhali nchini Kenya bei hiyo hukadiriwa kwa kuzingatia mafuta yaliyoagizwa baada ya kipindi cha siku 30.
“Hii ndio maana baada ya bei ya mafuta hupanda katika masoko ya kimataifa Watanzania wanaweza kufurahia bei za chini kwa siku 30 zaidi kuliko Wakenya,” akasema Bw Oimeke ambaye alikuwa ameandamana na mkurugenzi anayesimamia kitengo cha petroli na gesi katika EPRA Bw Edward Kinyua.
Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Nyeri Ephraim Maina ilikuwa imemwita Bw Oimeke aeleze sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta nchini hata wakati ambapo bei ya bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa huwa imeshuka.
Bw Oimeke alisema bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa imekuwa ikipanda kuanzia Januari mwaka huu kuliko ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka jana.
“Kwa mfano mnamo Januari mafuta yaliuzwa kwa Dola 59.5 (sawa na Sh6,000) kwa pipa. Bei hiyo imepanda hadi dola 73.05 (takriban 7,400) mnamo mwezi wa Mei),” akasema.