Habari

Uhispania yapongeza Ajenda Nne Kuu na vita kukabiliana na ufisadi Kenya

June 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA na PSCU

UHISPANIA Jumanne ilimpongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa msimamo wake thabiti wa kukabiliana na ufisadi na uhalifu wa kiuchumi hapa nchini huku ikiahidi kupiga jeki mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama ya chini.

Akizungumza alipomtembelea Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi, Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni na Ushirikiano wa Muungano wa Ulaya wa Uhispania Joseph Borrell Fontelles alisema hatua ya kujitolea wakati huu kumaliza ufisadi itasaidia sana kuleta imani miongoni mwa wawekezaji kote ulimwenguni.

Waziri huyo pia alimpongeza Rais Kenyatta kwa uamuzi wake wa Machi 9, 2018, wa kuafikiana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, hatua ambayo imeendelea kuhakikisha nchi hii inafurahia amani na uthabiti katika ukanda wa Afrika Mashariki linalokumbwa na misukosuko.

“Maafikiano yalikuwa kielelezo chema cha jinsi ya kusuluhisha mizozo ya ndani na hali ya kutoelewana,” akasema waziri Fontelles.

Kuhusu Ajenda Nne Kuu za Maendeleo za Serikali kuu ya maendeleo, Rais Kenyatta na waziri huyo walikubaliana kuchunguza jinsi nchi hizi zitakavyoshirikiana katika ujenzi wa nyumba za gharama ya chini kwa manufaa ya raia wa mapato ya chini.

Waziri huyo alisema Uhispania iko tayari kushiriki katika kufikiwa kwa lengo la ujenzi wa nyumba za ghama ya nchini kama mojawapo hatua za kuboresha maisha ya Wakenya.

“Tuko na kampuni nyingi ambazo zinaweza kuwa washirika wazuri katika ujenzi wa nyumba za gharama ya chini,” akasema Bw Fontelles.

Uhispania ina mfano mzuri wa mpango ambapo nyumba zinajengwa, kukarabatiwa na kununuliwa kwa mchango wa Serikali kupitia upunguzaji wa riba kwa kampuni zinazotoa mikopo.

Masharti

Nyumba zinazojengwa kupitia mpango huu unaotambulika (Ulinzi wa Nyumba za Umma) au ‘Vivienda de Proteccion Publica’ hutolewa kwa umma chini ya masharti ambapo wanaoishi katika nyumba hizo basi huzimilki, badala ya kuzikodisha.

Chini ya nguzo ya ujenzi wa nyumba za gharama ya chini, Kenya inakusudia kujenga nyumba 500,000 za gharama nafuu ifikapo mwaka wa 2022.

Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Masuala ya Kigeni Balozi Dkt Monica Juma, Naibu wa Msimamizi wa Wafanyakazi wa Ikulu anayehusika na Sera na Mikakati Bi Ruth Kaggia na Mkurugenzi wa Ulaya na Jumuiya ya Madola Balozi Jean Kimani.