Duale aunga mkono kuandaliwa kwa kura ya maamuzi
Na CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Aden Duale ameunga mkono mpango wa marekebisho ya Katiba kupitia kwa kura ya maamuzi chini ya mpango wa “Punguza Mzigo” unaomaanisha kupunguza mzigo kwa mlipa ushuru.
Akiongea bungeni Jumatano wakati wa mjadala kuhusu ripoti ya makadirio ya bajeti, Bw Duale amesema baadhi ya viti vitakavyofutuliwa mbali ni Wabunge Wawakilishi wa Wanawake katika Kaunti zote na Maseneta.
“Tayari sahihi zilizowasilishwa na Ekuru Aukot zinaendelea kukaguliwa na shughuli hiyo itakamilishwa hivi karibu. Nawahakikishia kuwa kura ya maamuzi itafanyika hivi karibuni na viti vya wawakilishi wa wanawake na maseneta viko hatarini. Hatutaki viti kama hivi ambavyo vinaongeza mzigo kwa wananchi ilhali havina maana yoyote,” akasema Duale.
Bw Duale amefichua kwamba amekuwa akifuatilia mchakato huo kwa makini kwa kuwasiliana na Bw Aukot ambaye ni kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance.
“Hata jana usiku (Jumanne usiku) nilikutana naye na akanihakikishia kuwa mambo ni shwari,” akaongeza.
Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini alibashiri kuwa mswada wa marekebisho ya katiba utapata uungwa mkono mkubwa bungeni utakapowasilishwa katika bunge la kitaifa baada ya kuwasilishwa katika mabunge ya kaunti.
Kudunisha
Kauli hiyo iliwakasirisha wawakilishi hao wa kike waliosema kuwa Bw Duale ni mmoja wa viongozi wanaume ambao wamekuwa wakidunisha hadhi yao katika bunge hilo.
“Mheshimiwa Spika, Duale anafaa kukoma kuwatisha na kuwadunisha wanawake kila mara ndani na nje ya bunge hili. Sisi pia ni viongozi ambao tumechaguliwa na Wakenya kuja kuwawakilisha katika bunge hili na tunahitaji heshima,” Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Lamu Bi Mohammed Obbo amefoka.
Wengine waliomkemea Bw Duale ni Bi Gladwell Cheruiyot (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Baringo) na mwenzake wa Murang’a Bi Sabina Chege.
Na kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo kiranja wa wengi Benjamin Washiali amesema kauli ya Bw Duale ni yake kama mtu binafsi na haiwakilisha msimamo wa uongozi wa Jubilee bungeni.
“Yale ambayo kiongozi wangu Bw Duale amesema ni maoni yake na ni haki yake kutoa kauli kama hizo. Lakini ningependa kukuhakikisha kuwa kura ya maamuzi haitafanyika mwaka huu au hivi karibuni kwa sababu shughuli hiyo haijatengewa pesa fedha katika bajeti itakatosomwa kesho ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020,” akasema Bw Washiali ambaye ni Mbunge wa Mumias Mashariki.
Mnamo Jumanne Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilisema tayari imekamilisha ukaguzi wa sahihi 500,000 miongoni mwa sahihi 1.4 milioni zilizowasilishwa na chama cha Thirdway Alliance.
Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema mchakato huo unaendelea vizuri ukiendeshwa na makarani 120 na wasimamizi 24.
“Tunatarajia kukamilisha mchakato huo katika majuma machache yajayo” akasema.
Baadhi ya wabunge wa ODM na wenzao wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa “Kieleweke” wamekuwa wakishinikiza mageuzi ya Katiba kupitia kura ya maamuzi ili kubadili mfumo wa uongozi.
Wanashikilia kuwa muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga hautakuwa na maana yoyote pasina kura ya maamuzi.