• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Hapa majitapo tu kuelekea fainali za Chapa Dimba

Hapa majitapo tu kuelekea fainali za Chapa Dimba

Na JOHN KIMWERE

WAVULANA wa South B United wanasisitiza kwamba bado hawajayeyusha tumaini la kutwaa ubingwa wa taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Two mwaka huu. South B United ambayo ndiyo bingwa wa kipute hicho katika Mkoa wa Nairobi imepania kumalizia shughuli zilipoachiwa na Gor Mahia Youth mwaka uliyopita.

Fainali za kitaifa za pambano hilo zitachezwa ijayo Uwanjani Kinoru Stadium, Kaunti ya Meru. South B United itakuwa kati ya timu nane za wavulana zitakazowakilisha maeneo nane kote nchini.

”Tunaendelea na mazoezi ili kujiweka pazuri kukabili wapinzani wetu kwenye michezo hiyo inayopigiwa chapuo kuzua ushindani wa aina yake mwaka huu,” kocha wa South B United, John Mandela anasema na kuongeza kuwa watashiriki mechi hizo huku wakilenga kushindana na kubeba kombe la kipute hicho.

Katika mpango mzima alidokeza kuwa kamwe hawawezi kupuuza wapinzani wao maana nao pia wamejipanga kuonyesha ujuzi wao kwenye michuano hiyo.

”Tunalenga kucheza kila mechi kama fainali hatutakuwa tunaenda kulaza damu maana timu zote zinaendelea kunoa makucha yazo ili kujiweka sawa kwa pambano hilo,” alisema na kuongeza kuwa ana imani tosha mechi za ufunguzi (robo fainali) hazitakuwa mteremko.

Wavulana wa South B United bingwa wa Chapa Dimba na Safaricom Season Two Mkoani Nairobi. Wiki ijayo wataelekea mjini Meru kuwakilisha Nairobi katika fainali za kitaifa zitakazopigiwa Kinoru Stadium, mjini humo. Picha/ John Kimwere

Naye kocha wa Berlin FC (Mkoa wa Kaskazini Mashariki), Ahmed Mohamed Hirmoge anasema ingawa ndiyo mwanzo kutinga fainali za kitaifa ana imani tosha ameandaa vijana wake vizuri kuvuruga matumaini ya wapinzani wao.

”Tumepania kutimiza mambo mawili kwenye kipute hicho, kutwaa tiketi ya fainali na kutwaa ubingwa wa kinyang’anyiro hicho la sivyo tumalize katika nafasi ya pili,” alisema.

Kulingana na droo ya mechi za robo fainali kwa wavulana, South B United (Nairobi) itafungua kampeni zake na Shimanzi Youth(Coast).

Bingwa wa Mkoa wa Magharibi, Lugari Blue Saints itacheza na Super Solico (Mashariki), Euronuts (Mkoa wa Kati) itaumana na Manyatta United (Nyanza), nayo Berlin FC (Kaskazini Mashariki) itakutanishwa na Al Ahly (Bonde la Ufa).

Kitengo cha wasichana fainali hizo zitashirikisha timu saba tofauti na wavulana baada ya Mkoa wa Kaskazini kukosa timu ya wasichana.

Mchezaji wa South B United, Wanjala Kepha (mbele) akizuia mpira kutoka kwa Kavaya Bramwel wa Jericho Allstars katika fainali ya Mkoa wa Nairobi kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Two. South B United ilishinda mabao 2-1. Picha/ John Kimwere

Acakoro Ladies (Nairobi) itapepetana na NCOED (Nyanza), Barcelona Ladies (Mkoa wa Kati) itatifua vumbi dhidi ya St Mary’s Ndovea (Mkoa wa Mashariki) huku Kitale (Bonde la Ufa) ikivaana na Archbishop Njenga (Mkoa wa Magharibi).

Nayo Changamwe Ladies (Coast) ilituzwa tiketi ya moja kwa moja kushiriki nusu fainali itakocheza na mshindi kati ya Acakoro Ladies na NCOED.

South B United ilifuzu kwa fainali za kitaifa baada ya kufunga Jericho Allstars mabao 2-1 katika fainali.

Kwenye nusu fainali za Mkoa wa Nairobi, South B United ilikomoa Uweza FC mabao 2-0 nayo Jericho Allstars ilitwaa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Brightstar Academy.

Kadhalika South B United ilifuzu kushiriki fainali za Mkoa wa Nairobi ilipobamiza Vapor Sports kwa mabao 5-4 kupitia mipigo ya matuta kwenye fainali za FKF Tawi la Nairobi West.

Gor Mahia Youth iliyotwaa ubingwa wa taji hilo Mkoani Nairobi ilibanduliwa kwenye nusu fainali za Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF) Tawi la Nairobi East.

Kwenye fainali za Mkoa wa Nairobi kwa warembo, Acakoro Ladies ililaza Carolina For Kibera mabao 5-4 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1.

Kwenye nusu fainali, Acakoro Ladies iliichoma County Queens kwa magoli 4-1 nayo Carolina For Kibera ilivuna mabao 4-3 mbele ya Dagorettti Mixed kupitia mipigo ya matuta.

Mkoa wa Kati, Barcelona Ladies ilivuna mabao 2-1 dhidi ya bingwa mtetezi, Limuru Starlets katika fainali. Barcelona ilifuzu kwa fainali ilipokomoa Kirinyaga Dynamo kwa mabao 4-1 nayo Limuru Starlets ilisajili bao 1-0 mbele ya JYSA.

Mchezaji wa South B United, Wanjala Kepha (mbele) akishindana na Kavaya Bramwel wa Jericho Allstars katika fainali ya Mkoa wa Nairobi kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Two. South B United ilishinda mabao 2-1. Picha/ John Kimwere

Nao wavulana wa Euronuts waliihifadhi ubingwa huo baada ya kubugiza Lufa Graduates kwa mabao 2-1.

Mkoa wa Mashariki, Super Solico ilinyakua tiketi ya fainali hizo ilipoibuka mabingwa kwa kulaza Isiolo Young Stars mabao 5-4 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Kwenye nusu fainali, Super Solico ya Mwingi iliiponda Samba FC ya Marsabit mabao 3-2.

Nao wasichana wa St Mary Ndovea Secondary walibeba mabao 2-1 mbele ya Chuka Starlets katika fainali iliyochezewa Kitui Show Ground mjini humo.

St Mary Ndovea ilinasa tiketi ya fainali za Mkoa huo  ilipokanyanga Sakuu Queens kwa mabao 3-0, nayo Chuka Starlets iliipepeta Karugwa Queens mabao 2-1.

Katika Mkoa wa Kaskazini Mashariki, vijana wa Berlin FC walirarua Al-Ansar kwa magoli 4-3 kupitia mikwanju ya penalti kwenye fainali iliyosakatiwa Uwanja wa Chuo cha Garissa mjini humo.

Timu itakayoibuka ya kwanza kwa wavulana na wasichana kila moja itatia mfukoni kitita cha Sh1 milioni kutoka kwa wafadhili wakuu wa kampuni mawasiliano ya Safaricom.

You can share this post!

Nataka kufurahia soka ya Ufaransa, asema Griezmann

Akasirisha hakimu kutaka dhamana ya Sh10,000 katika kashfa...

adminleo