• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
BIASHARA MASHINANI: Mchoraji mabango aliye na kipaji adimu

BIASHARA MASHINANI: Mchoraji mabango aliye na kipaji adimu

Na DUNCAN MWERE

NI watu wangapi duniani huishi kwa kutegemea vipaji vyao maishani?

Jibu: Ni wengi.

Kipaji chochote kinapochipuka kinafaa kuchochewa na kupaliliwa pasi na kudunishwa, kuzimwa wala kukejeliwa.

Hebu tafakari ni waja wangapi wanaovuna mabilioni ya pesa kutokana na vipawa vyao walivyojaaliwa na Rabuka mathalani michezo uwanjani, burudani jukwaani, sauti redioni na kwenye runinga au waandishi wa vitabu, magazeti au majarida na kadhalika?

Wapo wengi katika fani na tasnia nyingine. Akilimali ilifanya mahojiano ya kina na mchoraji mabango aliyebobea kwenye fani ya uchoraji na kuwa kati ya wachoraji mahiri kwenye jamhuri ya Kenya.

Vilevile ameweza kuvuna ghawazi lukuki. Fauka ya hayo amezuru katika maeneo mengi nchini na pia kupata mialiko maridhawa kutokana na kipaji chake adimu na adhimu.

Huyu si mwingine bali ni James Mwaniki kutoka mji wa Karatina eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri.

Mchoraji James Mwaniki akiwa kazini. Ametokea kuwa maarufu hasa maeneo ya Mlima Kenya kutokana na kazi safi na ubunifu wa hali ya juu. Picha/ Duncan Mwere

Kipawa chake kilijitokeza tangu akiwa shule ya msingi ya Ihwagi.

Hata hivyo, ndoto yake ya kuendeleza kipawa chake ilionekana kuzimika baada ya kukosa kuendelea na masomo yake katika Shule ya Upili ya Kiarithaini mjini Karatina. Hii ni kutokana na wazazi wake kukosa uwezo wa kumlipia karo akiwa kidato cha kwanza.

Akiwa Darasa la Sita alitumwa dukani kununua mafuta taa lakini pale mjini aliona mchoraji aliyekuwa na ubunifu wa aina yake, alikaa katika sehemu hii na kusahau alikuwa ametumwa.

“Nilimpata msanii akichora picha maridadi kwenye ukuta nikamwangalia akifanya kazi yake hapo nikasahau nilikuwa nimetumwa dukani, nilipogutuka maduka yalikuwa yamefungwa,” akumbuka Mwaniki. Alipofika nyumbani baba yake alimwadhibu kwa madai alikuwa mtovu wa nidhamu.

Bado akiwa Kidato cha Kwanza alianza kupata kibarua kwenye vijiji na mji wa Karatina. Kazi yake aliyofanya vyema ilikuwa ni kuchora mchoro ya mama akisukwa nywele katika saluni.

Wengi walimsifu na kuvutiwa na ubunifu wake wa hali ya juu. Akiwa na umri wa miaka ishirini na miwili pekee nyota yake kwenye taaluma hii ilizidi kufana na kung’aa kwani wengi walimfahamu kutokana na utunzi wake murwa.

Msanii huyu mwenye umri wa miaka 34 anaeleza kuwa alichochewa na mchoraji stadi kutoka kaunti ya Nyeri, Michael Karugu.

Fauka ya hayo Mwaniki aliyeasisi kampuni yake ya Mwaniki Arts and Designs alifichua kazi yake ya usanii imemvunia mengi wala hajuti kufuata sanaa ya uchoraji.

Kwanza inamkimu kimaisha bila usumbufu wowote.

Vilevile, kazi hii imemwezesha kununua kipande cha ardhi alichojenga kupitia kazi hii.

Aidha amenunua gari ambalo humwezesha kusafiri kwa haraka.

Asasi za elimu

Baadhi ya sehemu ambazo amekuwa akipata ajira ni taasisi za elimu, makanisani, hotelini na baa.

“Ni nadra nikose kazi kwani kila wakati huwa naibuka na mbinu za kisasa ambazo huwavutia wateja wangu katika maeneo mengi nchini,” asema. Ameweza kuzuru maeneo mengi nchini.

Mbali na kaunti ya Nyeri, Mwaniki ameweza kuzuru kaunti za Kirinyaga, Laikipia, Nandi, Mararal, Kiambu, Nyandarua na Nairobi. Kwa wiki Mwaniki huchora michoro ambayo hupatia takriban Sh35,000.

Mnamo mwaka wa 2010 Mwaniki alipata mwaliko katika kaunti ya Nandi kuchora picha ya aliyekuwa mkuu wa tarafa ya Mathira, baada ya kupata uhamisho.

Hata hivyo, Mwaniki anaeleza kuwa kazi yake haijakosa changamoto tele ila ana mbinu anazotumia kuepukana na haya. Mojawapo ni baadhi ya wateja wake kukosa kuwa waaminifu na kutomlipa kwa wakati.

Pili, gharama ya rangi anayotumia ni ghali kwani hawezi kununua mtungi mzima kutokana na kuharibika kwa urahisi isipotumika. Mwaniki ana mikakati ya kuasisi chuo cha kufunzo sanaa ambayo anaungama wadau wameifumbia macho.

You can share this post!

AKILIMALI: Weledi wa chipukizi wa 4K Club katika kilimo...

Wakulima wa majanichai Gatundu Kaskazini wataka malipo ya...

adminleo