Makala

Kutandika au kutotandika kitanda chako hukuangazia kwa msingi gani?

June 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

IPO dhana iliyojengeka eti kuamka asubuhi na utandike kitanda chako au chenu kunamaanisha una mpangilio mwema wa kimaisha.

Kumaanisha ukiwa mume unafaa uamke na utandike kitanda chenu cha ndoa, bali sio kumwachia mkeo akitandike kila siku.

Ikiwa utapata hilo likiwa suala gumu, muwe mnafanya hivyo kwa awamu au zamu.

Wengi wa wanaume hasa wale ambao hawajaoa watakiri kuwa kutandika kitanda ni kazi moja ambayo inaepukika kwa urahisi.

“Hakuna nyapara wa kuja kunichunguza hadi ninamolala chumbani. Nina umri wa miaka 39 kwa sasa na sijawahi kutandika kitanda changu. Mimi nikiamka huwa nawacha mashuka na blanketi jinsi mwili wangu uliyatoka, nikirejea usiku najiingiza na kutumia miguu na mikono kutandaza mashuka na blanketi. Upo wakati ninapata mashuka yalianguka chini lakini hiyo si hoja, hakuna maksi hupeanwa kwa watandikao vitanda vyao,” anasema James Mburu, mkazi wa Githurai 45.

Na kuna ukweli mwingi sana katika uwazi huu wa Bw Mburu; ukweli ambao ndio wengi wa wanaume wanaweza wakakiri wangekuwa tu na ujasiri.

Wanawake ni sawa na kawaida kutandika vitanda; jukumu ambalo hukua wakihamasishwa sana kulihusu na mama zao, wavulana wakiachiliwa kujipa uzooefu au kusahau jukumu hilo.

Katika utafiti wa 2017 nchini Amerika, raia 2,000 wakishirikishwa katika utafiti wa kuchambua suala hilo la kutandika vitanda na Shirika la OnePoll kuliibuka masuala kadha ambayo ni nyeti.

Watandikao vitanda vyao kila asubuhi bila kusahau au kuchoka walibainika kuwa ni wenye mtazamo wa kusonga mbele kimaisha, wana ujasiri, wanapenda kutangamana na wanajua kujitunza.

Nao wale ambao hawatandiki vitanda vyao walisemwa kuwa walibainika kuwa na haya, hukabwa na hisia mseto kimaisha na ambapo hujiangazia kama wa kukasirika na kufurahi bila mpangilio wowote, wana ile hamu ya kujua kuhusu kila kitu na pia hupenda sana kuongea kwa kinaya.

Ni hapa ambapo wasomaji wa Taifa Leo watajiuliza kama Douglas Mutua ambaye huandaa makala ya kinaya cha siasa kila Jumamosi ni mmoja wa wale ambao hawaheshimu jukumu la kutandika kitanda chake au chao yeye mwenyewe akiwa ndiye wa kuliwajibikia.

Wale ambao hupenda kutandika vitanda vyao walisemekana kuwa hawahitaji kukumbushwa kwa aina yoyote kwamba wakiamka asubuhi wana jukumu hilo muhimu kwa kuwa wana ile nidhamu ya kurauka mapema na kwa wakati ulio na mpangilio.

Pale utafiti huo ulibainisha mbivu na mbichi ni pale unasema kuwa walio na mazoea au mapenzi ya kutandika vitanda vyao huwa katika riziki za safu za teknolojia au afya, huku wale wasiotandika vitanda vyao wakiwa sanasana wapenda anasa ambao huingia kwa vitanda kama ni adhabu wanatii.

Na hao, wasiotandika, walisemwa katika utafiti huo kuwa wa riziki ndani ya nyanja za burudani, kifedha au ni wafanyabiashara.

Nchini Kenya, kuna wanasiasa wawili ambao kila wakati wakinafasika huwa wanaelezea jinsi walivyounda pesa zao kupitia biashara na wao ni Naibu Rais Dkt William Ruto na Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu.

Pengine itakuwa ni busara siku moja mmoja wa waandishi wa habari awaulize ikiwa wao ni wapenzi wa kutandika vitanda vyao. Pengine kwa kufanya hivyo ukweli utabainika kama ni kweli wafanyabiashara kwa mujibu wa utafiti huu hutandika vitanda vyao au la.

Afisa mstaafu katika kikosi kinachoogopewa cha kijeshi nchini Amerika cha Navy Admiral Seal, Bw William McCraven anasema kuwa kutandika kitanda chako kunaonyesha una nidhamu za kimsingi na unapenda mazingara safi ya pale wewe hulala.

McCraven hata ameandika kitabu kinachofahamika kama ‘Tandika kitanda chako: Masuala madogo ambayo yanaweza yakakugeuzia maisha yako au hata yageuze dunia’ (Make Your Bed: Little Things Can Change Your Life… And Maybe the World).

Maarifa ya busara

Katika hotuba moja kwa wanafunzi alisema kutandika kitanda ni mojawapo ya maarifa ya busara alipata katika kikosi hicho.

“Ukilifanya jukumu la kutandika kitanda chako kuwa mazoea ya kila uamkapo, utajihisi kuwa una mwanzo mwema wa siku, utajihisi mkamilifu na aliye na maringo kiasi na utajipata kutekeleza majukumu mengine ya siku ni sawa na kawaida na jioni utahesabu ufanisi mkuu wa kutekeleza majukumu,” akasema McCraven.

Anasema kuwa ikiwa siku yako itakuwa mbovu, utarejea kwa kitanda ambacho wewe mwenyewe ulikitandika ili kikupe tulizo, lakini ikiwa hukukitandika utaingia kwa masaibu mengine usiku kucha.

Lakini utafiti huo uliwiana kuwa kutandika au kutotandika kitanda chako sio kigezo cha kuamua ule usingizi utapata.

Kuna watakaolala usingizi wa pono kiwe kimetandikwa au la; hapa Waititu akikupa dokezi kuwa hata umkamate na umweke kwa seli hutaweza kumzimia raha ya kulala kwa kuwa “nitalala na ning’orote kwa kuwa mimi ni mtu wa kawaida.”