Wacheza kamari, walevi wafinywa
Na BENSON MATHEKA
WANAOPENDA kubashiri na kutabiri matokeo ya michezo wakilenga kushinda mamilioni ya pesa sasa watatozwa ushuru wa asilimia 10.
Wanaopenda starehe ya kunywa pombe kali na mvinyo nao itawabidhi kulipia pesa zaidi sawa na waraibu wa kuvuta sigara.
Maisha ya wahudumu wa bodaboda na tuktuk nayo yatakuwa magumu zaidi kwani polisi sasa wana sababu ya kuwahangaisha.
Hii ni baada ya Waziri wa Fedha, Henry Rotich kuagiza waanze kuchukua bima kwa ajili ya abiria wao na watu wengine iwapo watapata ajali.
Hatua hiyo inatarajiwa kulazimu wahudumu hao kuongeza nauli wanayolipisha abiria wao.
Ushuru wa magari yenye injini yenye uwezo wa zaidi ya 1500cc nao watalipia asilimia 5 zaidi ya ushuru wa sasa.
Kwenye taarifa ya bajeti aliyowasilisha bungeni Alhamisi, Waziri wa Fedha, Henry Rotich alisema serikali itakuwa ikitoza ushuru wa asilimia 10 kwa pesa zote zinazochezwa kwenye kamari.
Ikizingatiwa kuwa watu wengi wametekwa na uraibu wa kushiriki bahati nasibu nchini, serikali inatazamia kukusanya pesa nyingi kutokana na uchezaji kamari.
Hii inamaanisha kuwa ada za kushiriki kamari zitapanda, sawa na ushuru ambao wanaoshinda wanatozwa. Bw Rotich alisema hatua hii inalenga kukinga vijana kutokana na uraibu wa kucheza kamari ambao umeathiri maisha yao.
“Uchezaji wa kamari umekuwa na athari mbaya hasa kwa vijana. Ili kupunguza uraibu huu, ninaanzisha ushuru wa asilimia 10 kwa kila zawadi inayoshindaniwa,” alisema Bw Rotich.
Mwaka 2018, serikali ilianzisha ushuru wa asilimia 20 kwa kampuni za kamari kwa kila pesa zilizoshindwa.
Kwenye taarifa ya bajeti ya mwaka huu, Bw Rotich alisema ingawa sekta ya bodaboda imeajiri vijana wengi na inatumiwa na watu wengi kwa usafiri, kuna ongezeko la ajali ambazo zinaacha wengi na majeraha na hata ulemavu.
“Kuna haja ya kulinda abiria wa bodaboda dhidi ajali ambazo zimekuwa zikiongezeka, na kwa kufanya hivi watakuwa wakilipia abiria wao bima,” alisema Bw Rotich.
Kwa wanaopenda mvinyo na pombe na wavutaji wa sigara, Bw Rotich aliongeza ushuru kwa asilimia 15.
Bei ya chupa ya mvinyo ya mililita 750 itaongezeka kwa Sh18 nayo pakiti ya sigara 20 itaongezeka kwa Sh8.
Serikali pia iliongeza ushuru kwa bidhaa zinazosafirishwa kwa reli kutoka asilimia 1.5 hadi asilimia 2.
Inua jamii
Hata hivyo, alitengea mpango wa kusaidia wazee na wasiojiweza maarufu kama “Inua Jamii” Sh16.9 bilioni kutoka Sh12.2 bilioni zilizotengewa mpango huo mwaka 2018, mayatima na watoto wanaokabiliwa na hatari Sh7.9 bilioni na watu walio na ulemavu nao walitengewa Sh1.1 bilioni kupitia mpango huo.
Makundi ya vijana katika mitaa ya mabanda nao walitengewa Sh4.4 bilioni za kufadhili miradi ya kujiletea mapato huku hazina ya maendeleo ya vijana na hazina ya Uwezo zikitengewa Sh600 milioni na 400 milioni mtawalia.
Hazina ya wanawake pia ilitengewa Sh400 milioni.
Kulingana na Bw Rotich, pesa hizi zinalenga kusaidia vita dhidi ya umasikini, kuhakikisha usawa na kusaidia wasiojiweza katika jamii.