UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia za kujifunza lugha (Sehemu ya Tatu)
Na MARY WANGARI
Mbinu ya utambuzi (Communitive code method)
CHIMBUKO la nadharia hii ni ukosoaji, uhakiki au ukipenda udhaifu wa nadharia ya mbinu ya sarufi na ile ya moja kwa moja
Mbinu hii ilianzishwa mnamo 1970.
Waasisi wa nadharia hii wanadai kwamba ni bora mwanafunzi apewe vipengele vyote vya lugha kwa ujumla.
Hii itampa mwanafunzi maarifa mapana kuhusu lugha pamoja na kanuni za msingi kuhusu lugha husika.
Itamwezesha mwanafunzi kuielewa lugha kulingana na utambuzi wake binafsi.
Kulingana na nadharia hii, mkufunzi anapaswa kufundisha kanuni za msingi.
Kwa mfano, katika lugha ya Kiswahili, ni lazima ujue ngeli za majina.
Hii itakusaidia kutumia nomino katika mazingira tofautitofauti pamoja na vitenzi na kuwasaidia kueleza namna ambavyo vinaweza kukaa peke yake kama sentensi.
Mbinu ya mwitiko jumuishi (Total physical response)
Nadharia hii pia hujulikana kama mkabala asilia. Mwasisi wa nadharia hii ni James Asher (1969). Kipengele kinachotiliwa mkazo katika nadharia hii ni mfumo na muundo wa lugha.
Sawia na nadharia ya usikizi, nadharia hii pia inasisitiza umuhimu wa kumudu mazungumzo kama sehemu ya umilisi wa lugha.
Ufundishaji unapaswa uhusishe mazoezi ya kurudia rudia ambayo angalau unamfanya mwanafunzi kumudu anachojifunza
Nadharia hii inasisitiza matumizi ya vitendo na ishara mbalimbali kama nyenzo mojawapo katika kujifunza lugha.
Mbinu ya upendekezi (Suggestopidia method)
Nadharia hii iliasisiwa na msomi Lonzano Georgi (1979).
Mazingira bora ya mtu kujifunza lugha yanapatiwa kipaumbele katika nadharia hii kama nyenzo mojawapo muhimu katika kujifunza lugha.
Hii inamaanisha kwamba mazingira yanayotumika kujifunzia lugha ni lazima yamkumbushe mwanafunzi kile alichojifunza siku iliyotangulia.
Isitoshe, inagusia kuhusu namna ya mkao wakati wa kufundisha wanafunzi wageni. Mkao katika darasa uwe ni wa kutazamana kama vile kwa duara.
Sauti nyororo na laini bila muziki wa kelele.
Marejeo
Todd, L. (1987). An Introduction to Linguistics. Essex: Longman Group Limited.
TUKI (1990). Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Yule, G. (2010). The Study of Language (4th ed.). Cambridge: Cambridge University Press.