• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:20 PM
TAHARIRI: Tuwe macho kuhusu Ebola

TAHARIRI: Tuwe macho kuhusu Ebola

Na MHARIRI

TAARIFA kwamba ugonjwa hatari wa Ebola unazidi kusababisha maafa nchini Uganda ni za kutamausha hasa baada ya mtu wa pili kufariki Alhamisi.

Maafisa wa afya wanazidi kufanya kila wawezalo kuzuia kuenea kwake. Imethibitika kwamba aliyefariki ni nyanyake mvulana aliyefariki Jumatano kutokana na virusi vya ugonjwa huo uliosambaa kutoka taifa jirani la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Nyanya huyo alifariki usiku wa kuamkia jana katika Hospitali Kuu ya Bwera ambako kitengo maalum cha kuwatibu wagonjwa wa Ebola kilianzishwa baada ya mvulana huyo mwenye umri wa miaka mitano kufariki katika eneo la Kesese Magharibi mwa Uganda.

Thibitisho hili ni muhimu kwa matabibu wetu humu nchini kukaa ange ili kuzuia usambaaji wa Ebola.

Ugonjwa huu umeripotiwa nchini Uganda baada ya kusababisha vifo vya wengi DRC kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Juhudi za madaktari nchini Uganda ni za kuridhisha katika kukabili Ebola. Walifanya haraka kutenga watu waliofiwa ili kudhibiti maambukizi na pia kuwapa matibabu ya haraka.

Ili watu wasiendelee kuambukizwa ugonjwa huo hatari, serikali imepiga marufuku mikutano ya hadhara, zikiwemo siku za soko, mikutano ya maombi na hata siasa maeneo ya mpakani.

Msiba huu nchini Uganda hauko mbali sana na Kenya kutokana na mzunguko wa watu wakifanya biashara na safari nyinginezo kkati ya mataifa haya mawili.

La msingi hapa ni kwamba ni rahisi sana maambukizi hayo ya Ebola kuingia Kenya iwapo watu hawatawajibika na kujilinda dhidi ya maambukizi.

Maafisa wa afya hasa katika mpaka wa Busia na Malaba wawe macho kuhusu maambukizi ya Ebola kutoka Uganda. Ni wakati mwafaka serikali pia kuchunguza wanaoingia Kenya kutoka Uganda ili iwapo yeyote atapatikana na Ebola atengwe kwa ajili ya matibabu ya dharura.

Ebola imeua watu 1,300 nchini DRC, kwa hivyo ni ugonjwa unaohitaji umakinifu mkubwa katika kuudhibiti.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia za kujifunza lugha...

UCHAMBUZI: Viongozi waeleza ni kipi kinafaa kufanywa...

adminleo