• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
AHADI YANGU: Hazard aahidi kuiwajibikia Real Madrid ipasavyo

AHADI YANGU: Hazard aahidi kuiwajibikia Real Madrid ipasavyo

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

EDEN Hazard ameahidi Real Madrid na mashabiki wake mambo makubwa akisema anataka kuwa supastaa (Galactico) katika klabu hii yake mpya.

Hazard alitambulishwa mbele ya takriban mashabiki 50,000 uwanjani Santiagio Bernabeu mnamo Alhamisi baada ya uhamisho wake kutoka Chelsea uliosubiriwa kwa hamu kubwa, kuthibitishwa juma lililopita.

“Mimi si supastaa. Bado sijafika kiwango hicho, lakini natumai nitafika hapo siku moja,” alisema Hazard katika kikao na wanahabari baadaye.

“Licha ya kila kitu nilichofanya hapo awali, itakuwa sawa na kuanza maisha mapya hapa. Mimi si supastaa, mimi ni Eden Hazard, mchezaji mzuri tu.”

Madrid italipa Chelsea Sh11.4 bilioni kwanza halafu nyongeza ya Sh5.1 bilioni kwa mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 28 ambaye ametia wino kandarasi ya miaka mitano.

Hazard alikiri kwamba Madrid ilimvizia baada tu ya Kombe la Dunia mwaka wa 2018, lakini akasisitiza kwamba wakati huu ulikuwa mzuri wa kuondoka Chelsea.

“Sidhani nimechelewa, nimegonga umri wa miaka 28 ambao ni wakati mzuri kwa mchezaji yeyote,” alisema Hazard.

“Nimekuwa na vipindi tofauti katika maisha yangu, nikiwa Lille na Chelsea, na sasa nilihisi wakati umewadia mimi kujiunga na klabu nzuri kabisa duniani.

Madrid ilichechemea bila gunge Cristiano Ronaldo msimu uliopita na Hazard atakuwa na majukumu ya kujaza pengo la mchezaji huyo wa Ureno aliyejiunga na Juventus nchini Italia.

Licha ya kuwasili kwa Eder Militao, Luka Jovic na Ferland Mendy katika kipindi hiki cha uhamisho, Hazard ndiye mchezaji mkali zaidi aliyesajiliwa na Real tangu Zinedine Zidane arejee Bernabeu mwezi Machi.

“Unapochezea timu kama Real Madrid hakuna mtu mmoja utasema ni nyota kwa sababu timu yote imejaa nyota,” alisema Hazard.

“Nimekuwa Chelsea miaka saba, lakini sasa mimi ndiye mchezaji mpya katika timu hii na nitajaribu kuchangia kwa kiwango kikubwa niwezavyo.”

Alipoulizwa ikiwa anataka kuwa mwanasoka bora duniani akichezea Real Madrid, Hazard alisema, “Nitajaribu, lakini kwanza nitajaribu kuwa na mshikamano na timu hii bora duniani.

“Hiki ni kiwango tofauti. Nilipata mafanikio makubwa Chelsea na ninataka pia kushinda mataji zaidi hapa Madrid. Kuwa tu hapa, ni mtihani mpya.”

Hazard alikiri Zidane pia alikuwa kishawishi kikubwa katika uamuzi wake wa kujiunga na Madrid.

“Kila mtu anajua Zidane alikuwa shujaa wangu nikikuwa,” alisema.

“Yeye kuwa kocha ni kitu muhimu, ingawa si pekee yake alifanya nikuje hapa. Tayari nilitaka kuchezea klabu hii.

“Nilikuwa mtoto mdogo nikianza kucheza soka na ndugu zangu nilipoanza kushabikia Real Madrid.

“Kisha, nilienda Ufaransa halafu Uingereza, lakini kuwa mchezaji wa Real Madrid, kuvalia jezi hii, ni heshima kubwa. Nasubiri kwa hamu kubwa msimu kuanza.”

Nambari

Shati alilovalia Hazard mbele ya mashabiki halikuwa na nambari na alikiri kwamba alikuwa ameambia Mateo Kovacic akiwa Chelsea kuuliza raia mwenzake wa Croatia, Luka Modric, kuhusu jezi nambari 10.

“Nimepata kuzungumza na Modric kupitia kwa Kovacic na nilikuwa nikimtania tu nilipomuuliza aniazime jezi yake ya nambari 10,” alisema Hazard.

“Alisema, la, kwa hivyo itabidi nitafute nambari tofauti.”

Hazard alifungia Chelsea mabao 110 na kutajwa mchezaji bora wa mwaka nchini Uingereza mara nne.

Mashabiki wa Real watapata kuona Hazard akichezea klabu yake mpya katika mashindano ya kujiandaa kwa msimu mpya ya International Champions Cup. Miamba hawa wa Uhispania watalimana na mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich (Julai 21), Arsenal ya Unai Emery (Julai 24) na Atletico Madrid (Julai 27). Madrid pia itakutana na Tottenham Hotspur mnamo Julai 30 katika soka ya Audi.

You can share this post!

Wananchi kuumia zaidi bei ya mafuta ikipanda

Bajeti haramu?

adminleo