Bajeti haramu?
Na CHARLES WASONGA
UTATA umeandama bajeti iliyosomwa bungeni Alhamisi baada ya kuibuka kuwa Serikali ilikiuka agizo la Mahakama na kuiwasilisha kabla ya kupitisha Mswada wa Fedha 2019.
Isitoshe, mabunge yote mawili yalikosa kukubaliana kuhusu mswada muhimu wa ugavi wa pesa.
Mashirika ya Kijamii nchini, jana yalishikilia kuwa bajeti iliyosomwa bungeni na Waziri wa Fedha Henry Rotich ili kuwa haramu kwani haikufuata Katiba na kanuni zilizowekwa.
Hii ni licha ya mashirika hayo kushindwa kusitisha shughuli ya kusomwa kwa bajeti hiyo kupitia kesi waliyowasilisha katika Mahakama Kuu.
Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, wawakilishi wa mashirika manne ya kutetea haki na utawala bora walisema, bajeti hiyo haiwezi kukubalika kwa sababu iliwasilishwa kabla ya kupitishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Mapato kati ya Serikali Kuu na zile za Kaunti (DORB).
Hii ni baada ya wabunge na maseneta kukataa kukubaliana kuhusu kiasi cha fedha ambazo zinapasa kugawiwa serikali za kaunti hata baada ya kamati ya maridhiano kubuniwa na maspika Justin Muturi (Bunge la Kitaifa) na Kenneth Lusaka (Seneti).
“Tunawataka Wakenya kukataa bajeti iliyowasilishwa na Waziri Rotich kwa sababu inakiuka kipengee cha 202 (1) cha Katiba kinachosema kuwa sharti mswada wa ugavi wa mapato kati ya viwango viwili vya serikali upitishwe kwanza kabla ya makadirio ya bajeti kuwasilishwa,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la African Centre for Governance (AfriCoG) Bi Gladwel Otieno.
“Kwa hivyo, kusomwa kwa bajeti hii ni sawa na mapinduzi dhidi ya Katiba ambayo Wakenya walipitisha kwa kauli moja katika kura ya maamuzi mnamo Agosti 10, 2010,” akaongeza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Haki ya Kibinadamu Nchini (KHRC), George Kegoro, alisema kuwa hatua ya Waziri Rotich kusoma bajeti kabla ya kupatikana na maafikiano kuhusu ugavi wa pesa za kupelekwa kwa serikali za kaunti ni sawa na kuua ugatuzi.
“Tunashuku kuwa hii ni sehemu ya mpango wa serikali hii kuua ugatuzi. Kwa hivyo, tunawataka Wakenya kujitokeza na kuitetea ugatuzi na katiba ambayo waliipigania kwa zaidi ya miaka 20,” akasema akionekana kuwataka Wakenya kufanya maandamano.Wabunge wanapendekeza kuwa serikali 47 za kaunti zipate mgao wa Sh316 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 huku maseneta wakipendekeza serikali hizo zipewe Sh327 bilioni.
Muafaka
Kukosekana kwa muafaka kunamaanisha kuwa Spika Muturi ataamuru mswada mwingine wa ugavi wa mapato uandaliwe. Kwa hivyo, serikali za kaunti hazitaweza kuandaa bajeti zao kabla ya maafikiano kuhusu suala hilo kupatikana.
Maafikiano yakipatikana itabidi Bw Rotich kufanyia mageuzi ya bajeti za idara tofauti au hata kuongeza kiwango cha pesa ambacho ananuia kukopa kujaza pengo katika makadirio ya 2019/2020.
Mkurugenzi mkuu wa Taasisi wa Sera na Utatuzi wa Mizozo (ICPC) Ndungu Wainaina pia alitaja bajeti ya mwaka huu kuwa haramu akisema serikali haikuzingatia katiba, Kwenye taarifa, Bw Wainaina alisema serikali ya Rais Kenyatta inaendeleza mtindo wa kuangamiza serikali za mashinani.