Habari

Waliojisajili kuanza kupokea kadi za Huduma Namba mwezi Julai

June 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA na BENSON MATHEKA

WAKENYA na wageni waliojisajili wataanza kupokea Huduma Namba zao kuanzia Julai, Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru ametangaza.

Bw Mucheru alisema takriban watu 37.7 milioni, wenye umri wa miaka sita kwenda juu, waliojisajili watahitajika kuchukua nambari zao maalum kutoka kwa afisi ya machifu na manaibu wao katika maeneo walikosajiliwa.

“Baada ya mwezi mmoja kuanzia sasa serikali itaanza kupeana nambari maalum kwa wale wote waliojisajili. Na baadaye, watapewa kadi maalum za kieletroniki ambazo zitaweka pamoja maelezo yote yaliyoko katika kadi zilizotolewa na asasi nyingine za serikali,” akasema.

Bw Mucheru alisema hayo Alhamisi wakati wa ufunguzi rasmi wa Wiki ya Maonyesho ya Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

“Huduma Namba inalenga kuisaidia serikali kuimarisha utoaji huduma na kuhakikisha kuwa watu wanapata hudumu zinazofaa na kwa wakati ufaao,” Bw Mucheru alieleza.

Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na mawaziri George Magoha (Elimu) na mwenzake wa Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Kijamii Profesa Margaret Kobia.

Kwingineko duniani

Bw Mucheru aliongeza kuwa mpango wa usajili wa watu kwa Huduma Namba umetekelezwa katika mataifa mengine kama vile Amerika, Uingereza, Estonia na hata Ghana.

Usajili wa Huduma Namba ulianza mnamo Aprili 2 na kukamilika Mei 25 ambapo serikali ililenga kusajili jumla ya Wakenya 45 milioni humu nchini na katika mataifa ya nje.

Mitambo ya kieletroniki 31,500 ilitumika katika shughuli hiyo iliyoendeshwa na makarani 42,000 katika kaunti ndogo 8,500 kote nchini.

Hii ni licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya Wakenya walioshuku lengo la zoezi hilo.

Huduma hiyo ilitolewa bila malipo, kwa hiari, huku ikigharimu serikali Sh8 bilioni.

Mahakama ilisema shughuli hiyo inafaa kuwa ya hiari na kwamba hakuna Mkenya anayefaa kunyimwa huduma kwa kukosa kusajiliwa. Hii ilikuwa katika kesi iliyowasilishwa na mashirika ya kijamii yaliyodai kwamba kunyima Wakenya huduma ni kuwanyima haki zao.