Makala

SHERIA: Ndoa bila tendo la ndoa huzua doa

June 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA BENSON MATHEKA

Wasomaji wengi wameniuliza ikiwa ni kosa wanandoa kukosa kushiriki tendo la ndoa na ikiwa mtu anaweza kutalikiwa kwa kumnyima mchumba wake tendo hilo. Nimewahi kuangazia suala hili lakini kwa sababu safu hii ni ya kufaidi wasomaji, nitafafanua zaidi.

Ukioa na ukose kufanya tendo la ndoa na mkeo katika muda wa miezi mitatu, huwa haujatia muhuri ndoa yako na hiyo huwa sio ndoa tena. Hivi ndivyo inavyosema sheria ya ndoa ya Kenya.

Hili ni hitaji la kisheria lisiloweza kujadiliwa, ni lazima wanandoa watie muhuri ndoa yao kwa kulishana uroda katika miezi mitatu ya kwanza ya ndoa yao.

Kulingana na sheria, ndoa isiyoshirikisha tendo la ndoa katika kipindi cha miezi mitatu baada ya ndoa, huwa ni batili na inaweza kufutiliwa mbali na mahakama kwa msingi kuwa haijathibitishwa.

Hii inaonyesha sheria inatambua umuhimu wa tendo la ndoa. Hivyo basi haitoshi mtu kuchukua harusi pekee kama dhihirisho la ndoa.

Ni lazima mtu awe tayari kumtimizia mchumba wake mahitaji yake ya chumbani. Ni muhimu kukumbuka kuwa sheria inatilia mkazo mchango wa tendo la ndoa katika ndoa hivi kwamba inasema ni haki ambayo mtu hafai kumnyima mkewe au mumewe. Kuna ndoa nyingi zilizobatilishwa na mahakama kwa sababu ya wanandoa kukaushana kitandani.

Ningetaka kufafanua kuwa kubatilishwa kwa ndoa kwa sababu ya wanandoa kukosa kulishana uroda miezi mitatu baada ya kuoana sio sawa na talaka.

Hii ni kwa sababu tofauti na talaka, watu wakikosa kufanya mapenzi katika kipindi cha miezi mitatu baada ya harusi, yao haitambuliwi kama ndoa. Ndoa ni lazima ihusishe tendo la ndoa.

Hii inamaanisha nguzo kuu ya ndoa ni tendo la ndoa. Hata hivyo, haimaanishi mtu amlazimishe mchumba wake kumlisha uroda ikiwa hayuko tayari kufanya hivyo au kuna sababu za kutosha kuepuka tendo la ndoa.

Mtu anaweza kuugua ghafla punde tu baada ya kufunga harusi na katika hali hii mchumba wake anaweza kumwelewa na kumpa muda wa kupona.

Lakini ikiwa mtu hawezi kabisa kutekeleza tendo la ndoa, basi miezi mitatu inatosha mchumba wake kuchukua hatua ili ndoa hiyo itangazwe batili. Kwa hivyo, japo dini inasema kwamba watu wakioana hawafai kuachana hadi kifo kiwatenganishe, sheria ambayo inalinda aina zote za ndoa Kenya, iko wazi kuhusu suala hili.