Hofu ya Ebola Kenya
VITALIS KIMUTAI, CECIL ODONGO Na PETER MBURU
HOFU ilienea nchini jana watu wanne walipotengwa katika Hospitali ya Kericho Referral, baada ya mmoja wao kuonyesha dalili za ugonjwa hatari wa Ebola.
Habari hizo zilizua wasiwasi mjini Kericho na kuwafanya watu wengi kuhepa kuingia mjini.
Hii ni baada ya mwanamke aliyekuwa na dalili za Ebola kuwekwa kwenye wadi maalum mnamo Jumapili. Lakini matokeo ya awali ya uchunguzi yalionyesha hakuwa akiugua ugonjwa huo.
Kabla ya matokeo kutolewa, mumewe na jamaa wawili waliompeleka hospitalini pia walitengwa kwenye wadi maalum ingawa hawakuwa wameonyesha dalili zozote za kuugua Ebola.
“Tumechukua tahadhari kutokana na kisa kilichoshukiwa kuwa maambukizi ya Ebola, na tumewatenga watatu hao huku wakiendelea kufanyiwa uchunguzi,” akasema waziri wa afya wa Kaunti ya Kericho, Shadrack Mutai.
Shirika la Afya Duniani (WHO) pia liliwatuma wataalamu wa kimatibabu katika hospitali ya Kericho ili kusaidia kuchunguza iwapo kweli mgonjwa huyo alikuwa akiugua Ebola.
Mwanamke huyo aliyekuwa amesafiri kutoka mji wa Malaba, Kaunti ya Busia kwenye mpaka wa Kenya na Uganda, alilazwa katika hospitali ya Siloam mjini Kericho mnamo Jumapili, kabla ya kuhamishwa hadi hospitali ya Kericho Referral baada ya kuonyesha dalili za Ebola.
Chembechembe za damu za jamaa watatu wa mgonjwa huyo pia zilichukuliwa na kupelekwa kati maabara ya KEMRI.
Ebola ni ugonjwa hatari ambao uligunduliwa kwa mara ya kwanza mnamo 1976 kwa visa viwili Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Inaaminika popo ndio huwa na virusi vya Ebola, na binadamu anaweza kuambukizwa kwa kugusa damu, majimaji ya mwili ama viungo vya wanyama walioambukizwa kama nyani, popo, swara, nungunungu ama sokwe.
Mtu anayeugua anaweza kuambukiza mwingine endapo watagusana ama kugusa nguo ama sehemu ambayo imeathirika na virusi hivyo.
Dalili zake ni uchovu, kuumwa na misuli, kichwa na koo, kutapika, kuhara na kuvuja damu.
Kufuatia kisa kilichoripotiwa Kericho, serikali ya kaunti jirani ya Kisumu ilituma taarifa ikisema imetenga sehemu maalum katika hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga kushughulikia kisa chochote kitakachoshukiwa kuwa cha Ebola.
Ugonjwa huo tayari umewaua watu 1,400 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na mwishoni mwa wiki jana watu wawili waliripotiwa kufariki nchini Uganda. Pia kuna kisa kimoja kinachochunguzwa Somalia.
WHO imeonya kuhusu uwezekano wa Ebola kusambaa Afrika Mashariki kutokana na hali ya kuwa rahisi kuvuka mipaka kutoka taifa moja hadi lingine.
Hapo Jumatatu, Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki, alisema kisa cha mgonjwa aliyelazwa Kericho kiliripotiwa visivyo.
Bi Kariuki pia alisema serikali iko tayari kupambana na kisa chochote cha Ebola iwapo kitatokea nchini.
Alisema wizara yake imeimarisha ukaguzi katika mipaka yote ya Kenya na mataifa jirani.