• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
MATHEKA: Tutafute suluhisho la kuongezeka kwa mauaji

MATHEKA: Tutafute suluhisho la kuongezeka kwa mauaji

Na BENSON MATHEKA

WAKATI umefika Wakenya tusemezane ukweli kuhusu mauaji katika jamii ambayo yanaelekea kuwa janga katika nchi yetu.

Watu wanachinjana kwa sababu ya masuala ambayo yanapaswa kusuluhishwa kupitia mazungumzo au kwa kufuata mkondo wa kisheria wa kutafuta haki.

Si hayo tu, visa vya watu kujitoa uhai vimeongezeka sana katika jamii yetu.

Miili ya watu imekuwa ikipatikana imetupwa vichakani au hata kando ya njia baada ya kuuawa na watu wasiojulikana au katika hali ya kutatanisha.

Kisa cha Mildred Odira aliyeuawa baada ya kuondoka nyumbani kwa teksi kwenda hospitali mwaka jana ni kimoja cha vile vinavyoacha maswali mengi.

Hii ni baada ya polisi kutangaza kuwa wamegonga mwamba katika uchunguzi, kumaanisha kuwa waliomuua hawatapatikana na kuadhibiwa kulingana na sheria.

Katika hali hii, wahalifu wana uhuru wa kuendelea kutekeleza vitendo vya kumwaga damu bila kujali, na hivyo idadi ya vifo katika jamii inaongezeka nchini.

Huu ndio ukweli mchungu ambao umekuwa ukifanya umma kuchukua sheria mikononi na kuwaadhibu washukiwa wa mauaji, wakidai polisi wamekuwa wakizembea katika kazi yao kwa kutowachukulia hatua za kisheria.

Na umma unapochukua sheria mikononi, matokeo huwa ni idadi ya mauaji katika jamii kuongezeka. Ukweli mtupu ni kuwa kuna tatizo kubwa katika jamii ambalo limepuuzwa.

Tatizo lenyewe ni kupuuzwa kwa jamii yenyewe hivi kwamba watu wamepoteza matumaini maishani. Nasema hivi kwa sababu tafiti zimeonyesha kuwa kuna uhusiano kati ya hali ya uchumi na mauaji katika jamii hasa pale mtu anapoamua kuua familia yake.

Hali gumu ya maisha inayowakabili maskini imewafanya kuzongwa na mfadhaiko na kuchukua maamuzi yanayoacha huzuni tele kwa kuangamiza watu wa familia.

Inasikitisha kwamba serikali inaendelea kufanya maamuzi yanayoongezea maskini mzigo kama vile kuongeza viwango vya kodi.

Ninahisi kwamba serikali inayojali raia wa kawaida inapaswa kusitikishwa na ongezeko la mauaji katika jamii, na kuweka mikakati dhabiti kwa vitendo kukabiliana na hali hii kabla haijakuwa janga na kusababisha maafa makubwa.

Baadhi ya ripoti zimehusisha mauaji katika jamii na mmomonyoko wa maadili.

Ripoti hizo zinalaumu viongozi wa kidini kwa kutelekeza majukumu yao ya kushauri jamii huku wakifuata pesa. Huu ni ukweli ambao viongozi wa kidini wakiukumbatia unaweza kuwa suluhu la mauaji ya kutisha nchi.

Wakizingatia mafunzo ya dini yanayojenga umma kiroho badala ya kutoa mahubiri ya kuchochea hisia, wakizingatia mafunzo ya kujenga maadili katika jamii, nina hakika hali itabadilika na mauaji tunayoshuhudia kupungua.

Kukabiliana na hali hii kunahitaji mchango wa serikali kupitia sera zinazoweka mazingira bora ya uchumi ili kupunguzia umma gharama ya maisha, kuheshimu utawala wa sheria, mfumo wa elimu unaotilia maanani maadili na ushauri, kufanya raia kuwa na imani na mfumo wa haki na viongozi wa kidini kuzingatia mafunzo ya kujenga jamii kiroho na kimaadili.

You can share this post!

ODONGO: Tuwache lalama na tuunge Harambee Stars Afcon...

GWIJI WA WIKI: Geoffrey Nyaega Mogere

adminleo