• Nairobi
  • Last Updated March 18th, 2024 8:55 PM
NIKO TAYARI: Nipeni mikoba ya Chelsea – Lampard

NIKO TAYARI: Nipeni mikoba ya Chelsea – Lampard

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Frank Lampard atakubali haraka kufanya mazungumzo na Chelsea FC iwapo klabu hiyo ya Stamford Bridge itawasiliana rasmi na timu yake ya Derby County inayoshiriki ligi ya Daraja la Pili nchini hapa.

Lampard ambaye alichezea Chelsea kwa miaka 13 alikoacha rekodi ya kufunga mabao mengi, ameibukia kuwa kileleni mwa wanaopigania kutwaa nafasi ya kumrithi Maurizio Sarri aliyerejea nyumbani Italia kunoa miamba wa Serie A, Juventus.

Hata hivyo, ili kumpata nyota wao huyo wa zamani kujaza nafasi ya Sarri, lazima Chelsea ikubali kulipa Sh2.5 bilioni kumng’oa uwanjani Pride Park, kiasi ambacho hakiwezi kuwatatiza kutokana na ripoti kwamba watapokea Sh6.3 bilioni kutoka kwa Juventus kufuatia uhamisho wa Sarri.

Frank Lampard wakati akiichezea klabu ya Chelsea. Picha/ Maktaba

Ingawa kuna wale wanaomuona Lampard kama kocha asiye na ujuzi wa kutosha kunoa klabu ya hadhi kubwa kama Chelsea, kiungo huyo mstaafu amesema yuko tayari kutekeleza jukumu hilo.

Derby wamekuwa na uhusiano mwema na Lampard ambaye aliwaongoza hadi kutinga hatua ya mchujo wa kurudi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lakini wakabanduliwa na Aston Villa kwa 2-1 ugani Wembley, mwezi Mei.

Ushindi huo uliwawezesha Villa kurejea kwenye EPL kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016.

Chelsea haina kocha

Kwa sasa Chelsea haina kocha na tayari wakuu wake wangependelea kumpata Lampard ambaye anelewa falsafa ya klabu hiyo ya Kusini mwa jiji hili la London.

Mwenyekiti wa Derby, Mel Morris alisema wako tayari kufanya mazungumzo na Chelsea kuhusu kocha wao Lampard, huku akiongeza kuwa wangependa kiungo huyo mstaafu aendelee kuinoa Derby, na kuwa hata wako tayari kuurefusha mkataba wake.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini hapa, Lampard anaongoza orodha ya makocha wanaofikiriwa kumrithi Sarri aliyejaza pengo la Massiliano Allegri ambaye alipigwa kalamu na Juventus majuzi, licha ya kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Serie A kwa mara ya nne mfululizo.

Awali kulikuwa na habari kwamba kocha huyo, Allegri, ndiye aliyekuwa na nafasi kubwa ya kutwaa mikoba hiyo baada ya kuripotiwa kwamba anajifunza Kiingereza.

Makocha wengine wanaohusishwa na kazi hiyo ni pamoja na aliyekuwa kiungo mahiri wa Arsenal, Patrick Vieira, Diego Simeone wa Atletico Madrid na Nunu Espirito Santo aliyeongoza Wolves kumaliza ligi katika nafasi ya saba. Mbali na nafasi hiyo ya saba kwenye jedwali la EPL, kadhalika Nuno aliisaidia Wolves kutinga nusu-fainali ya Kombe la FA kabla ya kuzimwa na Watford ugani Wembley.

You can share this post!

Kuria: Mimi ni wa pili kwa umaarufu Kisumu baada ya Raila

Mashabiki wa Manchester United ndio watundu zaidi –...

adminleo