KINA CHA FIKIRA: Mafanikio ya Tume ya Kiswahili Afrika Mashariki
Na KEN WALIBORA
ABUBAKARI Zein ni mbunge wa Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki lenye wabunge kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Burundi na Rwanda.
Baadhi ya watu wanamjua tu ahlan wa sahalan.
Kwao ni mtu mwingine tu anayefanya hili na lile; mengine kumhusu hawana habari nayo. Hawajui kwamba aliibuka na riwaya ya Mbio za Sakafuni aliyoichapisha mwenyewe miaka ya mwishomwisho ya 1990.
Muhimu hapa ni kwamba yeye ni miongoni mwa waandishi wa Afrika Mashariki walioyavulia nguo maji ya Kiswahili na kuyaoga kwa ubunifu wao.
Kajichapishia mwenyewe na hili la kujichapishia lisiwe kigezo cha kupimia ubora wa ubunifu wake.
Watu wengi siku hizi wanajichapishia kazi zao, ingawa mimi sijafanya hivyo bado, labda baadaye. Ila leo naanza kutoa kauli yangu kwa kumtaja Abubakari Zein kwa hatua ya kihistoria aliyoichukua hivi karibuni katika utetezi wa lugha ya Kiswahili.
Mnamo Agosti 25, mwaka wa 2019 Zein aliwasilisha hoja katika bunge la Afrika Mashariki kulitaka likifanye Kiswahili lugha rasmi ya eneo hili. Hoja yake iliungwa mkono na wabunge Shyrose Bhanji na Abdullahi Mwinyi (wote wabunge wa Tanzania).
Katika hoja yake Zein alisisitiza kuwa Kiswahili ndiyo lugha inayokua na kuenea kwa kasi zaidi duniani na kwamba Muungano wa Afrika ulikwishaifanya lugha yake rasmi katika vikao vyake.
Ni mbunge anayewakilisha Uganda Mike Sebalu ndiye aliyependekeza marekebisho ya hoja na kukifanya Kiswahili mojawapo lugha rasmi, na wala si lugha rasmi ya pekee.
Vvyovyote viwavyo, historia iliandikishwa kwa wabunge wa bunge la Afrika Mashariki kupitisha azimio kwamba Kiswahili kiwe lugha mojawapo ya mawasiliano.
Hilo si dogo. Ni mafanikio makubwa kwa wakereketwa na wapenzi wa Kiswahili wa mbali na karibu na wa ndani na nje.
Azimio hilo ni tokeo la juhudi za wadau wengi wanaojulikana na wasiojulikana.
Waasisi wa shughuli hizi ni wazee kama vile Prof Chacha Nyaigoti Chacha aliyehudumu katika sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, mjini Arusha.
Waunda tume
Kutokana na juhudi zake Prof Chacha Nyaigoti Chacha na za wadau wengine hatimaye mataifa ya Afrika Mashariki yaliunda Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.
Tume hiyo iliyobuniwa 2015 (na ambayo Watanzania wanapenda kuiita Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki), inaongozwa kwa sasa na katibu mtendaji Prof Kenneth Inyani Simala.
Makao makuu ya tume ni Zanzibar.
Kwa sasa tume ina wafanyakazi wachache, na kama bunge la Afrika Mashariki lilivyotamka, ipo haja kuwaaajiri wengine.
Hili linamaanisha kwamba kila taifa mwananachama wa Jumuiya linawajibika kutoa fungu lake la kifedha bila kukawia ili kufadhili na kufanikisha utendaji wa Tume.
Kwa kweli baadhi ya nafasi za ajira zimetangazwa na kuna mikakati chungu nzima iliyopangwa na Tume kukuza Kiswahili ndani na nje ya shule na vyuo.
Mathalan tume imejitolea sabili kushirikiana na serikali na asasi mbalimbali zinazohusika katika kuboresha mitalaa ya masomo ya Kiswahili.
Tayari Tume imekwishashauriana na wawakilishi wa serikali, na asasi mbalimbali, vikiwemo vyombo vya habari ambavyo vina mchango mkubwa katika kueneza au kudumaza Kiswahili.
Katika Kongomano lililofanyika katika Taasisi ya Ukuzaji Mitalaa nchini Kenya (KICD) mapema mwaka huu, wajumbe kutoka Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Tanzania walipitia na kupitisha rasimu ya mpango-mkakati wa Tume wenye mustakabali bora sana kwa eneo zima.