HabariSiasa

AJIRA: Mwiba wa kujichoma unavyoitesa serikali

June 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

TANGAZO la Serikali mnamo Jumanne kuwa kuanzia Julai itaajiri wafanyikazi wake kwa kandarasi ili kubana matumizi yake, ni hatua nyingine kati ya nyingi zilizokosa kuzingatiwa awali.

Hii ni kutokana na kuwa juhudi zote za awali za kupunguza matumizi serikalini zimeshindwa, na gharama hiyo imekuwa ikipanda badala ya kushuka.

Kulingana na bajeti iliyosomwa bungeni wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Henry Rotich, serikali itatumia Sh790 bilioni kuwalipa mishahara watumishi wa serikali kati ya Julai 1 mwaka huu na Juni 30, 2020.

Ni kutokana na kiasi hicho kikubwa cha pesa ambapo Serikali imetangaza kuwa kuanzia Julai 1 itakuwa ikiwaajiri watumishi wa umma kwa kandarasi za miaka mitatu.

Lakini hii si mara ya kwanza kwa Serikali kutangaza mikakati ya kupunguza mzigo wa malipo ya wafanyikazi wake, ila jitihada hizo zote zimekuwa kazi bure.

Hii ni kutokana na kuwa viongozi wakuu wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta wamekuwa wakitenda kinyume cha sera za Serikali za kupunguza gharama za matumizi katika sekta ya umma.

Kuongezea mzigo

Mara baada ya kuchaguliwa kuhudumu muhula wa pili mnamo 2017, Rais Kenyatta alibuni wadhifa wa Waziri Msaidizi (CAS) akisema kuwa watasaidia kuboresha huduma katika wizara, licha ya kuwa kila wizara ina katibu (PS) na nyingine hata zaidi ya mmoja.

Wengi wa CAS hao ni wanasiasa waliokataliwa na wananchi kwenye uchaguzi mkuu wa 2017. Wadhifa huo umewaongezea Wakenya mzigo zaidi wa kuwalipa CAS hao 22 mishahara, marupurupu, magari, ofisi na wafanyikazi wanaowahudumia.

Mbali na kila mmoja kulipwa mshahara wa zaidi ya Sh700,000 kwa mwezi, CAS pia wanalipiwa bima ya matibabu ya zaidi ya Sh10 milioni.

Hatua nyingine ambayo imefanya sera za Serikali za kupunguza matumizi yake kuwa domo kaya ni kushindwa kuunganisha mashirika ya serikali kama ilivyokuwa imeshauriwa na jopo kazi lililoongozwa na Abdikadir Mohamed.

Mnamo 2013, Rais Kenyatta alibuni jopokazi hilo kutoa mwelekeo wa mageuzi katika mashirika ya umma.

Jopokazi hilo lilipendekeza mashirika ya umma yanayofanya kazi sawa yaunganishwe ili kuyapunguza kutoka 262 hadi 187.

Lakini hadi sasa serikali haijatekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo huku ikiendelea kulipa mamilioni ya fedha kwa wanachama wa bodi za mashirika yaliyostahili kuvunjwa.

Hawajui majukumu

Ripoti hiyo ya Abdikadir ilibaini kuwa wengi wa wajumbe wa bodi katika mashirika ya umma hawajui majukumu yao. Hii ni kutokana na kuwa wengi wa wanaopewa kazi hizo ni wanasiasa walioshindwa kwenye uchaguzi, washirika wa wanasiasa wakuu na jamaa zao ambao hawana ujuzi wa majukumu yao.

Hatua nyingine inayotilia shaka nia ya serikali kupunguza matumizi ni ile ya 2014 wakati Rais Kenyatta alipoagiza Wizara ya Ugatuzi kukagua watumishi wote wa serikali ya kitaifa ili kuondoa wafanyakazi hewa.

Rais alitoa agizo hilo baada ya kubainika kuwa Kenya inapoteza Sh1.8 bilioni kila mwaka kuwalipa mishahara wafanyakazi hewa. Mwishoni wa shughuli hiyo, serikali ilitangaza kufichua wafanyakazi hewa 12,500 katika sajili yake ya mishahara.

Wafanyakazi hewa

Akisoma bajeti wiki iliyopita, Bw Rotich alisema kuwepo kwa wafanyakazi hewa katika sajili ya mishahara ni miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha serikali kutumia mamilioni ya fedha kulipa mishahara, hivyo kumaanisha shughuli hiyo ya 2014 ilikuwa ya kupoteza wakati kwani wahusika hawakuondolewa.

Rais Kenyatta alipokuwa Waziri wa Fedha mnamo 2010, alipiga marufuku maafisa wa serikali kutumia magari yenye injini zilizozidi ukubwa wa 1800cc.

Agizo hilo limepuuzwa na serikali, kaunti na mashirika huku wengi wakiendesha magari makubwa yanayonunuliwa kwa bei ya juu, kutumia mafuta mengi na gharama za juu za kuyatengeza.