• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
ZARAA NA TALANTA: Mahindi yalimvutia njaa akaona akimbilie mboga na maharagwe

ZARAA NA TALANTA: Mahindi yalimvutia njaa akaona akimbilie mboga na maharagwe

Na CHRIS ADUNGO

STEPHEN Wanyonyi ni mkuzaji wa maharagwe na kunde katika sehemu ya Kibomet, Kitale.

Amekuwa akitegemea kilimo hiki kwa miaka 10 sasa na kulingana naye, kimemwezesha kujiajiri na kupata mapato mazuri tu.

Alianza rasmi kujihusisha na kilimo cha mahindi lakini baada ya muda, akapanua ukulima wake na kuingilia ukuzaji wa maharagwe na mboga za kiasili aina ya kunde.

Kilichomsababishia wazo hili ni namna alivyoona mahindi kwa kawaida yanakaa sana shambani bila kumpa hela za mara kwa mara.

Hivyo basi, ikambidi aongeze mahali pa kufanyia upanuzi wa kilimo cha maharagwe na kunde.

Wanyonyi mwenye umri wa miaka 37 sasa, huwa anapata mapato ya mara kwa mara kwani mimea hii huwa inachukua muda mfupi kukomaa na kuvunwa, tofauti na ilivyo kwa mahindi ambayo wakulima husubiri sana kwa zaidi ya miezi saba katika eneo hili.

Kulingana naye, kunde huwa zinahitaji muda wa hadi mwezi mmoja pekee kukomaa na mara moja, huwa anaanza kuzivuna na kuuza. Maharagwe huwa yanachukua muda wa miezi mitatu kukomaa.

Anasema kuwa kwa muda mrefu, shamba lake huwa linaendelea kustawisha mimea hii na jambo hili analionea fahari kwani hela anazozipata mara kwa mara huwa zinamwezesha kuikimu familia yake ya mke na watoto wanne.

Anaeleza kuwa kufanikiwa kwake katika kilimo hiki kunatokana na bidii zake za kila siku kwani ni lazima atunze mimea yake vyema kwa kila namna.

Anadokeza kuwa huwa ananunua mbegu za mimea hii zilizoidhinishwa katika shirika la Kenya Seeds, Kitale. Yeye huwa anajifanyia shughuli zote za kila aina kuanzia upanzi, kupalilia na hata kuvuna.

Anapovuna huuza mazao yake kwa wafanyabiashara wadogowadogo kwa wingi ambapo pia wao huenda kuuza katika maeneo mbalimbali ya Kibomet na Kitale mjini. Wakati mwingine, watu binafsi hujia bidhaa hizi shambani mwake.

Baadhi ya changamoto anazokumbana nazo ni pamoja na ukosefu wa mvua katika misimu ya kiangazi ambayo huwa inasababisha kukauka na kudhoofika kwa mimea.

Vilevile, mvua inaponyesha kwa wingi bei ya bidhaa hizi huteremka pakubwa kwa sababu ya ushindani kutoka kwa wakulima wengine wa mazao hayo.

Ufugaji

Wanyonyi anaelezea kuwa katika miaka ya hivi karibuni, ataingilia ufugaji wa ng’ombe kama njia ya kujinufaisha zaidi.

Ana imani kwamba ndoto hii yake itatimia kutokana na bidii ambazo ameweka kwa sasa na kulingana mapato ambayo amejipa kutokana na ukuzaji wa kunde.

Mwito wake kwa vijana na Wakenya kwa jumla ni wajitose kwa ukulima zaidi kwa ajili ya kupata chakula kwa wingi na bila shaka watavuna na kupata faida nyingi ambapo itakuwa ni manufaa kwa nchi nzima.

Anasimulia kuwa kilimo kinalipa na watu wakijituma kwenye shughuli hizi hatua kubwa nchini zitapigwa.

Japo yeye hukuza sana maharagwe aina ya Rose-Coco, anakiri kwamba yale aina za Samantha na Teresa huwa yanahitajika sana katika masoko, na kwa hivyo wakulima wengi hupanda aina hizi mbili hasa.

“Baada ya siku 90 hivi, mkulima anaweza kuanza kuvuna maharagwe maanake huwa hayachukui muda mrefu shambani kabla ya kukomaa,” anasimulia.

Katika msimu mzuri wa mavuno kulingana naye, mmea mmoja wa maharagwe una uwezo wa kutoa mazao ya hadi kilo mbili.

Kwa muda huu wa miezi mitatu, mavuno hupatikana kwa wingi kiasi cha kumwezesha kuvuna kati ya kilo 1,800 na 2,500 kila msimu.

Anasema wakulima wanahitaji mafunzo zaidi ili wajue mbinu za kisasa na za kiteknolojia za kufanya kilimo ili kupata mazao mengi.

Kulingana naye, wawekezaji wa nje wanastahili kuruhusiwa wawekeze kwa viwanda vya kuongezea thamani ya maharagwe na kunde, kisha kuuza katika masoko ya kigeni.

You can share this post!

AKILIMALI: Amepata tuzo mbalimbali kwa ufugaji bora wa mbuzi

Wakazi Laikipia Kaskazini walia wawekezaji, wakulima...

adminleo