Habari

Wakazi Laikipia Kaskazini walia wawekezaji, wakulima wanabadili mikondo ya mito

June 20th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa Laikipia Kaskazini wameiomba serikali kuweka sheria kali zitakazonusuru mito iliyoko eneo hilo.

Wanalalamika kwamba maji kwenye mito eneo hilo hutiririka msimu wa mvua pekee, kwa sababu ya kampuni na mashirika yanayofanya kilimo na ambayo hubadilisha mikondo yake wakati wa kiangazi.

“Kitambo wakati wa kiangazi mito ilikuwa na maji, haingekauka. Kwa sasa maji kwenye mito hutiririka msimu wa mvua pekee. Sababu ni moja tu; kuna kampuni na mashirika ya kilimo yanayomilikiwa na raia wa kigeni, mikondo ya maji wameielekeza katika mashamba yao,” analalamika mkazi wa eneo la Mukima na linaloonekana kuathirika pakubwa.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, wenyeji hao walidai mkulima wa kiwango cha chini ndiye anaendelea kuumia na kusababisha Laikipia kuwa mojawapo ya kaunti zinazopokea chakula cha msaada kila mwaka.

Chanzo cha maji ya mito hiyo ni Mlima Kenya, na wanaonya kwamba sheria maalum zisipowekwa kudhibiti ubadilishaji wa mikondo kiholela huenda wakakosa kufanya kilimo.

Aidha, wanateta kuwa ni jambo la kuhuzunisha kuona wanategemea maji ya mvua ilhali wana mito ambayo inaweza kuwafadhili maji hata msimu wa kiangazi.

“Hufanya upanzi mvua inyeapo, kiangazi kinapobisha hodi mito inakauka kwa ajili ya maji kutekwa na mikondo kubadilishwa na ‘wakulima wakubwa’. Kilele ni mimea yetu shambani kunyauka,” wakalalamika.

Licha ya kuwa msimu wa mvua kubwa, Mto Onterere na ambao kiini chake ni Mlima Kenya unaonekana kuwa na maji kidogo ukilinganishwa na mingine eneo la Kati inayotegemea mlima huo.

John Muthee ni mkulima na anasema ni kutokana na changamoto wanazopitia, amelazimika kukuza mimea inayozalisha kwa muda mfupi.

“Shamba langu na mengine ya kukodi, nimeligeuza uga wa Maharagwe ya Kifaransa ambayo huvunwa baada ya siku 45 au miezi miwili. La mno, hutegemea mvua, na mto unapokauka mashamba yanasalia mahame,” akasema Bw Muthee.

Kilio chao kwa viongozi humo wanasema kimeambulia patupu, mabwanyenye wanaofanya kilimo wakiendelea kuwanyanyasa kwa kufunga maliasili hiyo muhimu. Laikipia pia ni tajika katika ufugaji, na wanyama wao huhangaika kwa kukosa maji wakati wa ukame.