AFCON: Timu zitaumiza nyasi katika viwanja hivi
Na GEOFFREY ANENE
MABINGWA mara saba Misri watatumia viwanja saba vya kimataifa kuandaa Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019
Uwanja mkubwa wa Misri, ambayo iliandaa makala ya pili mwaka 1957, 1974, 1986 na 2006, ni Cairo International unaobeba mashabiki 74,100. Mechi tano kati ya sita za Kundi A linalojumuisha Misri, Uganda, DR Congo na Zimbabwe, zitachezewa humu.
Mechi za Kundi C, ambalo linaleta pamoja Senegal, Algeria, Kenya na Tanzania, zitasakatiwa uwanjani 30 June ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 30,000.
Mechi zote za makundi za Kenya na Senegal zitachezewa humu, pamoja na ile ya Kundi A kati ya Zimbabwe na DR Congo na pia mchuano wa Kundi D kati ya Namibia na Ivory Coast.
Uwanjani wa Al Salaam jijini Cairo unaobeba mashabiki 30,000, utatumiwa kwa mechi za Kundi Kundi D (Ivory Coast, Morocco, Afrika Kusini na Namibia) pamoja na mechi inayokutanisha Tanzania na Algeria.
Suez Stadium ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 27,000 utatumika kwa mechi za Kundi E linaloleta pamoja Tunisia, Mali, Mauritania na Angola pamoja na ile ya Kundi F kati ya Guinea-Bissau na Ghana.
Uwanja wa Alexandria mjini Alexandria utakuwa makao ya mechi za Kundi B (Nigeria, Guinea, Madagascar, Burundi). Unabeba mashabiki 20,000.
Uwanja wa mwisho utakaochezewa mechi za AFCON mwaka huu ni Ismailia. Unabeba mashabiki 18,525. Mechi zote za makundi za Cameroon zitasakatiwa humu pamoja na ile ya Kundi E inayokutanisha Angola na Mali. Cameroon iko katika Kundi F pamoja na Ghana, Benin na Guinea-Bissau.
Viwanja hivi saba vitaandaa mechi mbalimbali za raundi ya 16-bora kati ya Julai 5 na Julai 7, huku viwanja vya 30 June, Al Salam, Suez na Cairo International vikitumiwa kwa mechi za robo-fainali mnamo Julai 10 na Julai 11.
Uwanja wa 30 June utaandaa nusu-fainali moja nao Cairo International nusu-fainali nyingine. Nusu-fainali ni Julai 14.
Fainali itakuwa Cairo International hapo Julai 19. Kabla ya fainali, mechi ya kutafuta nambari tatu itachezewa uwanjani Al Salaam mnamo Julai 17.
Ni mara ya kwanza Kenya inashirii AFCON nchini Misri. Ilishiriki makala ya mwaka 1972 (Cameroon), 1988 (Morocco), 1990 (Algeria), 1992 (Senegal) na 2004 (Tunisia).