AFCON: Mamilioni yatakayong'ang'aniwa na timu 24
Na GEOFFREY ANENE
KENYA itajizolea tuzo ya Sh458.5 milioni ikiwa Harambee Stars itafaulu kutwaa ubingwa wa kindumbwendumbwe cha Kombe la Afrika (AFCON) kitakachoandaliwa nchini Misri mnamo Juni 21 hadi Julai 19, 2019.
Vijana wa kocha Sebastien Migne wako katika Kundi C, ambalo liko na Teranga Lions ya Senegal, Desert Foxes ya Algeria na Taifa Stars ya Tanzania. Ni kundi ngumu.
Senegal anayochezea Sadio Mane na Algeria ya Riyad Mahrez zinazopigiwa upatu kunyakua tiketi mbili za moja kwa moja za kusonga mbele zinashikilia nafasi ya 22 na 68 duniani.
Kenya inayojivunia kuwa na kiungo wa Tottenham Hotspur Victor Wanyama, iko katika nafasi ya 105 nayo Tanzania anayochezea Mbwana Samatta ni ya 131.
Kenya ilishiriki makala ya mwaka 1972 (Cameroon), 1988 (Morocco), 1990 (Algeria), 1992 (Senegal) na 2004 (Tunisia).
Haikutoka makundi. Inamaanisha kwamba ili kupata tuzo hiyo ya juu kabisa, Kenya itahitajika kuanza na kufanya miujiza kwanza ya katika mechi dhidi ya Algeria (Juni 23), Tanzania (Juni 27) na Senegal (Julai) mbali na kufagilia mbali wapinzani wengine katika awamu ya 16-bora, robo-fainali, nusu-fainali na kisha, fainali.
Kwa kufuzu pekee kurejea katika AFCON baada ya kukosa makala saba yaliyopita, Kenya ilijihakikishia tuzo ya Sh48.4 milioni. Hii ni kando na Sh26.4 milioni ambazo Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) lilitarajiwa kuzipa timu zote 24 zinazoshiriki makala ya mwaka huu kufanikisha maandalizi yao.
MGAO WA TUZO (AFCON 2019)
Mabingwa: Sh458.5 milioni
Nambari mbili: Sh254.7 milioni
Nambari tatu: Sh203.8 milioni
Nambari nne: Sh203.8 milioni
Robo-fainali: Sh81.5 milioni
Nambari 3 kwa makundi: Sh58.5 milioni
Nambari 4 kwa makundi: Sh48.4 milioni
MAKUNDI
Kundi A: Egypt, DR Congo, Uganda, Zimbabwe
Kundi B: Nigeria, Guinea, Madagascar, Burundi
Kundi C: Senegal, Algeria, Kenya, Tanzania
Kundi D: Morocco, Ivory Coast, South Africa, Namibia
Kundi E: Tunisia, Mali, Mauritania, Angola
Kundi F: Cameroon, Ghana, Benin, Guinea-Bissau