• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
AKILIMALI: Mbegu mpya za viazi kuwafaa wakulima

AKILIMALI: Mbegu mpya za viazi kuwafaa wakulima

NA RICHARD MAOSI

WAKULIMA wengi eneo la Bonde la Ufa wanafahamu tija inayotokana na upanzi wa viazi kwa kutumia mbegu halali zilizoidhinishwa na serikali kuu.

Mbali na mazingira kuwa mwafaka, mvua ya kutosha na rutuba tele,ili viazi vinawiri mkulima aepuke kupanda viazi kwenye udongo unaofanya maji kutuama.Uchachu wa asidi unaokolea mchangani unaweza kufanya mimea inyauke.

Ndiposa serikali ya Kenya kupitia wizara ya kilimo,kwa ushirikiano na KEPHIS (Kenya Plant Health Inspectorate Service) waliona haja ya kukagua mbegu kwanza, kabla ya kuzisambaza kwa wakulima mashinani.

Aidha KEPHIS walifanya uchunguzi wa maabara , na kuweka kanuni kali kwa mbegu zinazozalishwa na wafanyibiashara wasiofikia kiwango cha ubora,katika harakati za kukabiliana na matapeli wa kuuza mbegu waliofurika sokoni.

Shamba la Ol-Rongai lililoandaliwa tayari kwa upanzi wa viazi vya kigeni, Kaunti ya Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Mojawapo ya kampuni zilizopiga hatua kubwa katika operesheni ya kusambazia wakulima mbegu bora ni Agrico EA,inayopatikana katika eneo la Ol-Rongai, Kaunti ya Nakuru.

Kazi ya Agrico EA ni kuagiza mbegu za aina mbalimbali ya viazi,kuzikuza katika shamba la Ol -Rongai na kuwauzia wakulima kama mbegu kwa bei nafuu.

Aidha, hutoa ushauri kuhusu utaratibu wa kufuata wakati wa kupanda,viazi kwa kuzingatia kanuni zote.

Agrico EA imefanikiwa kuwasaidia wakulima wadogo kuwekeza katika kilimo cha ukuzaji wa viazi kutokana mbegu za kigeni, ambazo huchukua kati ya siku 90-120 kukomaa.

Aina hii ya viazi hukua kwa kasi. Picha/ Richard Maosi

Maeneo kame kama vile Kajiado,Turkana na Samburu hatimaye yameanza kupata mashiko , huku wakulima wengi wakiacha ufugaji wa ng’ombe na kugeukia kilimo.

Akizungumza na Akilimali,meneja wa uzalishaji Willem Dolleman Junior anasema,ukuzaji wa viazi una faida nyingi endapo mkulima atafuata utaratibu wa kitaalamu.

Anasema kampuni ya Agrico EA iliagiza aina 12 ya mbegu za viazi, kutoka nchini Uholanzi na kufanyia majaribio humu nchini katika shamba la Ol-Rongai kabla ya kuzisambaza kwa wakulima.

Maeneo yaliyolengwa ni Solai,Lanet,Nyahururu,Gilgil na Naivasha.

“Ikumbukwe nchi ya Uholanzi inaongoza kote ulimwenguni katika uzalishaji wa spishi za viazi zinazochukua miezi mitatu hivi kukomaa,” akasema.

Mimea ya viazi inavyonawiri kwenye rutuba. Picha/ Richard Maosi

Alieleza kuwa kilo 800 ndizo zinahitajika kupandwa katika kila ekari,ambapo kati ya tani 12-16 huvunwa na zinaweza kumpatia mkulima zaidi ya milioni moja akiondoa gharama zote za matumizi kama vibarua,mbolea na usafirishaji.

“Bei ya viazi huwa ni nzuri hata wakati mwingine gunia moja hufika 10,000.Gunia moja ya viazi ina uzani wa kilo 100,hii inamaanisha kuwa mkulima anaweza kupata hadi milioni 1.6 kila msimu wa upanzi, “Willem alisema.

Willem akisema kuna wakulima wanaopanda misimu mitatu kwa mwaka,na faida wanayopata haina kifani.

Kulingana na mtaalam wa kilimo Athanasious Kaituyu msimamizi wa shughuli za upanzi kwenye shamba la Ol-Rongai, ambaye anawahimiza wakulima kuhakikisha wananunua mbegu zilizoidhinishwa na serikali.

Anasema ingawa mbegu hizo ni ghali mazao yake ni mazuri na yatamridhisha mkulima wakati wa kuvuna.

Athanasious Kaituyu akionyesha aina za viazi vinavyokuzwa Ol-Rongai ambavyo huchukua muda mfupi kukomaa. Picha/ Richard Maosi

Alitoa mfano wa spishi inayofahamika kama Manitou ambayo huchukua siku 90 kabla ya kukomaa.Ni aina ya mbegu iliyo na uwezo wa kukabiliana na hali mbaya ya anga kama vile ukame pamoja na vidudu .

Anasema mkulima anaweza kuanzisha mradi wake hata akiwa na mtaji kidogo muradi awe na mbegu zinazostahili.

Kwanza anasema kabla ya kuzipanda, mkulima ahakikishe anazihifadhi mbegu zake katika sehemu iliyo salama mbali na kemikali za aina yoyote.

Pili ahakikishe zimefunikwa vizuri wakati wa usafirishaji ili zisije zikaota mizizi na kumea kabla ya kuzipanda katika kipande cha ardhi.

Ikiwezekana mkulima anaweza kutumia masine ili kuhakikisha hatua zote zinazingatiwa kuanzia hatua ya kupanda,kukabiliana na magugu na hatimaye kuvuna.

Anahimiza umuhimu wa kutumia mitambo kwa sababu husaidia kutunza saa na hupunguza gharama ya kuajiri vibarua.

Mashine hii hutumika mtambo unaotumika kuandaa shamba, kuchimba mashimo, kupanda na kung’oa magugu. Picha/ Richard Maosi

Kaituyu anasema kwanza mkulima anaweza kuchunguza aina ya udongo ili wadudu waharibifu wasipate maficho ya kuzaana.

“Mbegu huwekwa ndani ya mchanga katika mitaro iliyochimbwa vizuri na masine kisha kupitia mfumo wa planter mbegu moja moja huangushwa ndani ya kila shimo,” Kaituyu alisema.

Anasema mchanga unafaa kuinuliwa na kufanya uwe matuta ili kuwezesha mimea ifikiwe na miale ya jua kwa wakati mzuri.Pia humsaidia mkulima kung’oa magugu yanayoweza kuchipuka bila kuharibu mimea.

Anawakumbusha wakulima wasiweke mbegu kwenye mashimo ya kina kirefu kwa sababu mizizi ya viazi humea karibu na ardhi.

Anawahimiza wakulima kwa upande mwingine, wasitegemee maji ya mvua na badala yake watumie unyunyizaji wa kila mara ili matawi ya viazi yasije yakakauka kutokana na joto kali.

You can share this post!

AKILIMALI: Biashara ya vyungu na miche ina hela kama...

Aelezea sababu ya kujifanya muuguzi wa kike tangu 2009

adminleo