• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
AFCON: Jiandaeni kwa kipute cha joto kali Misri – CAF

AFCON: Jiandaeni kwa kipute cha joto kali Misri – CAF

Na GEOFFREY ANENE

KENYA pamoja na mataifa 23 yatakayoshiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 yameonywa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kwa yajiandae kwa mashindano yatakayochezewa kwa joto kali.

Taarifa kutoka nchini Misri ambako mashindano haya yataandaliwa kutoka Juni 21 hadi Julai 19 zinasema kwamba Kamati ya mashindano inayojihusisha na masuala ya afya kwenye CAF imeitisha mapumziko ya lazima ya dakika tatu baada ya dakika 30 za kwanza na pia itakapogonga dakika ya 75, mbali na yale ya kawaida ya dakika 15 kipindi cha kwanza kinapokatika.

Mashindano haya makubwa barani Afrika yalihamishwa kutoka tarehe zake za kawaida za Januari/Februari hadi Juni/Julai kwa mara ya kwanza kutokana na mivutano kati ya klabu na nchi. Hali ya joto nchini Misri wakati huu inatarajiwa kufikia kati ya nyuzi joto 35 na 38.

Kiwango cha unyevu angani pia kitakuwa kati ya asilimia 40 hadi 60. “Ni muhimu timu zote zizingatie onyo hii pia wakati zinafanya mazoezi,” taarifa kutoka CAF ilisema jana.

“Katika kiwango hiki, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) linashauri mechi kusimamishwa kwa dakika tatu ifikapo dakika ya 30 na dakika ya 75.” Wachezaji na maafisa watapewa vinywaji vilivyowekwa kwenye masanduku ya barafu iliyosagwa. Pia, watapokea taulo baridi.

Huku mataifa kama Algeria, Uganda, Zimbabwe na Tanzania yakifanyia mazoezi yao katika mataifa ya Qatar, Milki za Kiarabu, Misri na Misri mtawalia, Kenya ilijiandaa katika kibaridi jijini Paris nchini Ufaransa kutoka Mei 31 hadi Juni 17 kabla ya kutua jijini Cairo mnamo Juni 18.

You can share this post!

DPP akosolewa kumfungulia mashtaka wakili Nyakundi

AFCON: Mataifa yaliyojipanga kwa mtanange Vs yale...

adminleo