NUKSI TWAIKATAA: Stars yalenga kuondoa ‘swara’ Afcon
Na GEOFFREY ANENE NA MASHIRIKA
HARAMBEE Stars itatumai kumaliza msururu wa ‘swara’ kwenye Kombe la Afrika (AFCON) itakapofungua kampeni yake dhidi ya Algeria mnamo Jumapili jijini Cairo nchini Misri.
Kenya, ambayo ina hamu kubwa ya kupata ufanisi wakati huu, imesakata mechi 14 katika makala tano ya AFCON na kushinda mechi moja pekee. Ilichapa Burkina Faso mabao 3-0 mwaka 2004 nchini Tunisia.
katika kombe hili baada ya kukosa makala saba yaliyopita.
Mabingwa hawa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) watahitaji ghera maradufu kutokana na hali kwamba wako katika kundi gumu linalojumuisha Senegal na Algeria, ambao wanapigiwa upatu kusonga mbele, na Tanzania.
Kenya, ambayo haijawahi kupita hatua ya makundi katika AFCON, itaongozwa na viungo Victor Wanyama na Ayub Timbe pamoja na mshambuliaji Michael Olunga.
Itakosa huduma za beki Brian Mandela, ambaye aliumia goti katika mechi ya kirafiki dhidi ya Madagascar na kufanyiwa upasuaji nchini Ufaransa.
Mmoja wa mabeki watakaotegemewa na Kenya sasa ni Joash Onyango wa Gor Mahia.
Katika mechi zilizoratibiwa kusakatwa leo Jumamosi, Uganda watapambana na majirani DR Congo katika Kundi A.
Congo inapigiwa upatu kuzoa alama tatu dhidi ya Cranes.
Hata hivyo, DR Congo, ambayo inaorodheshwa ya 49 duniani, italazimika kutia bidii zaidi hasa baada ya kuambulia ushindi mmoja katika mechi nane zilizopita.
Nyingi ya mechi hizo zilimalizika kwa sare ikiwa ni pamoja na 1-1 dhidi ya Kenya katika mechi ya mwisho ya kujipima nguvu kabla ya AFCON hii.
Mechi saba kati ya 13 za mwisho za mabingwa wa mwaka 1968 na 1974 DR Congo kwenye AFCON pia zimekuwa sare.
Uganda, ambayo inashikilia nafasi ya 80 duniani, inafukuzia ushindi wake wa kwanza baada ya kurejea katika AFCON mwaka 2017.
Ilichapwa 1-0 na Misri na Ghana katika mechi za makundi za makala iliyopita na kugawana alama dhidi ya Mali katika mechi iliyotamatika 1-1.
Baadhi ya wachezaji wanaoweza kuamua mwelekeo wa mechi hii ni Tresor Mputu na Cedric Bakambu (DR Congo) na Mganda Emmanuel Okwi.
Mabingwa wa mwaka 2013, Nigeria wataanza kampeni yao dhidi ya washiriki wapya kabisa Burundi katika mech ya kwanza ya Kundi B.
Super Eagles, ambayo ilikosa makala ya 2015 na 2017, itakuwa mawindoni kumaliza msururu wa matokeo duni baada ya kutoka 0-0 na Zimbabwe na kulimwa 1-0 na Senegal kabla ya AFCON.
Matokeo ya mechi hii huenda yakaamuliwa na washambuliaji Ahmed Musa (Nigeria) na Cedric Amissi (Burundi).
Amissi ameona lango katika mechi nne kati ya tano zilizopita. Washiriki wengine wapya kabisa Madagascar pia wako katika kundi hili. Watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Guinea ambayo ina uzoefu wa kushiriki Afcon mara 11 ikiwemo kufika robo-fainali mwaka 2015.
Ratiba Leo: DR Congo na Uganda (5.30pm, Kundi A), Nigeria na Burundi (8.00pm, Kundi B), Guinea na Madagascar (11.00pm).