• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
MWANAMKE MWELEDI: Aliwafungulia milango wanawake wengine

MWANAMKE MWELEDI: Aliwafungulia milango wanawake wengine

Na KEYB

HII leo anatambulika kama mwanamke aliyewafungulia milango wanawake wengine sio tu humu nchini bali barani kote, ili kuwawezesha kufikia huduma za benki, na hivyo kujitegemea kiuchumi.

Katika huduma yake ya zaidi ya mwongo mmoja katika sekta ya benki, Dkt Mary Okelo alijiundia jina na kitambulisho kiasi cha kubandikwa jina ‘Mrs Barclays’, yaani Bi Barclays, kuambatana na mojawapo ya Benki kuu duniani.

Mbali na hayo, yeye ni mwanzilishi wa Kenya Women’s Finance Trust (KWFT), taasisi inayongoza kwa sasa kwa kutoa mikopo midogo kwa wafanyabiashara hasa wanawake.

Aidha, yeye ni muasisi wa chama cha Barclays Bank Women’s Association, chama kilichoanzishwa kwa minajili ya kunasihi wasichana waliokuwa na ndoto ya kuunda taaluma katika sekta ya benki.

Lakini kando na masuala ya huduma za benki, amenawiri pia katika sekta ya elimu ambapo pamoja na marehemu mumewe, walianzisha Makini Group of Schools, mojawapo ya shule maarufu za kibinafsi nchini.

Baada ya kuhudumu kwa muda mfupi katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ambapo akiwa hapa alikuza ndoto za kuwa balozi, alituma maombi mara kadha ili kupata nafasi ya kujifunza kazi katika benki ya Barclays Bank, bila mafanikio.

Lakini hatimaye maombi yake yalikubaliwa mwaka wa 1967 ambapo alipata fursa ya kwenda kupata mafunzo ya kikazi katika Benki ya Barclays jijini London.

Ni akiwa hapa aliona haja ya kurahisisha uwezekano wa wanawake kufikia huduma za benki. Mwaka wa 1976 alianzisha chama cha Barclays Bank Women’s Association kwa minajili ya kunasihi wasichana waliokuwa na ndoto ya kuwa na taaluma katika sekta ya benki.

Mwaka wa 1977, Dkt Okelo alikuwa meneja wa kwanza mwanamke katika eneo la Afrika Mashariki, wakati ambapo wanawake hawakuruhusiwa kupokea mikopo pasipo idhini ya mwanamume na hasa mume au baba.

Nyakati hizo, wanawake waliokuwa wakihudumu katika benki walishikilia nyadhifa duni kama vile za kusafisha, kuandaa chai na keshia miongoni mwa zingine, kwani hawangeruhusiwa kupanda madaraka na kuchukua nyadhifa za juu za uongozi.

Lakini dhana hii haikuzima ndoto na azma yake ya kung’aa kwani kwa ujasiri na ushupavu aliweza kupambana na kujitoma katika sekta iliyotawaliwa na wanaume.

Mwaka wa 1982 alizindua taasisi ya Kenya Women’s Finance Trust (KWFT) ambapo nia yake ilikuwa kusaidia wanawake kufikia mikopo na huduma zingine za kifedha.

Kuendeleza ukuaji

Dkt Okelo aliendelea kuwafungulia wanawake njia hata alipoondoka benki ya Barclays mwaka wa 1985, kwani alikuwa mwakilishi mwanamke wa kwanza wa Kiafrika katika Women’s World Banking, taasisi iliyonuia kuendeleza ukuaji wa kiuchumi wa wanawake.

Jukumu lake hasa lilikuwa kuhamasisha wanawake kuhusu umuhimu wa kujitegemea kifedha, na kuomba serikali za mataifa ya Kiafirika kubadilisha sheria zilizokuwa zikibagua wanawake hasa katika masuala ya kufikia huduma za benki.

Baadaye alihudumu kama mshauri mkuu wa kwanza wa kike wa benki ya African Development Bank, wadhifa alioshikilia kati ya mwaka wa 1987 na 1990, alipokuwa naibu mkuu wa Women’s World Banking.

Mwaka wa 1992, Dkt Okelo aliaga sekta ya benki na kuendelea kusimamia shule za Makini Group of Schools. Shule hii ilianza na wanafunzi wanane pekee katika chumba kimoja nyumbani kwake, lakini chini ya uongozi wake, imekuwa mojawapo ya shule za haiba ya juu za kibinafsi nchini.

Zaidi ya yote, huku wanawake wakiendelea kushikilia nyadhifa kuu katika sekta ya benki nchini, jambo dhahiri ni kwamba ushawishi wake katika vita dhidi ya ubaguzi wa wanawake katika fani hii kamwe hauwezi kupuuzwa.

You can share this post!

Jamaa wazozania mahari ya dada

Atwoli aongoza kampeni za kuzima Ruto Magharibi

adminleo