Michezo

Taekwondo inavyotumika kukuza nidhamu shuleni

June 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA RICHARD MAOSI

Kisaikolojia michezo ina nafasi kubwa kwa ukuaji wa mtoto, katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiakili,kimwili na kijamii.

Ni kwa sababu hiyo wazazi au walezi wanaombwa kuwahimiza watoto wao kushiriki michezo kama vile kukimbia,kuruka kuchora,kuhesabu na kutengeneza maumbo.

Mojawapo ni Taekwondo au karate, mchezo ambao si maarufu sana, ulianzishwa humu nchini rasmi mnamo 1975 na nguli Li Ki -Jin.

Ingawa ulichukua muda kukubalika,baadhi ya watu walifikiri ulikuwa ni utamaduni wa mataifa ya Asia hasa Uchina ambapo ulitumika kucheza filamu za Kunfu.

Hatimaye mwaka wa 2008 Kenya iliwakilishwa,kwenye mashindano ya Olimpiki nchini Beijing kwa mara ya kwanza Dickson Wamwiri akiwakilisha kwenye kitengo cha wanaume,na Milkah Akinyi wanawake.

Kinyume na riadha au kandanda wafuasi wa mchezo huu sio wengi,huku shirikisho la Kenya Taekwondo Association (KTA) limeweka mikakati ya kuufufua.

Mshiriki hufanya vyema akianza kama mtoto kwani viungo vya mwili huwa bado ni nyumbufu na vinaweza kuimarika na kuboreka kadri ya wakati.

Katika kaunti ya Nakuru shule ya wasichana ya Venessa Grant,inayopatikana katika kaunti ndogo ya Rongai ni mfano usiotajwa tu bali pia kuigwa kwa kuhimiza umuhimu wa spoti yenyewe miongoni mwa wanafunzi.

Mwanzilishi wa taekwondo James Wainaina alizindua spoti mnamo 2018 kwa ushinikiano na usimamizi wa shule.

Wainaina anasema ni mchezo unaohitaji stadi ya aina ya kipekee ikiaminika kuwa sio shule nyingi humu nchini zinazoshiriki katika mchezo huu.

Kwa upande mmoja anashindwa kwa nini wasimamizi wa shule hawajaamua kuujaribu miongoni mwa wanafunzi ambao wana vipaji,isipokuwa hawajapata ukumbi wa kujitangaza.

Alielezea kuwa katika mataifa ya Afrika bado wanawake wanakabiliana na changamoto za ukatili kutoka kwa wanaumeume na ndio maana wanahitaji kujilinda.

“Wanahitaji ujuzi wa kukabiliana na wahalifu wadogo ambao wanaweza kuwadhuru na kukatiza ndoto yao kuendelea na masomo,”akasema.

Ingawa zana za kujihami ni bei ghali kama vile sare,kofia na mabuti wanafunzi wamefaidika kwa kupata ufadhili wa shule uliowekeza pakubwa kwenye spoti.

Wainaina alisema shule imeajiri mkufunzi anayewanoa wanafunzi mara mbili kwa wiki ili kuwapatia makali na ujuzi wa kutosha.

Pili shule ndiyo humlipa mkufunzi lakini ijapo katika hatua ya kutathmini ubora wa mwanafunzi mzazi ndiye hugharamikia mtoto wake.

Ili kubaini ubora wa mchezaji,atalazimika kukalia mtihani kubaini endapo amefikia kiwango cha kimataifa.

Kenya Taekwondo Association (KTA),hutumia fomu maalumu kutuza alama kwa kila mwanafunzi anayeshiriki kwenye mchezo huu ili kutoa vipimo vya weledi wake.

Kitu cha msingi ambacho kila mchezaji anahitaji kufahamu kabla ya kushiriki kwenye mchezo huu ni kuhakikisha kuwa hali yake ya mwili ni imara.

Pili awe amejizatiti kwa kufanya mazoezi ya kila mara,kupunguza mafuta mwilini au uwezekano wa kupata majeraha wakati wa kufanya mazoezi.

“Wanafunzi wanaoshiriki huchaguliwa kulingana na kiwango cha nidhamu,wale wasiokuwa na matatizo ya nidhamu wanaweza kufuata masharti kwa urahisi,”alisema.

Ni mchezo unaounganisha ubongo na sehemu za mwili ili kuchangia utulivu anaohitaji binadamu katika maisha kila mara.

Aidha humsaidia mchezaji kuwa na mtazamo chanya kuhusu maisha ambapo anastahili kupambana na kila hali za maisha bila kukata tamaa.

Huwapatia wanafunzi motisha ya kupanda daraja kila anapopata cheti na kuidhinishwa kuwa amepanda daraja la uhitimu.

Mwalimu huyo anaamini kuwa wanafunzi wa taekwondo katika darasa lake wamekuwa huandikisha matokeo mazuri katika masomo yote.

2019 wanafunzi wa Venessa Grant walibwaga wapinzani wao Greensted na Turi International school katika kivumbi wachotwaa nishani ya dhahabu.

Baadae mwezi uliopita wanafunzi wa mwalimu Wainaina walijizatiti na kufikia mzunguko wa wanafunzi katika shule za upili makundi yao yote yakitua fainali.

Gift Muthoni ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Venessa Grant anasema tangu aanze kushiriki taekwondo anaweza kufanya mambo mengi ambayo awali hangemudu.

Amejifundisha umuhimu wa kuheshimu walimu,wazazi na jamii kwa ujumla, siku za mbeleni ataufanya kama taaluma ili aje kujiajiri na kuwaajiri wengine.

Anasema amekuwa akishirikiana na wanafunzi wenzake katika hafla mbalimbali ya michuano inayoandaliwa ndani na nje ya kaunti ya Nakuru.

Anawaomba wazazi kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika mchezo huu,ambao humsaidia mwanafunzi kukomaa kimwili na kiakili.

Kwa upande mwingine mwalimu Wainaina anasema miaka ya themanini ndipo mchezo wa taekwondo ulikuwa umepata mashiko humu nchini.

Lakini kwa sababu ya utepetevu wa washikadau ulianza kudorora kwa mujibu wa viwango na idadi ya klabu zlizokuwa zikishiriki zikaanza kupungua.

Lakini hata hivyo hiyo haifuti dhana kuwa taifa halijakuwa likiwasilishwa vizuri la hasha lakini mikakati zaidi inafaa kuwekwa ili kuwavutia washiriki zaidi.

Samson Lipuka ni mtangazaji mkongwe wa miaka ya 70 aliyechangia kuweka misingi muhimu kwenye fani hii ya mchezo na mpaka leo tunasherehekea mchango wake

Master Moog Yoong ni mfanyiabiashara mwingine aliyefadhili vijana wengi miaka hiyo ya nyuma akitaka waje kuwa wanaspoti mahiri.

Hawa ni baadhi ya manguli ambao walipendekeza kuwa walinzi wa rais, wawe wamejifundisha taekwondo mbali na kutegemea silaha tu kama vile bunduki.