SWAGG: Keanu Reeves
Na THOMAS MATIKO
MWIGIZAJI Keanu Reeves amekuwa kwenye tasnia ya uigizaji tangu miaka ya kenda mia themanini (1980s).
Toka alipoanza uigizaji, mara nyingi amekuwa akivalia uhusika wa mtu katili, mnyama na asiyejali.
Utotoni
Raia huyu wa Canada na Marekani alizaliwa miaka 64 iliyopita mjini Beirut katika taifa la Lebanon.
Hata hivyo alilelewa Hawaii, Marekani. Babake Samuel Reeves alikuwa mwanajiografia na mamake Patricia Taylor alikuwa mnenguaji uchi (stripper).
Akiwa na umri wa miaka mitatu, baba yake aliwakimbia na kumwacha na mamake pekee.
Ili kukidhi mahitaji ya mwanawe, Patricia alilazimika kuzunguka miji mbalimbali akisaka maisha.
Kwenye harakati hizo Keanu aliishia kukulia maisha Australia, Hawaii, New York na Canada.
Hali hiyo iliathiri masomo yake akilazimika kusomea shule nne tofauti za sekondari kitu kilichomsumbua sana na kumpelekea kuachana na masomo hayo akiwa na miaka 17 pekee.
Kiu yake ya sanaa ilianza mapema mno akijikuta akijihusisha na masuala ya drama alipokuwa kidato.
Ari hiyo ilimchochea sana kiasi cha kuamua kuhamia Los Angeles ili aweze kusaka michongo ya kuendeleza taaluma yake ya uigizaji.
Alibahatika na kuangukia mchongo wa kuigiza kwenye esisodi moja ya kipindi cha Hanging In.
Toka hapo akaanza kupata dili za kimatangazo za televisheni.
Sanaa
Mchongo wake mkubwa kwenye uigizaji ulimwangukia 1986 aliposhirikishwa kwenye filamu ya River’s Edge.
Ilihusu kundi la washikaji matineja waliopatwa na mshtuko mkubwa uliotishia kuwaathiri baada ya mauaji ya mmoja wao.
Keanu aliishia kusifiwa sana na wachambuzi wa filamu kutokana na kiwango alichokionyesha mule.
Hilo likachangia kumfungulia milango zaidi ya nuru akiishia kupata dili za kuigiza kwenye komedi maarufu enzi hizo Bill & Ted’s Excellent Adventure.
Ufanisi wa komedi hiyo ukamsababishia kupata mchongo kwenye filamu za Bram Stoker’s Dracula na My Own Private Idaho.
Aanza kuunda mkwanja
Taratibu alizidi kupanda akitokea kwenye filamu nyingine iliyofanya vizuri sana Speed (1994) alikoshirikiana na nyota Sandra Bullock.
Ufanisi wa filamu hiyo ulimpelekea kulipwa dola 1.2 milioni huku yenyewe ikitengeneza dola 350 milioni.
Kazi iliyofuatia ikawa kubwa hata zaidi alipoangukia mchongo wa kuigiza kwenye misururu ya filamu za The Matrix.
Kwenye msururu wa kwanza, alilipwa dola 10 milioni kisha akapokea dola 15 milioni kwa ya pili na kiasi kingine kama hicho kwa ya tatu.
The Matrix Reloaded ndiyo filamu aliyoigiza na katika zote iliyoweza kuandikisha mauzo makubwa kwenye Box Office.
Pia ndiyo ilichangia thamani yake kupanda kwelikweli huku ikimpatia utajiri wa maana.
Kwa mujibu wa takwimu, Keanu ambaye kwa sasa anatamba na John Wick 3, anakadiriwa kuwa na utajiri wa thamani ya dola 350 milioni.
Mjengo
Keanu anamiliki jumba la kifahari mjini Los Angeles linalokadiriwa kuwa la thamanai ya dola 4 milioni.
Ni mjengo wa kizamani uliojengwa 1980 ila umekuwa ukifanyiwa ukarabati wa mara kwa mara ili kuendana na wakati. Kwa mfano kuongezwa dimbwi la kuogelea, uwanja wa kucheza soka na mambo kama hayo.
Usafiri
Ni mraibu mkubwa wa pikipiki akimiliki moja aina ya 1973 Norton 850 Commando ambayo ni nzuri kwa masafa marefu.
Pia anayo West Coast Choppers ambayo hutumia sana kwa matanuzi ya mji na nyingine Harley-Davidson Dyna Wide Glide. Anayo pia Porsche 911 C4 na Mercedes Benz.
Usilolijua
Akiwa kwenye harakati zake za kuanza taaluma ya uigizaji, 1989, Keanu aliishia kuunda ushikaji wa karibu sana na mwigizaji mwenza River Phoenix ambaye nyota yake ilikuwa imeanza kung’aa kama yake.
Hata hivyo, ushikaji wao ulikatizwa baada ya Phoenix kuwa mraibu wa dawa za kulevya.
Siku moja mwaka 1993 alizidisha vipimo vya mchanganyiko wa mihadarati kwa kuchanga kokeni, heroin na valium na kwa bahati mbaya zilimuua. Kifo chake kilimvuruga sana Keanu.
Kipindi hicho alikuwa na miaka 23, umri sawa na Phoenix.
Miaka mitano baadaye alikutana na mwanamke mrembo Jennifer Syme na kuwa wapenzi.
Jennifer alipata mimba na kujifungua mtoto wa kike akiwa amekufa Desemba 1999.
Kitu hicho kilivuruga uhusiano wao na kuwapelekea kuachana wiki chache baadaye.
Mwaka mmoja na nusu baadaye toka watengane, Jennifer alihusika kwenye ajali ya barabarani akiwa anatoka pati na kupoteza maisha yake.
Toka wakati huo, Keanu hajawahi kuwa na tamaa ya kuingia kwenye mahusiano ya kudumu kwa kuhofia kuumizwa tena.