• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Uhai wa DP Ruto kuwa hatarini ni ishara Rais hana udhibiti?

Uhai wa DP Ruto kuwa hatarini ni ishara Rais hana udhibiti?

Na MWANGI MUIRURI

WADADISI wa masuala ya kiusalama na kisiasa sasa wanaonya kuwa udhibiti wa kiserikali wa Rais Uhuru Kenyatta uko na shaka.

Kuwa vyombo vya habari vimeripoti kuwa suala hili liliwasilishwa kwa Rais kabla ya kuanikwa hadharani, Rais akasemwa kuwa aliandaa mkutano wa dharura wa kiusalama na hatimaye akaagiza usalama wa Naibu Rais William Ruto uimarishwe na pia suala hilo lichunguzwe, matukio hadi sasa yanaashiria hakuchukuliwa kwa uzito.

“Lau angechukuliwa kwa uzito, basi Ruto angeandikisha taarifa rasmi ili kusaidia uchunguzi wa kina ufanywe, maafisa husika hasa wale wa idara ya ujasusi (NIS) wangekuwa na ushahidi wao wa kumpa Rais na pia maafisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) wangeshughulikia suala hili kama la dharura,” anasema mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri.

Anasema kuwa ikiwa Rais ana ule udhibiti wa kiserikali, kuna adabu za kimsingi ambazo mawaziri wanaosemwa kuwa wanapanga njama hiyo wangetekeleza walipojitokeza kukataa kuwa waandalizi wa njama ya kumuua DP Ruto.

“Walimsuta DP Ruto wakisema kuwa amechukua mkondo wa kipuuzi. Huwezi ukamsuta Naibu Rais kwa maneno kama hayo ikiwa kwa kweli unamheshimu au unaheshimu Rais. Hii serikali haina ule ushikamano,” anasema.

Anasema kuwa ni wakati mwafaka wa Rais kutembeza mjeledi wa kinidhamu ndani ya serikali yake kwa kuwa huu mkondo ambao umeanza kujipa taswira ni ule wa serikali ambayo “iko katika vita vya wenyewe kwa wenyewe katika kila afisi ya huduma na kiutawala.”

Mhadhiri wa somo la sayansi ya siasa, Gasper Odhiambo anasema Rais Uhuru Kenyatta ndiye ametoa mfano wa kuigwa wa kupayuka hadharani kuhusu masuala nyeti badala ya kuyashughulikia kwa weledi na tajriba ya kiuongozi.”

“Rais ndiye ametupa mfano wa kuiga wa kupiga kelele hadharani, kutoa vitisho, kuahidi bila kutimiza na hata kuzomeana hadharani pasipo nia ya kuandaa vikao na hao wadogo wake na kuwapa masharti ya utendakazi katika usiri wa miundombinu ya kiutawala,” amesema Odhiambo.

Kuiga

Anasema kuwa naye Ruto amechukua tu mfano wa mkubwa wake wa kuchukua suala nyeti kuhusu usalama wake na kuligeuza kuwa la kisiasa hadharani ambapo kwa sasa mawaziri wanne na makatibu kadhaa na pia wakurugenzi wa mashirika ya umma wako katika mtandao wa wachunguzi wa makosa ya jinai kwa madai kuwa wanapanga kumuua.

“Wakati serikali haina mwongozo thabiti wa kushughulikia masuala nyeti katika usri mkuu wa serikali ambao unafaa kuwa nembo ya serikali, kila mtu akiwa na lake la kutangaza anakimbia mitaani na kupayuka. Rais akiwaongoza kufanya hivyo, nao lazima wafuate nyayo,” asema.

Aliyekuwa Mkuu wa Kiutawala kwa muda mrefu, Joseph Kaguthi anasema haya yanayojadiliwa kwa sasa ni masuala nyeti sana.

“Sitaki kujiingiza kwa mjadala huu kwa kuwa hauna mashiko kwa sasa. Mimi kama afisa mstaafu wa serikali katika usiri wa serikali nitangoja kama wengine kuona mwisho wa madai haya,” amesema Kaguthi.

Anasema wakati madai kama haya yanaanza kusambaziwa umma, mambo mengi hufanyika, akiyataja baadhi ya mambo hayo kuwa kejeli kwa vyombo vya usalama, kudunishwa kwa hadhi ya wengi katika sakata hiyo na serikali kugeuka kuwa ya kisarakasi.

Anasema kuwa wanasiasa tangu jadi wamekuwa wakilalamika kuwa uhai wao uko hatarini.

Anasema upo wakati madai kama hayo yameishia kuwa na ukweli, lakini mara nyingine yakiwa ni hali tu ya miereka ya kisiasa.

Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro (pichani) naye anasema wamekuwa wakilalamika.

Tumekuwa tukiteta kuwa kuna njama ya kuhangaisha wandani wa DP Ruto Mlima Kenya. Wengi wamekuwa wakitupuuza na hatuna lingine ila kusisitiza kuwa tutazidi kuchukua tahadhari. Kuna afisa mkubwa katika kitengo cha kiusalama ambaye amekuwa akiwakanya maafisa wa kiusalama mashinani dhidi ya kujitokeza katika hafla za DP Ruto mashinani,” anasema Nyoro.

Anashikilia kuwa “njama hizo za kumuanika DP Ruto kama asiyefaa kulindwa kiusalama ni njama fiche ya kuweka maisha yake hatarini.”

  • Tags

You can share this post!

Sauti mtaani kuhusu madai ya uhai wa Ruto kuwa hatarini

Arsenal kuvunja benki kumsajili Zaha

adminleo