• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
AFCON: Kivumbi chatarajiwa kwa ‘fainali ndogo’ Kenya Vs TZ

AFCON: Kivumbi chatarajiwa kwa ‘fainali ndogo’ Kenya Vs TZ

Na GEOFFREY ANENE

Harambee Stars ya Kenya na Taifa Stars ya Tanzania wameapa kuonyeshana kivumbi Juni 27 kila mmoja akitafuta kuepuka uwezekano mkubwa wa kutoka Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri bila pointi.

Kenya, ambayo imetaja mchuano huo wa pili wa Kundi C kama fainali, ilirejelea mazoezi Jumatatu jioni.

Kocha Sebastien Migne amekiri kwamba kupoteza mechi ya ufunguzi dhidi ya Algeria kumeweka timu yake pabaya.

“Mechi kati ya Kenya na Tanzania itakuwa ngumu sana. Tunafurahia kuwa AFCON baada ya kuwa nje miaka 15. Kwa bahati mbaya tulianza kampeni kwa kupoteza dhidi ya Algeria, ambayo ni timu nzuri ilio na uwezo wa kufika hata fainali.

“Hata hivyo, matumaini yetu ya kupata angaa ushindi mmoja bado yapo. Mechi dhidi ya Tanzani itakuwa kama fainali kwetu. Inatupa fursa kubwa na pengine ya kipekee kushinda mechi katika makala haya,” Mfaransa huyo alieleza Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) baada ya mazoezi ya Juni 24.

Tanzania pia imeapa kutafuta pointi zake za kwanza kwenye mashindano haya ya mataifa 24 dhidi ya Kenya. Akizungumzia mchuano huo utakaochezewa uwanjani 30 June jijini Cairo, beki Gadiel Michael (Young Africans), ameambia Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF), “Mechi dhidi ya Kenya ni yetu sisi kupata pointi. Sisi ni majirani. Tunawajua nao pia wanatujua. Itakuwa mechi ngumu. Sisi kama wachezaji tumejipanga. Tukipoteza dhidi ya Kenya haitakuwa vizuri.

“Itatupa mwanga tutakapoelekea. Mashindano haya ni mashindano ambayo kila mchezaji anatamani kuonyesha kile anacho ili angalau na sisi tupate kuenda nje ya nchi.”

Desert Foxes ya Algeria inaongoza jedwali kwa alama tatu ikifuatiwa kwa alama sawa na Teranga Lions ya Senegal ambayo ililima Tanzania 2-0. Kenya na Tanzania zinashikilia nafasi mbili za mwisho bila pointi. Algeria na Senegal zitakabana koo Juni 27 kabla ya kukamilisha mechi za makundi dhidi ya Tanzania na Kenya mnamo Julai 1, mtawalia.

Kenya na Tanzania, ambazo zinarejea katika AFCON baada ya kuwa nje miaka 15 na 39 mtawalia, zimewahi kukutana mara 48 katika historia yao. Harambee Stars inajivunia ushindi 20. Tanzania imelemea Kenya mara 14, huku mechi 14 zikimalizika sare.

Vijana wa Migne wanashikilia nafasi ya 105 duniani nao Tanzania, ambao wanafundishwa na raia wa Nigeria Emmanuel Amunike, wako katika nafasi ya 131.

Baadhi ya nyota watakaonogesha mchuano huu ni kiungo Victor Wanyama, mvamizi matata Michael Olunga na kipa Patrick Matasi (Kenya) na beki Gadiel, kipa Aishi Manula na washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Makocha Djamel Belmadi (Algeria) na Aliou Cisse (Senegal) pia wametaja mechi kati yao kuwa fainali kabla ya fainali kwa sababu bado wanahitaji angaa alama tatu katika mechi zao mbili zilizosalia kujihakikishia tiketi ya raundi ya 16-bora.

You can share this post!

Manyatta na Kitale Queens washindi wa Chapa Dimba

Rotich apewa siku 10 kujibu kesi ya bima ya bodaboda

adminleo