KINA CHA FIKIRA: Nahiari kusema benki badala ya banki, japo yote yanakubalika
Na KEN WALIBORA
NILIKWENDA hospitalini majuzi yale kuangaliwa meno nikakutana na mpokezi aitwaye Jennifer Mbwali.
Jambo la kwanza alilofanya ni kujaribu kunitambua kwa sauti yangu.
“Hiyo sauti nimeisikia wapi?” Akakuna kichwa na akafikia mkataa kwamba mimi ni Ken Walibora mtangazaji.
Yaani mtu anaweza kukutambua kwa sauti tu!
Hii ndiyo athari ya kitu kiitwacho redio. Na kama anakutambua kwa sura itakuwa labda keshakuona kwenye runinga.
Hilo la kutambuliwa kwa sauti au sura wala mimi halishtui sana. Sikushtuka sana.
Alichonishtua nacho Jennifer na swali lake punde tu aling’amua mimi nani.
“Hebu niambie nini sawa kati ya Banki na Benki?” aliuliza.
Hilo swali ndilo limekuwa linapiga vichwa vya habari hapa Kenya kwa majuma machache yaliyopita tangu Gavana wa Benki Kuu atangaze kubadilishwa kwa sarafu ya Kenya.
Kwa mtu aliyekwenda kuangaliwa meno hospitalini kukumbana na swali kama hilo ni jambo la kushangaza kwa kweli.
Sikutarajia. Ila naona kwamba labda inabidi “nikubali matokeo” kama wengi wanapenda kusema siku hizi kuelezea hali zisizoweza kuzuilika.
Kwangu kuuliza maswali yanayohusiana na Kiswahili si jambo geni.
Kwa hiyo sina budi kukubali kuulizwa na kujibu maswali anuwai na yeyote popote pale. Yamkini ndiyo ukweli halisi kuhusu maisha yangu kwa sasa.
Jennifer aliponiuliza nilikumbuka kwamba nilikuwa tayari nimeulizwa vivyo hivyo kwenye mitandao kama vile Twitter kwa simu na hata kupigiwa simu na vyombo fulani vya habari.
Jibu
Katika safu hii leo nataka nitoe tena jibu langu ambalo nimekuwa nalitoa kwa kila anayeuliza.
Kwanza sikubaliani na wale wanaodai kwamba Banki Kuu ni kosa.
Aidha, sidhani kwamba kwangu kusema Benki Kuu ni kosa. Almuradi kwangu mimi maneno yote mawili ni sahihi.
Kanuni ya utohozi ni kwamba unabeba neno lilivyo na kulihamishia katika lugha lengwa kutoka kwa lugha asili. Lugha asili ya habari ya Banki na Benki ni Kiingereza.
Nacho Kiingereza kimekuwa na kitaendelea kuwa lugha asili ya maneno mengi ya Kiswahili.
Kwa kweli siku hizi aghalabu kila neno jipya la Kiswahili linaelekea kutoka kwa Kiingereza.
Nafasi hatuna ya kuorodhesha maneno mengi yenye asili ya Kiingereza katika Kiswahili ingawa hapa sharti tuonye kwamba hata Kiingereza chenyewe huwa kimekopa asilimia themanini ya maneno yake.
Nasisitiza kwamba utohozi si dhambi kama watu wengine wanavyofikiria.
Lugha zote hutohoa katika ukopaji wa maneno. Neno lishatoholewa aghalabu hukaribiana sana na lilivyokuwa katika lugha asili.
Tatizo la utohozi wa Kiswahili ni kwamba wakati mwingine hakuna maafikiano kuhusu kama utohozi unajikita katika tahajia za neno au vile neno linavyotamkwa katika lugha asili.
Kwa mfano tunasema biolojia (tahajia) au bayolojia (matamshi)? Tunasema radio (tahajia) au redio (matamshi), Desemba (tahajia) au Disemba (matamshi)?
Nasisitiza maafikiano hapana, ndipo tunasema “benki” na “banki” yote ni sahihi. Ila mimi kwa hiari yangu mwenyewe napenda kusema benki.