VITUKO: Simba naye aahidi kumwondolea Mama Asumini ‘mzigo wa dhiki’
Na SAMUEL SHIUNDU
JAPO kongamano lao lilitia nanga, Simba hajarejea Bushiangala.
Angali ywatafuna vyakula vya pwani, ywavuta hewa ya huko, vywaogelea kwenye fuo za huko na ywafurahia matanuzi na Asumini.
Yalianzia Bushiangala.
Simbamwene alimtangazia kwamba angehudhuria kongamano la walimu wakuu. Alisikitika kwamba mfuko wake haungemruhusu kuandamana naye.
Asumini naye akamjibu kuwa hangeweza kukaa Bushiangala bila Simba, “Nina uwezo wa kutukalisha pwani kwa miaka kadhaa.” akamhakikishia.
Simba akaufyata asije akaipoteza nyota njema iliyomjongelea. Ni wangapi hutafuta wafadhili wakashindwa? Yeye kajaliwa mfadhili mzuri aliyekuwa radhi kugharamika kwake. Na mfadhili mwenyewe totoshoo la kuwatia wanaume kiherehere! ‘Sasa sitatumia hata senti moja kwa zile hela nilizozoa kwenye mikoba ya shule.’ Simba alijiambia.
Wakiwa pwani, Simba aligundua kuwa mhisani wake alipenda sana kumuulizia kuhusu pesa za awali.
‘Wanasemaje huko nje kuzihusu? Je huko kwenye kongamano mmezizungumzia? Mtu akipatikana nazo atafanywaje. Haya ni baadhi ya maswali aliyopenda kuuliza Asumii. Simba alivyokuwa na tajiriba ya kuzisoma nyuso za wanafunzi, aligundua kwamba Asumini alikuwa na wasiwasi kila alipoyagusia maswala ya pesa geni. Akaamua kutingisha kiberiti aone kama kilikuwa na njiti.
“Nasikia ukipatikana na zaidi ya laki tano ya pesa hizo za awali unaweza kuhukumiwa kifo,” Simba akaongopea.
Rafiki mwema
Asumini alimpima Simba na kumchukulia kama rafiki mwema.
Licha ya ulevi wake, hajapata hata siku moja kutaka kumuibia hata peni.
Hajawahi kumtazama kwa jicho la uchu kama wanaume wengi wa Bushiangala waliommezea mate na kumrushia mistari ya mapenzi kila walipopata upenyu wa kuzungumza naye.
Alijilinganisha na mgomba ulioota kwenye msitu wa nyani wenye njaa ya ndizi. Aligombaniwa kama mpira wa kona.
‘Huyu lakini ni mstaarabu. Akiniomba sitamkatalia’ Asumini alijihakikishia.
Walikuwa wameenda hata kumwona Riziki. Riziki ambaye alisemekana kuwa na uchawi wa kuwanasa wanaume.
Riziki ambaye alipapurana na mabinti wakigombea wanaume. Lakini Simbamwene hakumwangalia Riziki kwa macho ya ulafi. ‘Huyu naweza kumfichulia siri yangu, Asumini akajiambia. Wakafwatana chumbani.
Akamwambia kuwa alikuwa na mzigo na alitaka Simba amsaidie kuutua. Akalivuta begi moja kubwa kutoka mvunguni mwa kitanda na kulifungua.
Simba aliachama. Vibunda vya noti za elfu vililaliana kwa utulivu begini. Alizitwaa noti kadhaa na kuhakikisha kuwa hazikuwa ghushi. “Pesa hizi zote ulizipata wapi?” aliuliza.
“Hilo ni swali la kujibiwa siku nyingine, kwa sasa nataka ziniondokee,” Simba alimkumbatia Asumini na kumuahidi msaada katika wakati huo mgumu.