• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
USWAHILINI: Mila ya Wataita haikumruhusu baba mkwe kula mbele ya mkazamwana

USWAHILINI: Mila ya Wataita haikumruhusu baba mkwe kula mbele ya mkazamwana

Na LUDOVICK MBOGHOLI

BABA mkwe hakuruhusiwa na mila au utamaduni wa jamii hiyo kuwa karibu na mahali ambapo mkaza mwanawe anapika au kupakua chakula.

Desturi za Wataita zinasadikisha kuwa, endapo baba mkwe angekiuka mila na utamaduni huo, basi anaipa laana familia ya mwanawe.

Inadaiwa laana ambayo ingemwandama mwanawe na mkaza mwana ni pamoja na mikosi ya kukosa riziki, ugomvi usioisha, maradhi na hata watoto waliozaliwa kutokuelewana.

Pia inadaiwa baba mkwe hangeweza kusikilizana na wajukuu wake mbali na kuwepo kwa mikosi mingi ambayo ingeandama vizazi vya wanawe.

Kadhalika inasemekana baba mkwe hangeweza kuishi bila misukosuko endapo angekiuka maagizo ya kimila na kitamaduni, akawa anakula, anakunywa au kutafuna chakula mbele ya mkaza mwanawe.

Inaarifiwa kuwa familia ya baba mkwe pia ingeanza kuzorota huku baba mkwe huyo na mkewe wakiwa hawaelewani nyumbani, hasa katika masuala yanayohusu mashauriano ya pamoja.

Vilevile, ukiukaji wa mila hiyo pia unawafanya watoto wa familia kushindwa kujitatulia matatizo nyeti ambayo yanazikabili familia zao.

Katika historia inayoelekea kufifia, baba mkwe akiona mkaza mwana anakula, ni sharti aondoke machoni mwake.

Na endapo yeye (baba mkwe) anatafuna chakula, mkazamwana akitokezea mbele yake anasitisha kutafuna mpaka apite.

Wakati mkaza mwana anatokea ghafla, hata kama baba mkwe anamalizia kutafuna anachokula, basi ni lazima asitishe kumeza, ila atameza tu punde atakapomwondokea machoni.

Mambo kufifia

Maboma mengi ya jamii za Wataita yaliimarisha mila na utamaduni huo hadi Karne ya 21 ambapo mambo yalianza kufifia na mila kupitwa na wakati.

Kwa sasa ‘mambo leo’ yanachukua mkondo na kufifisha kabisa mila hiyo iliyoenziwa na wazee wa kikale. Hata hivyo baadhi ya wazee wa jamii ya Wataita wanasadikisha kuwa huenda upotofu wa imani katika mila na utamaduni ndio chanzo cha vijana wengi kushindwa kuimarisha ndoa zao.

Inadaiwa ndoa nyingi za kileo haziimariki, hujaa mizozo na hali ya suitafahamu kutokana na ukosefu wa imani sawa na kutofuatilia mila na utamaduni wa jadi.

You can share this post!

VITUKO: Simba naye aahidi kumwondolea Mama Asumini ‘mzigo...

SEKTA YA ELIMU: Magoha akome kutoa maagizo tu, amalize...

adminleo