Chepkoech na Manangoi wathibitisha kushiriki mbio za Herculis
Na GEOFFREY ANENE
WAKIMBIAJI nyota kutoka Kenya Beatrice Chepkoech na Elijah Manangoi wamethibitisha kushiriki mbio za mita 1609 (maili moja) za Herculis mnamo Julai 11-12 mjini Monaco, ambayo ni ya tisa ya Riadha za Diamond League.
Waandalizi wamesema kwamba Chepkoech, ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, atapata ushindani mkali.
Atakabiliana na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 Muethiopia Genzebe Dibaba pamoja na mzawa wa Ethiopia Sifan Hassan, ambaye ni mkimbiaji matata wa Uholanzi. Hassan anashikilia rekodi ya dunia ya mbio za kilomita tano.
Watatu hawa walipata rekodi zao za dunia mjini Monaco. Mwaka 2015, Genzebe alivunja rekodi ya Mchina Qu Yunxia ya dakika 3:50.46 iliyokuwa imedumu tangu mwaka 1993. Aliweka rekodi mpya ya dakika 3:50.07.
Chepkoech alifuta rekodi ya dunia ya mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi ya Mbahraini Ruth Jebet, ambaye alizaliwa Kenya, ya dakika 8:52.78 iliyokuwa imedumu tangu mwaka 2016 na kuweka 8:44.32 mwaka 2018. Hassan alitimka rekodi mpya ya dunia ya kilomita tano ya saa 15:48 mwezi Februari mwaka 2019.
Mfalme wa Riadha za Dunia za mita 1,500, Elijah Manangoi atashindania taji la Herculis la maili moja dhidi ya mshikilizi wa rekodi ya dunia ya ukumbini Samuel Tefera na bingwa wa Olimpiki na Riadha za Ukumbini za mita 1,500, Matthew Centrowitz.
Kabla ya duru ya Herculis, kuna duru za Prefontaine Classic mjini Sanford nchini Marekani mnamo Juni 30 na Athletissima mjini Lausanne nchini Uswizi mnamo Julai 4-5. Riadha za Diamond League zinajumuisha duru 14. Duru sita tayari zimefanyika ambazo ni Doha (Qatar), Shanghai (Uchina), Stockholm (Uswidi), Roma (Italia), Oslo (Norway) na Rabat (Morocco).