• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
UONGEZEAJI THAMANI: Kiwanda kipya cha maziwa ya ngamia chatoa fursa ya kipato

UONGEZEAJI THAMANI: Kiwanda kipya cha maziwa ya ngamia chatoa fursa ya kipato

Na RICHARD MUNGUTI

MAZIWA ya ngamia ambayo ni adimu katika maduka mengi yataanza kuuzwa kwa viwango vikubwa kufuatia kuzinduliwa kwa kiwanda cha upakiaji.

Ijapokuwa maziwa ya ngamia yanahusishwa na jamii za Kaskazini mwa Kenya, sasa yataanza kuuziwa kila mmoja.

Kiwanda kijulikanacho kama Nuug Camel Milk Products Limited kilichoko Enterprise Road eneo la Viwandani Nairobi kimeanza upakiaji wa maziwa ya ngamia.

Kiwanda hiki kinatengeneza maziwa ya ngamia ya ladha ya Embe (mango flavor), Vanilla na Strawberry mbali na kupakia maziwa ya kupika chai.

Maziwa haya sasa yanatazamiwa kutoa ushindani mkubwa kwa maziwa ya ng’ombe na mbuzi yanayotengenezwa na kampuni za Kenya Cooperative Creameries (KCC), Brookside, Daima na Delamere.

Kiwanda hiki kipya kilizinduliwa wiki jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ngamia Ulimwenguni (World Camel Day-WCD).

Siku ya WCD husherehekewa kila Juni 22 kote ulimwenguni na hapa Kenya siku hiyo iliadhimishwa katika hoteli ya Khulan inayouza vyakula miongoni mwavyo maziwa na nyama ya ngamia.

Kiwanda hiki kimeanza shughuli za kuzalisha bidhaa mbali mbali za maziwa ya ngamia.

Kiwanda hiki kinachomilikiwa na kampuni Khulan Foods Company ndicho cha kwanza hapa jijini Nairobi kuanza upakiaji wa bidhaa za maziwa ya ngamia.

Viwanda vingine viko mijini Garissa na Nanyuki.

Kiwanda cha kwanza kuzinduliwa nchini ni hicho cha Nanyuki kilichoanzishwa 2008 na cha pili ni cha Garissa.

Kwa mwaka, kati ya lita 340 na 500 milioni za maziwa ya ngamia huzalishwa na wafugaji Isiolo, Turkana, Mandera, Garissa na Laikipia.

Nchi ya Kenya ndiyo ya tano ulimwenguni katika ufugaji ngamia, ikiwa na 3.3 milioni ambazo awali zilikuwa zinatambuliwa kama wanyama pori.

Hafla ya kuzinduliwa kwa kiwanda hicho ilihudhuriwa na wasomi watajika katika sekta ya utafiti katika chuo kikuu cha Nairobi Profesa George Gitau, Mtafiti wa masuala ya tiba ya wanyama Dkt Kenneth Wameyo, Mkurugenzi wa mamlaka ya ustawishaji wa Mto Ewaso Nyiro iliyoko kaunti ya Samburu, Bw Robert Lemerketo, Mshirikishi wa kitaifa wa Chama cha Ngamia (KMCA) Bw Khalifa Abey na wabunge kutoka Kaskazini.

Wabunge waliofika ni Mwakilishi Mwanamke wa kaunti ya Wajir Bi Fatuma Gedi, Mbunge wa Kamukunji (Jubilee) Yusuf Hassan, Mbunge wa Mandera Kaskazini Meja Sheikh Bashir na aliyekuwa naibu wa Gavana Bw Guled Simba.

 

Baadhi ya viongozi kutoka Kaskazini Mashariki, Kenya wakionyesha bidhaa za maziwa ya ngamia wakati wa uzinduzi wake, Nairobi, majuzi. Picha/ Richard Munguti

Chama hiki cha kitaifa cha Ngamia kilianzishwa mwaka 1997 lakini hakikushika kasi bali kilizongwa na siasa duni.

Sasa kinasema kiko msitari wa mbele kustawisha ufugaji wa ngamia na uuzaji wa bidhaa zake ambazo ni maziwa, nyama na ngozi yake.

“Sasa tunazingatia kuimarisha uzalishaji bidhaa za maziwa ya ngamia zifikie upeo kama vile bidhaa zile nyingine za mifugo,” Bw Abey alisema.

Mshirikishi huyo alifichua kuwa kila mwaka wanaouza maziwa ya ngamia hujizolea zaidi ya Sh10 bilioni.

Akasema Abey: “Ni kina mama tu wanaohusika na uzalishaji wa maziwa ya ngamia. Wanaume hawashiriki hata na kina mama ndio wanaokama ngamia na kuuza maziwa. Familia nyingi hunufaika na maziwa haya kwani pesa za mauzo yake hugharamia karo za shule.”

Bw Abey alisema nia kuu ya kuzindua viwanda hivi ni kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa za viwango vilivyowekwa na shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini (Kebs).

Kwa sasa ni asili mia 15 tu ya maziwa ya ngamia yanayofikishwa sokoni na kuuzwa.

Kiwango kikubwa cha maziwa ya Ngamia huharibika kutokana na jinsi yamehifadhiwa.

Bw Abey alisema changamoto kubwa ni Serikali kutostawisha bidhaa za ngamia na kuwataka wabunge kutoka maeneo yanayofugwa ngamia wawasilishe hoja bungeni ya ustawishaji mifugo hao.

Alisema 2016 mamlaka ya ustawishaji ngamia ulizinduliwa ilipotambulikana maziwa yake yako na umuhimu kiafya.

You can share this post!

AKILIMALI: Mtaalamu wa kilimo na balozi wa siha njema

Uchambuzi: Jubilee ni chama imara au kigae?

adminleo