Wanyama aandalia Harambee Stars dhifa ya mlo wa jioni jijini Cairo
Na GEOFFREY ANENE
NAHODHA wa Harambee Stars, Victor Wanyama alionyesha ukarimu wake Kenya inapojiandaa kukutana na Senegal katika mechi yake ya mwisho ya Kundi C kwa kualika timu nzima kwa chakula cha usiku jijini Cairo nchini Misri mnamo Juni 28, 2019.
Kiungo huyu, ambaye tovuti ya michezo ya Spotrac inasema analipwa Sh439,132,420 kila mwaka na klabu ya Tottenham Hotspur nchini Uingereza (Sh8,444,854 kila wiki), aliamua kuwafurahisha baada ya Kenya kutoka chini mara mbili na kulipua Tanzania 3-2 uwanjani 30 June mnamo Juni 27.
Vijana wa Sebastien Migne walijipata chini bao 1-0 baada ya Saimon Msuva kumwaga kipa Patrick Matasi dakika ya sita. Ilisawazisha 1-1 kupitia kwa Michael Olunga dakika ya 39. Ilijipata nyuma tena sekunde chache baadaye baada ya Mbwana Samatta kurejesha Tanzania mbele 2-1 dakika ya 40 kabla ya Johanna Omolo kusawazisha 2-2 dakika ya 62 naye Olunga akafunga ukurasa wa magoli dakika ya 80.
Ushindi huu wa pili wa Kenya katika AFCON tangu ianze kushiriki mashindano haya ya kifahari mwaka 1972 baada ya kuchapa Burkina Faso 3-0 mwaka 2004 katika mechi za makundi, ulistahili sherehe.
Kama mchezaji anayelipwa fedha nyingi kuliko wachezaji wote pamoja na benchi la kiufundi katika Harambee Stars, Wanyama alikuwa mstari wa mbele kuonyesha kuridhika kwake. Aliwanunulia vyakula katika hoteli moja ya kifahari jijini Cairo.
Wengi waitikia mwito
Picha zilizochapishwa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) katika mtandao wake wa kijamii zinaonyesha timu nzima ya Harambee Stars wakiwemo Migne, Olunga na winga matata Ayub Timbe na wengineo, waliitikia mwito wake.
Karamu hiyo iliwasili siku chache tu baada ya Wanyama kugonga umri wa miaka 28 hapo Juni 25 na kutembelewa na kakake McDonald Mariga.
Kenya ilianza kampeni yake kwa kupoteza 2-0 dhidi ya Algeria mnamo Juni 23 kabla ya kulemea Tanzania na kufufua matumaini ya kuingia raundi ya 16-bora.
Vijana wa Migne watajikatia tiketi ya kushiriki mechi za kuingia robo-fainali wakipiga Senegal inayojivunia ushindi mbili za 3-0 pamoja na sare tasa dhidi ya Kenya katika historia ya mataifa haya.