Makala

Baraka ya ujauzito iligeuka kuwa mahangaiko na kudhoofika kiafya

June 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na MWANGI MUIRURI

[email protected]

Twitter: @Mlincoln

MNAMO Mei 12, 2012, gari dogo kuukuu, mwendo wa saa mbili usiku liling’orotesha injini yake hadi boma la mjane Ruth Njeri aliyekuwa na umri wa miaka 72 wakati huo.

Gari hilo lilikuwa limebeba balaa kubwa katika maisha ya huyu mjane na ambapo hadi sasa, hajawahi kutulia katika maisha yake akiwa na umri wa miaka 80 kwa sasa.

Bi Njeri ambaye anafanya kazi za kijungu jiko kupitia vibarua katika mashamba ya mabwanyenye kijiji cha Gikarangu ndani ya Kaunti ya Murang’a anasema ujio wa gari hilo ndani ya boma lake ulibadilisha maisha yake kabisa.

Anasema kuwa ule wakati mwingine gari liliingia katrika boma lake ilikuwa ni mwaka wa 2006 ambapo gari aina ya pickup linalomilikiwa na jirani yao liliingia kuchukua mwili wa mumewe – ambaye aliaga dunia akiwa usingizini – ili kuupeleka hadi mochari ya Murang’a.

“Majirani walijitokeza kunijulia hali kwa kuwa ni lazima ingekuwa hali isiyo ya kawaida kupata gari ndani ya boma langu… Ndipo kwa pamoja tuligundua kuwa gari hilo lilikuwa limembeba Hannah Wanjiru aliyekuwa katika hali mahututi,” anasema Bi Njeri.

Miaka miwili kabla ya tukio hili, Bi Wanjiru akiwa mwingi wa matumaini katika maisha na kesho yake alikuwa ameondoka nyumbani na kuelekea hadi jijini Nairobi kusaka ajira.

Miezi mitatu baadaye, habari zilifika nyumbani kuwa Bi Wanjiru alikuwa amejipa mume kwa jina Anthony Ng’ethe Munyua na ambapo walikuwa wakiishi katika mtaa wa Kinoo.

“Sijawahi kufika katika Jiji la Nairobi, lakini nilipopata habari hizo nilimshukuru Maulana na nikamuomba aibariki familia ya binti yangu na aijalie mema ya kimaisha,” anasema Bi Njeri.

Hata hivyo, mkosi wa kimaisha ulikuwa unaandama maisha ya binti huyu katika ndoa hii, taswira ikiwa kana kwamba Shetani alikuwa amekula kiapo kuwa hatawahi kunawiri katika maisha yake ya ndoa.

Wakati Bi Wanjiru alishika mimba ndipo mambo yaligeuka kuwa hasi na hadi leo hii, ‘kiapo’ hicho cha Shetani hakionekani kamwe kupungukiwa na makali yake.

“Mume wangu alifurahia sana habari kuwa nimeshika mimba… Mapenzi yake kwangu yalizidi na sijawahi katika maisha yangu ya hadi sasa kuoshwa na mapenzi ambayo alikuwa akinionyesha nikiwa na mimba hiyo… Hadi leo hii sijawahi kukutana na hali halisi ya kupendwa kama vile mume wangu alinionyesha mapenzi,” anasema Bi Wanjiru akikumbwa na ugumu mwingi wa kuongea kwa kuwa amepooza mwili kwa kiwango kikuu.

Bi Wanjiru hakuwa na kazi katika maisha hayo yao ya ndoa huku mumewe akiwa ni kibarua katika maeneo ya ujenzi wa majumba jijini.

Baraka

Kwa upande wa kulea mimba yake, Bi Wanjiru alishiriki mikakati ya kusaka utaalamu wa kimatibabu katika kliniki na hakukuwa na hali ya taharuki iliyokuwa ikijitokeza, matumaini yakiwa angejifungua bila wasiwasi wowote alee mwanaye akijiandaa kuzidisha uzazi ili kuweka ushahidi wa Baraka ya Mungu katika maisha ya kifamilia.

Aprili 28, 2012, alilazwa akiwa mgonjwa nambari 10294239 katika hospitali ya Kikuyu iliyoko Kaunti ya Kiambu akiwa na maumivu ya uzazi na madaktari wakamwambia kuwa uchungu huo wa uzazi ulikuwa umemjia mapema.

“Kilichofuatia ni mimi kulazwa na ambapo baada ya siku mbili nilijifungua mtoto wa kike na ambaye jina lake likawa ni Blessed Kangai (yaani, Baraka ya Mungu. Ni hapo tu hadithi yangu ya familia yangu inafikisha utamu wake kikomo. Maisha ya dhiki ndiyo yalifuatia; tena kwa nguvu,” anasema Bi Wanjiru.

Alipata shida za kuzaa kwa njia ya kawaida na ikahitaji afanyiwe upasuaji, na ambapo hali yake ya kiafya ilidhoofika na akapoteza fahamu kwa siku sita.

Bi Hannah Wanjiru, 35, (mbele kushoto) akiwa na mamake Bi Ruth Njeri, 80, nyumbani katika kijiji cha Gikarangu, Kaunti ya Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Aliporejelewa na fahamu zake, ikabainika kuwa alkikuwa amepooza mwili wake na ambapo mikono, miguu na kuanzia kiuno kuelekea chini alikuwa amepoteza hisia kabisa.

Yule mumewe wa kusaka vibarua katika maeneo ya mijengo akajipata katika hali hatari ya kulimbikiziwa madeni ya bili za kimatibabu.

Bili ya kwanza ilikuwa ya mkewe ambayo ilitinga ‘ukubwa’ wa Sh44,336. Naye yule mtoto wake akawa na matatizo ya kiafya akiwa na siku mbili ambapo hali ya kimatibabu iliyomkumba inafahamika kama neonatal jaundice na siku ya tatu, akakabwa na makali ya homa kali, bili yake katika hospitali hiyo ikitinga Sh20,458.

Kwa ujumla, bili hii ilitinga ukubwa wa Sh64,794 na ambapo Bw Munyua Ng’ethe aliweza tu kulipa Sh1,700 pekee.

Kulingana na Dkt James Mburu aliyekuwa akitibu wawili hawa, Bi Wanjiru alikumbwa na hali inayofahamika kama eclampsia na ambayo huandamana na kupoteza fahamu na kupooza.

Bi Wanjiru alielekezwa hadi hospitali kuu ya Kenyatta kupewa matibabu spesheli huku akijiingiza katika mkataba wa kulipa bili hizo zote.

Katika hospitali kuu ya Kenyatta, bili ilianza kujikusanya tena na ambapo ilitinga Sh42,000 hali ambayo ilimpa mume huyu taharuki kuu.

Ndipo aliomba apewe ruhusa ya kumtafutia mkewe huduma za kimatibabu katika hospitali mbadala na akapewa ruhusa.

Ndipo Bi Wanjiru alitolewa kutoka hospitali hiyo, akawekwa ndani ya lile gari kuukuu na kusafirishwa hadi kwa boma la mamake na ambapo waliwasili mwendo wa saa mbili usiku.

“Mumewe aliniambia kuwa alionelea ni heri amlete kwangu kwa kuwa yeye alikuwa hana wazazi ambao wangemtunza. Aliniambia kuwa akiwa katika boma langu, angerejea Nairobi na atafute pesa za kumsaidia mkewe pamoja na kulipa zile bili za hospitali,” anasema Bi Njeri.

Hiyo ndiyo siku ya mwisho ambayo mume huyu alionekana katika kijiji hicho na alitoka akiandamana na yule mtoto wao ambaye alikuwa amepata nafuu, akimwacha mkewe chini ya usaidizi wa mamake na majirani.

Shida kuu ni kwamba, Bi Njeri bado hutegemea vibarua ili ajipe riziki licha ya kuwa na umri wa miaka 80. Ingawa hivyo, yeye hupata afueni kupitia kupokezwa Sh2,000 ambazo serikali huwapa wakongwe wenye umri zaidi ya miaka 70 kila mwezi.

Kwa upande mwingine, Bi Wanjiru na ugonjwa wake huhitaji Sh3,000 kwa wiki kugharimia dawa, lishe speseheli na usafiri wa hadi Kliniki katika hospitali kadhaa za Kaunti ya Murang’a.

Majirani hupenyeza usaidizi wao katika hali hii ya masaibu kwa familia hii, sasa kukiwekwa shinikizo kwa Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Murang’a katika bunge la kitaifa Bi Sabina Chege awajibikie suala hili na atoe usaidizi wa kufaa.

Bi Hannah Wanjiru, 35, (mbele kushoto) akiwa na mamake Bi Ruth Njeri, 80, nyumbani katika kijiji cha Gikarangu, Kaunti ya Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Bi Chege ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Afya bungeni, sababu tosha ya kuwekewa presha awajibikie suala hili la mmoja wa anayewakilisha bungeni katika hali hii ya wazi kuwa inahitaji usaidizi wa dharura.

Kwa mujibu wa Dkt James Mburu aliyekuwa akitibu Bi Wanjiru katika hospitali ya Kikuyu, hali ambayo inamkumba mwathiriwa huyu wa uzazi ni hatari sana na hujidhihirisha kwa makali ya kupoteza fahamu baada ya kuzaa.

Anasema kuwa hali hii inafahamika kama eclampsia na ambayo huwa na ugumu sana kutambuliwa kabla ya kusababisha hali ya kupooza na kupoteza fahamu baada ya kujifungua.

Anasema kuwa hali hii huwakumba kina mama ambao huwa na shinikizo za mipigo ya damu na makali ya kujifungua huzua hali hatari inayofahamika kama chronic encapsulated intracerebral hematoma (CEIH).

Anasema kuwa ni asilimia 20 pekee ya wajawazito ambao huwa na bahati ya kutambuliwa wako na hatari ya kukumbwa na shida hii ya kiafya, hali ambayo iliingia katika madaftari ya kimatibabu mwaka wa 1981 na ambapo kati ya mimba 2000 na 3000, mmoja huwa katika hatari ya kuishia katika hali ya Bi Wanjiru ya sasa na ambayo (Mungu samehe) ataishi nayo hadi Mungu amjalie rehema zake katika maisha mapya ya kuzimu.