DINI: Mvumilivu hula mbivu mradi uwe nayo imani
Na FAUSTIN KAMUGISHA
WASWAHILI walisema mvumilivu hula mbivu.
Kuvumilia kunahitaji neema kutoka kwa Mungu.
Kuvumilia kunahitaji kuwa na imani na Mungu.
Sharti uamini kuwa Mungu ni mwaminifu na chochote alichoahidi atatimiza.
Biblia inasema pasipo imani huwezi kumpendeza Bwana, wala huwezi kumwona.
Sarafu yenye thamani kuu inayoweza kukupa chochote unachohitaji duniani si Dola ya Marekani wala Pauni ya Uingereza bali ni imani.
Lakini imani bila subira na uvumilivu si imani.
Watu wengi katika maombi yao hujifanya wana imani, lakini ukichunguza kwa makini, utagundua kuwa mbinu wanayotumia ni kujaribu kumlaghai Mungu.
Maombi yasipojibiwa kulingana na matarajio yao na kwa wakati wao, wanaishia kufanya maamuzi mabaya ambayo yanawadhuru baadaye.
Mungu hujibu maombi kwa wakati wake na kwa njia yake mwenyewe. Si lazima atumie njia unayojua na kutarajia.
Kuna dada mmoja aliyefanya kazi ya kibarua katika shirika moja la utangazaji, kwa muda mrefu aliyetamani awe mfanyakazi wa kudumu na mshahara wake uongezwe lakini haikuwezekana.
Ilifikia wakati ambapo alipoteza muda wake mwingi akilalamika kuhusu hali yake na mshahara wake mdogo. Alipojiunga na shirika lile, aliahidiwa ajira ya kudumu na nyongeza ya mshahara baada ya miezi sita, lakini alifanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja bila ahadi hiyo kutimizwa.
Katika hali ya kuzungumza na wafanyakazi wenzake aligundua kuwa kuna wenzake ambao pia walipewa ahadi sawa na yake lakini haikutimizwa. Jambo hilo lilimfanya kukata tamaa na akaamua kuacha kazi.
Wakubwa wake walimsihi asiache kazi maana walipenda kazi yake na tabia yake njema, wakamwahidi kwamba walinuia kutimiza ahadi yao siku chache zilizofuatia.
Lakini alikataa katakata kuwasikia na akaacha kazi kwa njia ya dharau.
Baada ya miezi mitatu, wakubwa wa shirika lile walitimiza ahadi yao kwa wafanyakazi waliosalia na kuwaongeza mshahara maradufu.
Habari hizo zilimfikia yule dada na kwa kuwa hakuwa amepata kazi nyingine, alijaribu kurudi na kuwabembeleza wakubwa hao wamrejeshee nafasi yake lakini hakuna aliyetaka kumsikia.
Majuto ni mjukuu
Alibaki akijuta, lakini wenzake waliovumilia waliendelea kufurahia uaminifu wa Mungu.
Katika kitabu cha Ruthu 1:1-6, Biblia inasema, “Ikawa zamani za Waamuzi walipoamua, kulikuwa na njaa katika nchi. Akaondoka mtu mmoja wa Bethlehemu ya Yuda, akaenda kukaa katika nchi ya Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili.
Na jina la mtu huyo aliitwa Elimeleki, na jina la mkewe Naomi, na majina ya wanawe wawili Maloni na Kilioni, Waefrathi wa Bethlehemu ya Yuda. Wakafika nchi ya Moabu, wakakaa huko. Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu.
Wakakaa huko yapata miaka 10. Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba Bwana amewajilia watu wake na kuwapa chakula.”
Walitoka Bethlehemu kwa sababu ya njaa. Bethlehemu maana yake ni Nyumba ya mkate. Kumbe hata katika nyumba ya mkate, kunaweza kuwa na njaa.
Elimeleki alijaribu kutafuta mkate katika nchi ya Moabu lakini badala ya kufarijika shida iliongezeka zaidi. Katika nchi ya Moabu, Elimeleki alifariki. Wanawe Kilioni na Maloni pia walifariki.
Naomi alibaki na wakweze Orpha na Ruthu ambao ni Wamoabu. Halafua baadaye Biblia inasema kuwa walipata habari kuwa Mungu amekumbuka Bethlehemu na kuwapa vyakula tele.
Kama Elimeleki angavumilia labda hangekufa katika nchi ya kigeni. Labda wanawe pia hawangekufa. Mara nyingi watu wanatoka walipo kwa sababu ya shida badala ya kumsikia Mungu kwanza.
Badala ya kupata furaha wanayoifwata, wanapata shida na kujuta. Ni heri kusubiri bwana katika kila hali.
Wakati mwingine anaweza kuonekana ni kama amechelewa lakini hayo ni mawazo yetu wanadamu. Mungu hachelewi wala hakawii. Mahali pazuri pia huwa na shida zake, lakini shida haibadilishi ukweli kuwa mahali hapo ni pazuri.
Tuwe na nia ya kubadilisha mahali tulipo ili pawe bora zaidi, badala ya kurukaruka, maana huenda tukapoteza baraka zetu kwa kukosa subira. Kama yule dada angevumilia kidogo tu, angefurahia nyongeza ya mshahara aliokuwa amesubiri kwa muda mrefu, lakini kwa kukosa uvumilivu alipoteza hata kazi na kuwaona wengine ambao hata labda hawakuombea nyongeza hiyo wakiifurahia.
Chunguza maisha yako na ujiulize ni wapi unakohisi kukata tamaa. Ni wapi unakojisikia kuchoshwa na kuvumilia. Ninazungumza kinabii juu ya maisha yako kuwa Bwana atakutimizia mahitaji ya moyo wako.
Hata kama umewahi kukosea usihukumike maana Mungu hubadilisha makosa yetu na kuyatumia kutubariki tena kwa utukufu wa jina lake.
Unaweza kuanza tena kumwamini Mungu na kuvumilia na hakika mwisho wako utakuwa mkubwa kuliko mwanzo wako. Amina!