Habari

Uhuru awaongoza Wakenya kuomboleza Bob

July 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta aliongoza Wakenya kumwomboleza Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Safaricom, Bw Bob Collymore aliyefariki Jumatatu asubuhi jijini Nairobi.

Mbali na kazi yake katika Safaricom, Bw Collymore alikuwa pia mwanachama wa Bodi ya Taasisi ya Kitaifa ya Kansa tangu Mei 2019 na mwanachama wa Bodi ya Ruwaza ya 2030.

“Tunapoomboleza na kutoa heshima zetu kwa kiongozi huyu mashuhuri mwenye maono, tukumbuke pia kusherehekea maisha na mafanikio yake. Ijapokuwa Bob Collymore ametuacha, amerithisha Wakenya na vilevile ulimwengu mzima kwa maisha yake ya kutia motisha,” akasema Rais kwenye taarifa.

Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga walimsifu Bw Collymore kama kiongozi shupavu wa kibiashara ambaye mchango wake haukuinua Safaricom pekee, bali maisha ya mamilioni ya Wakenya kwa jumla.

Risala za rambirambi sawa na hizi zilitolewa na viongozi wa matabaka mbalimbali wakiwemo wabunge, maseneta na magavana.

“Ni wakati wa usimamizi wake ambapo Safaricom ilikuza ushirikiano wake na Serikali za Kaunti kwa njia tofauti na kubadilisha mbinu za utendakazi katika Serikali za Kaunti,” akasema Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Bw Wycliffe Oparanya.

Wananchi nao walijumuika kwenye mitandao ya kijamii kuwapa pole jamaa na marafiki wa marehemu huku kifo chake kikigonga vichwa vya habari kimataifa.

Kutembea mitaani

Katika mtandao wa kijamii wa Twitter, Mwanaharakati Boniface Mwangi alieleza jinsi yeye pamoja na mwanamuziki Juliani walivyomtembeza Bw Collymore mitaa ya watu wa kipato cha chini ili afahamu vyema wateja wake.

Bw Collymore alijijengea sifa ya kutangamana na raia wa kawaida kwa njia tofauti ikiwemo kushiriki kwenye video za wanamuziki nchini.

Mtangulizi wake, Bw Michael Joseph alisema ingawa alifahamu Bw Collymore alikuwa anaugua sana, hakutarajia angefariki hivi karibuni.

“Sote tulishtushwa na kifo cha Bob. Huu ni wakati wa kusherehekea mchango wake kwa taifa hili mbali na Safaricom,” akasema Bw Joseph.

Wanahabari walimsifu mwendazake kama meneja aliyekuwa tayari kuhojiwa wakati wowote, tofauti na wakuu wengine wa mashirika wanaopenda kuhepa mahojiano ya wanahabari.