MAPOZI: Crystal Asige
Na PAULINE ONGAJI
KUSHIRIKI kwake katika kibao Extravaganza cha bendi ya Sauti Sol kumemfichua katika ulingo wa burudani huku sauti yake yake ya ninga ikizidi kumzolea mashabiki sio haba.
Ushiriki huu ulimpa Crystal Asige fursa sio tu ya kuimba pamoja na mojawapo ya bendi kuu barani Afrika, bali pia kumkutanisha na wanamuziki wengine kama vile Bensoul, Nviiri na kikundi cha Kaskazini.
Ingawa hivyo, wasilolijua wengi ni kwamba Crystal si mgeni ulingoni.
Ni mwandishi wa nyimbo na ana vibao kadha pia. Baadhi ya nyimbo zake ni pamoja na Me and You, Karibia, Back to Me na Show Me More miongoni mwa zingine.
Hasa anafahamika kwa kibao chake Pulled Under, wimbo unaojumuisha albamu yake ya kwanza Karibia.
Wimbo huu ulipanda hadi nambari moja kwenye chati za burudani nchini Uingereza mwaka wa 2016.
Hii ilimletea sifa na mashabiki wengi waliomsifu kwa kuleta mdundo mpya kwenye fani hii.
Aidha, kipaji chake cha uimbaji kimempa fursa ya kusafiri hapa nchini na ng’ambo na huenda hii ni mojawapo ya sababu zilizomfanya kuwa msanii wa kwanza na wa kike wa kipekee kusajiliwa chini ya lebo ya Sol Generation.
Crystal alilelewa mjini Mombasa ambapo alianza kuvutiwa na sanaa tokea utotoni huku ndoto yake ikiwa kuwa mwanamuziki au produsa wa filamu.
Akiwa katika shule ya upili aliendeleza ndoto hii huku akishiriki katika michezo ya thieta. Lakini matatizo yalibisha maishani mwake alipoanza kukumbwa na ugumu wa kusoma ubao na vitabu darasani kwa sababu ya kukosa kuona.
Ni suala lililomlazimu kupata matibabu lakini mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi ambapo ili kuficha udhaifu wake, angejifanya kwamba anaweza kufanya mambo sawa na wanafunzi wenzake.
Mwaka wa 2007 alipokamilisha shule ya upili, alienda nchini Uingereza kusomea masuala ya filamu na thieta katika Chuo Kikuu cha West of England, Bristol.
Akiwa huku matatizo yake ya macho yalizidi na baada ya kufanyiwa uchunguzi zaidi wa kimatibabu, alipatikana anaugua maradhi ya glaucoma yanayojulikana kuangamiza retina, sehemu inayopokea nuru ndani ya jicho.
Na baada ya kufanyiwa upasuaji mara kadha, hatimaye alipoteza kabisa uwezo wake wa kuona.
Japo kupoteza uwezo wake wa kuona kulikuwa changamoto kuu kwake sio tu katika maisha yake ya kawaida bali pia kimuziki, alijikakamua na kuzidi kujiundia jina katika fani ya burudani.
Mwaka wa 2014 alizindua albamu yake ya kwanza Karibia, iliyomtambulisha na kumshindia mashabiki sio haba.
Kutalii hapa na pale
Kama mwanamuziki binafsi, vilevile mwanachama wa bendi ya ‘Chemi Chemi LIVE’, amepata fursa ya kusafiri hapa nchini na ng’ambo.
Aidha, mbali na kuwa mwanamuziki, yeye pia ni msemaji na mjumbe wa VIP (Visually Impaired Person), shirika linaloangazia masuala ya watu wanaokumbwa na ulemavu wa kuona, ambapo yeye huzungumzia changamoto hizi kupitia chaneli yake ya YouTube “Blind Girl Manenos”.
Mojawapo ya mambo yanayomng’arisha sio tu muziki, bali imani yake thabiti na ukakamavu ambao amezidi kuuonyesha licha ulemavu wake.
Crystal ni kigezo cha wengi kwamba inawezekana kukabiliana na changamoto zako maishani na kuibuka mshindi kwa kutimiza ndoto zako, na haina shaka kwamba hii inampa nguvu ya kuzidi kujiendeleza kimuziki na kujijengea himaya katika ukumbi huu ambao umemfumbia macho kwa muda mrefu.