Makala

KAULI YA MATUNDURA: Haijathubutu kwamba kuna mkabala mmoja wa kuifasiri matini ya kifasihi

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BITUGI MATUNDURA

SOMO la fasihi ni muhimu katika mfumo wetu wa elimu.

Hakuna fasihi ya lugha moja iliyo muhimu kuliko ya lugha nyingine.

Ingawa baadhi ya wasomi teule huchangamkia fasihi iliyoandikwa kwa Kiingereza na kuipuuza ya Kiswahili, wasichojua ni kwamba wanakosa uhondo kuhusu Mageuzi ya Visiwani Zanzibar ya 1964 yaliyofumbatwa na watunzi kama vile Said A. Mohamed, (‘Asali Chungu’ na ‘Dunia Mti Mkavu’), Mohamed Suleiman Mohamed (‘Nyota ya Rehema na Kiu‘) na Shafi Adam Shafi (‘Kuli na Kasri ya Mwinyi Fuad‘) miongoni mwa waandishi wengine.

Nchini Kenya, tuna watunzi wakiwemo marehemu Peter Munuhe Kareithi (‘Kaburi Bila Msalaba’), Katama Mkangi (‘Walenisi’, ‘Mafuta’ na ‘Ukiwa’) ambao mchango wao katika utanzu huu hauwezi kupuuzwa.

‘Kaburi Bila Msalaba’ kwa mfano ni riwaya ya kihistoria inayoangazia madhila na mateso yaliyowakumba mashujaa wa Maumau ambao kwa bahati mbaya hawakunufaika kwa juhudi zao, pindi uhuru ulipopatikana.

Mashujaa wa uhuru kwa mfano Dedan Kimathi hawajulikani walikozikwa kwa sababu makaburi yao ‘hayana misalaba’. Hata hivyo, ili kuielewa na kuichanganua fasihi, msomaji anapaswa kufahamu mambo mawili muhimu.

Kwanza, kazi ya fasihi huwa na ulimwengu wake ambao hujengwa na mwandishi.

Huu ni ulimwengu ambao unadhibitiwa na kanuni za kifasihi – yaani kazi yenyewe hufuata kanuni zake. Pili, msomaji wa kazi ya fasihi huwa na ulimwengu wake.

Kwa hiyo, fasiri ya matini (texts) za kifasihi hutegemea makutano au kuja pamoja kwa ulimwengu wa msomaji na ulimwengu wa matini yenyewe. ‘Malimwengu’ haya chambacho Jay Kitsao huwafanya wasomaji wa fasihi kujiuliza maswali haya: Je, mtu anaposoma matini, maana ya kifasihi huwa wapi? Kwa matini? Kwa mwandishi? Kwa msomaji? Au kwa muktadha? Iwapo maana ipo kwenye matini, ni kwa nini wasomaji wawili au zaidi wanaosoma matini ileile wanaifasiri au kuielewa kwa namna mbalimbali?

Isitoshe, jinsi nilivyoifasiri tamthilia ya ‘Kinjeketile’ ya Ebrahim Hussein mwaka uliopita sivyo nitakavyoielewa na kuifasiri mwaka ujao.

Fasiri yaweza kubadilika

Matini haijabadilika ila kuna uwezekano mkubwa wa fasiri kubadilika. Iwapo maana inapatikana kwenye matini ya kifasihi, inakuwaje baadhi ya waandishi huwa hata hawajui maana zinazoibuliwa na wahakiki kuhusu kazi zao? Chinua Achebe kwa mfano aliwahi kushangazwa mno jinsi wahakiki walivyoielewa riwaya yake ya Things Fall Apart kuhusu maana aliyoikusudia.

Hili si jambo la ajabu kwa sababu jinsi wahakiki wanavyofasiri kazi ya mwandishi si shughuli ya mwandishi. Hata hivyo, ingawa matini hutiliwa mkazo sana tunapojaribu kuielewa maana ya kifasihi, kuna mambo mengine nje ya matini (patatext) ambayo yanaweza kuchangia katika kupata maana ya kifasihi katika kazi fulani.

Mambo haya ni pamoja na michoro (hasa katika fasihi ya watoto), habari kuhusu tajriba na mazingira yaliyomlea mwandishi, kusoma kazi nyingine za mwandishi yule yule, tahakiki za wahakiki wengine kuhusu kazi ile au hata kazi ambazo zinaingiliana kimatini na kazi fulani.

Kwa mfano, ili kuelewa tungo za Euphrase Kezilahabi na mwanatamthilia Ebrahim Hussein, falsafa ya ujamaa nchini Tanzania ni mhimili wa kurejelea.

Riwaya ya ‘Walenisi’ ya Katama George Chamanje Mkangi vilevile inaakisi pakubwa itikadi na mwegemeo wake alipokuwa hai.

Mkangi aliegemea falsafa ya ujamaa na hivyo basi, tungo zake zinaakisi hamaki dhidi ya mfumo wa kikapitalisti.

Kutokana na msimamo wake, Mkangi aliwahi kukwaruzana na serikali ya utawala wa Moi na kutiwa kizuizini.

Ngugi wa Thiong’o naye huegemea Umarx katika takriban tungo zake zote.