Habari

Zimbabwe yakosa fedha hata za kununua karatasi

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

SERIKALI ya Zimbabwe imekumbwa na upungufu mkubwa wa pesa kiasi kwamba, imeshindwa kununua karatasi na wino kutengezea pasipoti za raia wake.

Huduma hiyo imesimamishwa kwa sasa, huku maafisa wakuu wakisema hawana uhakika itarejeshwa lini, ikizingatiwa kuwa uchumi wa nchi hiyo unaendelea kuzorota.

Waliojisajili ili kupata hati mpya za usafiri au kubadilisha hati zao wanakabiliwa na tishio la kusubiri kwa muda usiojulikana kwa kuwa, serikali haina fedha za kigeni za kulipia karatasi maalum zilizoagizwa nje ya nchi, wino na raslimali nyinginezo.

Maafisa katika Afisi ya Msajili Mkuu walisema hata ikiwa wananchi wanataka kulipia usajili wa dharura wa pasipoti hawana budi kusubiri kwa muda wa hadi miezi 18 kabla ya hata kuwasilisha karatasi zao.

“Juni, wasajilishaji hao wa dharura walikuwa wakielezwa warejee mwishoni mwa 2020,” alisema afisa mmoja aliyechelea kutambulishwa.

Aidha, alisema waliotaka kujiandikisha walielezwa hakukuwa na tarehe yoyote iliyotengwa ambapo wangejisajili.

Mamilioni ya raia wa Zimbabwe wametorokea ughaibuni katika miaka 20 iliyopita wakisaka kazi huku mfumuko wa bei ukimeza akiba, nayo sekta rasmi ya ajira ikisambaratika.

Wengine wengi sasa wanatafuta njia za kuondoka huku hali ikizidi kuzorota chini ya uongozi wa Rais Emmerson Mnangagwa, aliyekuwa ameahidi ufufuo wa uchumi baada ya kumrithi Rais aliyetawala kwa muda mrefu, Robert Mugabe mnamo 2017.

Mfumuko rasmi wa bei ni takriban asilimia 100 – ambao ni wa kiwango cha juu zaidi tangu kuzuka kwa mfumuko wa bei uliokithiri ulioishurutisha serikali kuitema sarafu ya dola ya Zimbabwe mnamo 2009 – huku bidhaa muhimu kama vile mkate, dawa na petroli zikipungua mara kwa mara.

Mhitimu asiye na ajira

Isheanesu Mpofu, mwenye umri wa miaka 23 ambaye ni mhitimu wa chuo kikuu asiye na ajira aliwasilisha maombi ya kupata cheti cha usafiri mnamo Novemba 2018 lakini angali anasubiri.

“Nilirejea mwanzoni mwa Juni kufuatilia na nikaelezwa nirejee tena Agosti,” alisema Mpofu, akidokeza kwamba alitaka kuitembelea familia yake Ulaya.

“Vinginevyo, ni haki yangu kuwa na pasipoti ili niweze kusafiri kila nitakapo,” alisema. Mnangagwa aliangazia tatizo hilo mwezi uliopita, akisema mvutano na wachapishaji kuhusu deni ambalo halikuwa limelipwa ulimaanisha kampuni inayomilikiwa na nchi hiyo itachukua usukani wa kazi hiyo. “Walisema hawatachapisha pasipoti nyingine zaidi kwa sababu ya madeni ya ya awali” alisema.