• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
VITUKO: Patashika nguo chanika Pengo akifurushwa na bawabu wa TSC

VITUKO: Patashika nguo chanika Pengo akifurushwa na bawabu wa TSC

Na SAMUEL SHIUNDU

“USIMCHEZEE mtumishi wa Mungu aisee!” walimu wa Sidindi waliambiana kumhusu Pengo.

Wengi waliamini kwamba Mungu ndiye aliyemwokoa kutoka kwa kashfa aliyokuwa kapangiwa na mahasidi wake kwa ushirikiano na Sande, yule mwanafunzi mhuni. Wengine lakini walimshuku kwa kushiriki uchawi.

“Hakuna ramli asiyeijua huyo Pengo! Hata sasa nasikia yuko Tanzania kwa uchawi,” mwalimu mmoja aliwazulia wenzake walipokuwa wakinywa chai kuifukuza baridi ya Julai.

Aliyedhaniwa kuwa Tanzania alikuwa katika lango kuu la makao ya tume ya huduma kwa walimu akihangaishwa na bawabu.

“Siwezi kukusikiliza kama huna kibali kutoka kwa hedimasta wako!” bawabu alisema kwa kedi. Alimwangalia Pengo kwa dharau kana kwamba uwepo wa mwalimu huyu pale langoni ulimsahaulisha jambo muhimu.

“Hedimasta wangu kasafiri na nililojia ni la dharura. Tafadhali…” Pengo alijitetea kwa bawabu.

Bawabu alimhurumia Pengo lakini akakumbuka alivyotahadharishwa na wakuu wa tume. ‘Usimruhusu mwalimu yeyote kuingia hapa!. Buni visingizio vya kuwatimua.’

Aliufinga uso na kumwamuru Pengo kuondoka hapo mara moja.

Alikwaruza meno kama alivyofanya kila alipohamaki.

Hata mwenyewe hakujua kimemkasirisha nini. Hakujua iwapo alikasirishwa na kutoweza kumsaidia Pengo au kule kulazimishwa kuwadhalilisha walimu pale langoni.

Pengo aliufyata na kuondoka. ‘Kweli Mungu alinipa ualimu tu ati ndiyo kazi yangu?’ alijiuliza kwa huzuni. ‘Hakuna mtu anayedharauliwa hapa nchini kama mwalimu’ maneno ya Sindwele yalimjia akilini. Aliikumbuka siku hiyo Sindwele alipoitoa kauli hii. Mwenyekiti wa tume ya kuajiri walimu alikuwa kaizuru wilaya yao ya Sidindi na kuwahutubia walimu.

Kwenye hotuba yake, mkuu huyo wa tume alisisitiza kuwa licha ya kupandishwa vyeo hadi kuwa mwenyekiti wa tume, aliwaheshimu sana walimu na kazi yao ya ualimu.

“Mtaishi mzae na kujukuu na kamwe hamtaipata taaluma nyingine nzuri kama ualimu,” alisema mwenyekiti.

Makofi

Ukumbi ukaipokea kauli hii kwa makofi.

Huku wengi wakiifurahia hotuba ya mwenyekiti ambayo baadaye Sindwele aliifasiri kama kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa, Pengo na Sindwele hawakushangilia.

Pengo alikuwa akipitwa na maswali tele kumhusu mwenyekiti huyu aliyekuwa akiusifia ualimu. “Mbona kaiaga taaluma hii, kama kweli aliipenda na kuionea fahari kama anavyodai sasa?”

Pengo aliamini kwamba mwenyekiti huyu alikuwa tu kama wengine wengi ambao walikuwa wameishiba taaluma hii hadi kooni na kuigura. Lakini akina yakhe kama yeye waliachwa nyuma wakiitumia kupangusa machozi.

Yakhe waliomithilika na chungu ambao ganda la muwa la jana wao waliona kivuno.

You can share this post!

Zimbabwe yakosa fedha hata za kununua karatasi

Uhuru amzima Ruto

adminleo