Makala

MAPITIO YA TUNGO: Mzee Kigogo; maudhui mapana yanayoangazia jamii anuwai barani Afrika

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Jina la utungo: ‘Mzee Kigogo na Hadithi Nyingine’

Mhariri : Kitula King’ei

Mchapishaji: East African Educational Publishers Ltd

Mhakiki: Nyariki Nyariki

Kurasa: 140

HADITHI zilizomo katika diwani hii ya hadithi fupi ni kumi na zote zimetafsiriwa kutoka lugha ya Kiingereza.

Japo uandishi wa awali wa kazi hizi ulikuwa katika lugha ya Kiingereza, waandishi wazo ni Waafrika ambao wamekumbatia imani, itikadi, tamaduni na matamanio ya jamii pana ya Afrika – jambo ambalo yamkini lilichangia kwa kiasi kikubwa katika mwingiliano wa utamaduni wa Kiswahili na ule wa lugha nyingine za Kiafrika

Jambo jingine linalozipa hadithi hizi upekee wazo ni maudhui yake mapana ambayo yamezimulika jamii mbalimbali katika mataifa ya Afrika.

Humu mna maudhui ya mapenzi, usaliti katika mapenzi, siasa na usaliti katika kisiasa, ushirikina, ulaghai miongoni mwa mengine.

Maudhui ya mapenzi yanajitokeza katika hadithi ‘Veli Nyeupe‘ ambayo imeandikwa na Grace Ogot na kutafsiriwa na Kitula Kingei na ‘Pumzi za Mwisho’ ambayo imeandikwa na Samuel Kahiga na kutafsiriwa na Sarah Ngesu.

Wahusika wakuu katika ‘Veli Nyeupe’ ni Achola na Owila.

Ijapokuwa Achola anampenda Owila kwa dhati, hataki kushiriki naye ngono kabla ya ndoa.

Jambo hilo linamfanya Owila ‘kumtema’ Achola na kupanga kufunga ndoa na Bi Filomena Wariwa.

Hata hivyo, katika siku ya arusi, Achola anamtangulia bibi harusi kwenye ‘mimbari’ na kula kiapo na mpenziwe Owila huku Owila akimdhania Achola kuwa Bi Filomena.

Kunayo maudhui ya ushirikina ambayo yanajitokeza katika ‘Tekayo’ ambapo Tekayo, mhusika mkuu katika hadithi hiyo anawageukia wajukuu wake na kuanza kuwala mmoja mmoja baada ya kuonja utamu wa ini la binadamu alilompokonya tai.

Hadithi ‘Walimuuza Dadangu’ ambayo imeandikwa na Leteipa Ole Sunkuli inakashifu utamaduni wa kuwaoza watoto wa kike kwa lazima na kuzima ndoto zao za masomo.

Maudhui ya ulaghai yanajitokeza wazi katika hadithi ‘Mshindi’ ambayo imeandikwa na Barbara Kimenye na kutafsiriwa na Sarah Ngesu.

Habari zinapoenea kote kuwa Pius alikuwa ameshinda katika kamari ya kutabiri matokeo ya mpira, ghafla jina lake linaibukia kuwa maarufu katika ufalme wa Baganda.

Jamaa zake na watu wanaojinasibisha na Pius wanakusanyika nyumbani kwake si kusherekea ushindi wake bali kumwingiza mrija.

Kufikia mwisho wa hadithi, watu hao ambao hawaishi kumiminika katika kitende cha Pius wanaishia ‘kulifyeka’ shamba lake la ndizi. Wapo pia wanawake kama vile Sarah ambao wanamganda Pius mbavuni wakitaka kuolewa naye.

Hadithi nyingine katika mkusanyiko huu ni pamoja na Mzee Kigogo, Mazishi ya Benz, Kisa cha Baiskeli miongoni mwa nyingine.