Habari

Safaricom kufunga maduka ibada ya Bob ikifanyika

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MARY WANGARI

KAMPUNI ya mawasiliano ya Safaricom itafunga maduka yake yote Alhamisi, Julai 4, kama ishara ya heshima kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom, Bob Collymore aliyeaga dunia Julai 1.

Kufuatia hatua hiyo, vituo vyote vya Safaricom nchini vitafungwa kuanzia saa nne unusu asubuhi hadi saa nane unusu adhuhuri.

“Kama ishara ya heshima kwa kiongozi wetu mpendwa, Safaricom itafunga maduka yake yote nchini siku ya Alhamisi, Julai 4 kati ya saa 10.30 asubuhi na 2.30 adhuhuri ili kuwezesha familia na jamaa zake kukumbuka maisha yake,” kilisema kijisehemu cha tangazo lililochapishwa katika gazeti la Daily Nation.

Aidha, hatua hiyo inakusudia kutoa fursa kwa Wakenya kujumuika na familia na jamaa kukumbuka na kusherehekea maisha ya Bw Collymore.

“Kutakuwa na Ibada ya Ukumbusho kusherehekea maisha ya Bob mnamo Alhamisi, Julai 4 kuanzia saa tano itakayofanyika katika All Saints Cathedral, Nairobi,” ilisema taarifa hiyo.

Tangazo hilo lilisema kwamba ibada hiyo itapeperushwa moja kwa moja katika vituo vya kitaifa vya runinga na kuonyeshwa moja kwa moja katika uwanja wa Uhuru Park ili kuwapa Wakenya fursa ya kufuatilia matukio na pia kutoa heshima zao za mwisho kwa bosi huyo wa Safaricom.

Mwili wa mwendazake ulichomwa katika makaburi ya kuchoma miili ya wafu ya Kariokor mnamo Julai, 2.

Marehemu alifariki kutokana na maradhi ya saratani mnamo Jumatatu alfajiri Julai 1, akiwa nyumbani kwake Nairobi.

Haya yanajiri siku moja baada ya Bodi ya Safaricom kumteua aliyekuwa mtangulizi wa Bw Collymore, Bw Michael Joseph, kama kaimu kabla ya kumwajiri afisa mkuu wa kudumu.