Itumbi afikishwa mahakamani
Na MAUREEN KAKAH na MWANGI MUIRURI
DENNIS Itumbi amefikikishwa mahakamani Alhamisi kuhusiana na barua inayodaiwa kuwa ni feki ambayo ilidai kuna njama ya kumuua Naibu Rais William Ruto.
Upande wa mashtaka umeiomba mahakama kumzuilia kwa wiki mbili wakati ukiendelea na uchunguzi.
Itumbi anatuhumiwa kuchapisha barua katika kikundi cha WhatsApp cha mrengo unaohusishwa na kuunga mkono azma ya Ruto kuwania urais mwaka 2022.
Itumbi alikamatwa Jumatano alipokuwa akila chakula cha mchana jijini Nairobi na huenda akashtakiwa kosa la kuchapisha taarifa inayozuwa taharuki.
Uchunguzi wa mwanzo kabisa wa barua hiyo inayodai mawaziri wanne walikutana kupanga njama kumuua Ruto, unasema haiakisi ukweli, na kwamba iliandikwa na watu walio karibu na Naibu Rais.
Mawaziri wanne
Sicily Kanini Kariuki
Mwaka wa 2018 waziri huyu wa Afya alinusurika kitanzi cha kung’atuliwa afisini baada ya kuhudumu kwa miezi miwili pekee.
Njama hiyo ya kumtimua ilitibuka baada ya mashauriano na kile kilidaiwa ni vitisho vya kisiasa na ahadi za kutuliza hali kutembezwa kichinichini kutoka afisi za juu kisiasa.
Mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta na Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi, huyu Bi Kariuki alikuwa akituhumiwa kwa kuzembea kazini na kuwaonyesha wabunge dharau na kuchukua misimamo bila kujadiliana.
Ni madai aliyoyakanusha na akaondolewa lawama na kamati ya bunge kuhusu afya ikiongozwa na Bi Sabina Chege.
Bi Chege aliteta kuwa Bi Kariuki alikuwa akilengwa kwa kuwa ni mwanamke!
Mwaka 2018 kulizuka tena harakati za kutaka kumtimua baada ya visa vya ukiukaji wa haki za wagonjwa kuripotiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.
Kwa mara nyingine tena, alinusurika.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Afya, alikuwa Waziri wa Masuala ya Vijana na Jinsia, akichukua baadhi ya majukumu ya Bi Anne Waiguru aliyekabiliwa na tuhuma za kuwepo kwa ufisadi wizarani. Alilazimika kujiuzulu akisema daktari alimshauri kufanya hivyo. Ingawa hivyo, aliishia kuwania na kutwaa kiti cha ugavana katika Kaunti ya Kirinyaga.
Bi Kariuki ni mtaalamu aliyehitimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi katika biashara, akapata uzamili wa taaluma hiyo katika chuo cha Maastricht.
Pia ana shahada ya uzamifu (PhD) katika masuala ya ubora wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Michigan.
Kabla ya kupandishwa cheo na UhuRuto hadi kuwa waziri, alikuwa katibu maalumu katika Wizara ya Kilimo na Ustawishaji Mifugo na Samaki.
Katika utawala wa Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki, alikuwa mkurugenzi katika Bodi ya majanichai nchini na utendakazi wake ukainua sekta hiyo hadi kuvunia wakulima Sh130 bilioni mwaka wa 2012.
Madaraka mengine alishikilia wakati wa Mzee Kibaki yalikuwa katika Fresh Produce Exporters Association of Kenya na Kenya Investment Authority.
Ametuzwa na UhuRuto katika kitengo cha Life Governors Award.
Mkwasi si haba, mwaka wa 2015 alidokeza kuwa utajiri wake ni Sh168 milioni akisema ni jasho lake la kuchapa kazi na kuwekeza.
Wakati Sicily akichapa kazi katika mamlaka ya majanichai nchini, dadake naye kwa jina Loise Njeru alikuwa mkurugenzi katika mamlaka ya kahawa nchini, kwa pamoja ndugu hao wawili wakidhibiti sekta ambazo kwa utajiri zilikuwa zimetinga Sh400 bilioni.
Wao hushikilia kuwa baba yao mzazi ndiye aliwapa motisha kuafikia makuu katika maisha yao ambapo wakiwa wenye umri mdogo alikuwa akiwapa ushauri wa kuwaweka guu mbele katika kuafikia makuu ya kimaisha.
Huku Katiba ikitafsiriwa na wengine kuwa imewakanya mawaziri wa serikali kujingiza kwa siasa, taifa likielekea kwa uchaguzi wa 2017, Sicily alisema hilo halitambui.
Alisema kuwa “sio tu kumpigia debe Rais Uhuru Kenyatta, bali pia tutaparaga miti kufanya hivyo”.
“Umoja wa serikali unaruhusu kila aliye katika huduma ya kuafikia malengo yake ya kiutawala ahamasishe wananchi kuhusu yale yametimizwa na pia yale yanayoapangwa,” akasema Bi Sicily Kariuki.
Aliongeza: “Nasikitikia wale ambao kila uchao wanateta kuwa mawaziri wa Jubilee wanajihusisha na siasa za uchaguzi wa 2017. Nasema hivi: Rais Kenyatta ndiye mwafaka zaidi kuchaguliwa tena ili atimize mengi ambayo tumeandaa.”
Aliongeza kuwa kazi moja kuu ya waziri ni kutoa elimu ya uhamasisho kwa umma kuhusu suala lolote nyeti na lile la uchaguzi ni mojawapo ya masuala hayo.
Alisema kuwa wale ambao wamepitia shule ya somo la siasa wanajua wazi kuwa “jina mwanasiasa halina maana inayotambulika rasmi na hatimaye katika huo mchanganyiko, sote tunaorodheshwa kuwa wanasiasa.”
Alisema kuwa ufichuzi huo kwa wale ambao hawajang’amua hilo wasake maelezo kamili kuhusu “ambiguity of politics”, yaani, utata wa siasa.
Kariuki alisema kuwa kila Mkenya au mwingine yeyote ulimwengu huu ni mwanasiasa na “wale wote ambao wanasema waziri hafai kuwa mwanasiasa wanajidanganya wao wenyewe na pia kudanganya umma”.
Kando na hilo, alisema kuwa waziri wa serikali ana wajibu wa kikatiba wa kuandaa mikutano ya wadau ili kupata maoni kuhusu utenda kazi wa serikali na pia kuwapa wananchi hao mwongozo wa yale ambayo yameratibiwa kutekelezwa.
“Ikiwa ratiba ya utekelezaji inawiana na mito ya yule aliye mamlakani achaguliwe tena, basi tutapanda juu ya miti kutangaza hayo,” akasema.Sasa akiwa ndiye mwanamke wa kipekee kudaiwa kujiunga na wanaume watatu ambao ni mawaziri wenza katika serikali ya Jubilee kupanga mauaji ya DP Ruto, itabakia kuwa hali ya kumpa macho na masikio “kikieleweka.”
James Wainaina Macharia
Ndiye Waziri wa Uchukuzi, Miundombinu na Makazi.
Macharia alizaliwa mwaka wa 1959 katika kaunti ndogo ya Kigumo iliyoko katika Kaunti ya Murang’a.
Alisomea katika Shule ya Upili ya Kagumo na kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo ni mhitimu katika taaluma ya kibiashara. Ana shahada ya uzamili katika taaluma hiyo kutoka taasisi ya Henley Management College.
Pia, ni mhasibu (Chartered Public Accountant) baada ya kuhitimu katika taasisi ya Wales.
Akiwa mume wa Pamela Chanda na ambapo wamejaliwa watoto wawili, amefanya kazi za uhasibu katika Deloitte & Touche, akawa Mkurugenzi katika Benki za African Banking Corporation nchini Zambia na Tanzania, Benki ya NIC, na pia aliwahi kuwa mratibu wa masuala ya mikopo katika benki ya Standard Chartered kabla ya mwaka wa 2013 kujipata katika baraza la mawaziri akiwa Waziri wa Afya.
Akiwa waziri, Wakristo waliwahi kumsuta wakidai ana mapendeleo kwa mashoga na wasagaji baada ya kushinikiza hoja ya Seneta wa Murang’a, Irungu Kang’ata ya kukemea makundi hayo mawili iondolewe bungeni kwa msingi kuwa ilikuwa na nia ya kuwabagua.
Pia, alihusishwa na kutoweka kwa Sh5 bilioni za Wizara ya Afya mwaka wa 2016 na ambapo alitakiwa kujiuzulu lakini akanusurika.
Akiwa mwandani wa familia ya Rais Uhuru Kenyatta, hajajipata mkekani katika shinikizo za kutaka ang’atuke licha ya kuhusishwa na mradi mkubwa wa mtambo wa reli ya kisasa na ambao umeanza kuangaziwa katika taswira ya ufisadi.
Akitetea mradi huo uliogharimu Sh327 bilioni, anasema kuwa kwa mwezi SGR inaleta kipato cha Sh400 milioni.
Alisema kuwa kwa mwezi pato ni Sh2.2 bilioni huku gharama zikiwa ni Sh1.82 bilioni; hivyo basi kushikilia kuwa hiyo ni hesabu ya faida.
Anasema SGR ina faida tele katika uchukuzi wa abiria na inatarajiwa kuzidisha faida hiyo wakati biashara ya uchukuzi wa mizigo itashika kasi.
“Kwa sasa SGR iko katika mkondo sawa wa kibiashara. Hakuna shaka yoyote kuwa ni mradi wa manufaa halisi kwa uchumi wa taifa. Na kwa kuwa tunaendelea mbele na kujenga mkondo wa kuelekea hadi Naivasha, katika siku za usoni, faida kutoka uchukuzi wa reli itakuwa ya umuhimu mkubwa katika uchumi wa kimaeneo na taifa,” akasema Macharia.
Alisema katika kipindi cha mwaka wa kifedha wa 2019/20, ukadiriaji ni kuwa pato kwa mwezi kutoka huduma za SGR litakuwa Sh3.3 bilioni.
“Kabla ya mwaka wa 2022, faida pekee kutoka SGR itakuwa zaidi ya Sh5 bilioni. Walio na ufahamu wa hesabu za uwekezaji watakiri kuwa faida hupanuliwa katika kipindi fulani cha utendakazi. Kwa sasa SGR yetu iko katika mkondo huo wa upanuzi na itaimarika iwe kiungo thabiti cha pato kwa uchumi kwa taifa,” akasema.
Joseph Wakaba Mucheru
Ndiye Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).
Joseph Wakaba Mucheru, 53, alipewa kazi hii ambayo ilikuwa ndani ya udhibiti wa Waziri wa sasa wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’I aliyehamishiwa hadi Wizara ya Elimu kabla ya kutua kwa Wizara ya Usalama na ambapo pia ndiye mwenyekiti wa kamati ya baraza la mawaziri ya kushirikisha miradi ya serikali kuu.
Mucheru alikuwa mwajiriwa wa kampuni ya katika ukanda wa Sub-Saharan Africa (SSA) na akiwa balozi wa kampuni hiyo sambamba na kuwa Meneja wa taifa la Kenya wa Google.
Ashawahi kufanya kazi na kampuni ya Wananchi Online, ambayo alianzisha mwaka wa 1999.
Alizaliwa katika kijiji cha Kamirithu katika kaunti ndogo ya Limuru iliyo katika Kaunti ya Kiambu.
Alisomea katika Shule ya Msingi ya Nairobi Primary kabla ya kujiunga na ile ya Lenana High kwa masomo ya sekondari na hatimaye akajiunga na London’s City University na pia kile cha Stanford, alikohitimu mwaka wa 2008.
Rais mstaafu Mwai Kibaki alimtuza tuzo ya Moran of the Order of the Burning Spear mwaka 2010.
Amekuwa mwokovu katika imani ya Kikristo kwa miaka 27 sasa na ni mume na baba na ambaye anasema kivutio chake kikuu katika huduma ya serikali ni marehemu John Michuki.
“Uwezo wa Michuki wa kutekeleza masuala mazito bila kujali athari za kukemewa ndio nguzo yangu kazini na Mungu ailaze roho ya Michuki pema Peponi,” anasema Mucheru.
Mpenzi wa mchezo wa gofu, anasema kuwa ni mwanachama katika vilabu vya Muthaiga, Railways na Nyahururu na ambapo amejinunulia shamba katika Kaunti ya Nyeri ambapo hushiriki kilimobiashara.
Mwongozo wake katika maisha anasema kuwa ni: ‘Binadamu hupanga mkondo wake wa kimaisha, lakini Mungu ndiye wa kumwongoza’.
Peter Gatirau Munya
PETER Munya anajulikana vyema kwa weledi wake kisiasa, uwezo wa kujipanga upya kisiasa na kukuonyesha hadharani ikitokea kwamba mmetofautiana.
Aling’ang’ana kukutu; kufa kupona kuhifadhi wadhifa wake wa ugavana katika Kaunti ya Meru baada ya kuchaguliwa 2013 lakini mawimbi ya Jubilee yakivurumishwa na Kiraitu Murungi yakamsomba kwenye uchaguzi wa Oktoba 8, 2017.
Baada ya ushindi wa rais Uhuru Kenyatta kubatilishwa na mahakama ya Juu na kuamrishwa Wakenya warudi kwa debe Oktoba 26, 2017, Munya kwa hasira akatangaza kuwa alikuwa amejiunga na National Super Alliance (Nasa).
Ajabu ni 2007 Munya na Koigi wa Mwere kujitokeza katika Kaunti ya Kiambu katika hifadhi ya kitamaduni ya Kamirithu wakiandamana na wafuasi kadhaa wa kundi haramu la Mungiki na ambapo walitetea kundi hilo wakisema badala ya kuandamwa na maafisa wa polisi, walifaa kusajiliwa katika jeshi la kitaifa.
Alikuwa awali amekataa katakata kujiunga na Jubilee na ndipo akafufua chama cha Mzee Mwai Kibaki cha Party of National Unity (PNU).
Aliwania nacho akaangushwa sakafuni na Murungi na akainuka akiwa analia alichezewa ngware, hivyo basi kujiunga na Nasa ili akimbizane na haki yake ya kutambulika kisiasa.
Taharuki iliyowaingia UhuRuto kufuatia hatua hiyo ya Munya iliwaelekeza hadi Meru kumchumbia Munya na ndipo wakamwahidi kuwa wangemkumbatia ndani ya serikali ya kitaifa iwapo wangeishia kuwa washindi.
Leo hii, Munya ni Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki (EAC), wadhifa ambao sio mgeni nao kwa kuwa alihudumu katika afisi hiyo katika utawala wa Mwai Kibaki.
Mzawa wa eneo la Muthaara mwaka wa 1970, Munya anaonekana kubeba ndoto za vijana wa Meru ambapo anapendwa si haba bali kura zikawa hazitoshi kumnusuru kuanguka ugavana.
Ujasiri wake ulimzalia matunda alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Muungano wa Magavana nchini na ambapo hakuchelea kusuta serikali ya Uhuru Kenyatta mara kwa mara akitetea ugatuzi.
Aling’atuliwa kutoka kwa ugavana mwaka wa 2014 lakini akakimbia mahakamani kukata rufaa na ambapo alinusurika katika mahakama ya juu zaidi.
Januari 1995 alikuwa katika chuo cha Brussels nchini Ubelgiji ambapo alikuwa amefadhiliwa na ubalozi wa taifa hilo na ambapo alipata hati ya uzamili kwa sheria za kimataifa.
Aliishia katika chuo cha Georgia, Marekani ambapo alipata hati ya pili ya uzamili katika taaluma hiyo.
Mwaka wa 1993 alikuwa katika chuo kikuu cha Nairobi kwa shahada yake ya kwanza kuhusu uanasheria.
Ni mwanafunzi wa uanasheria katika kampuni ya Kamau Kuria na Kiraitu akiwa ni mwanafunzi wa zamani wa shule ya upili ya Chogoria na pia ile ya Meru.
Mwaka wa 2002 aliunda kampuni ya uansheria akishirikiana na mshirika na ikapewa jina Kimayo na Munya Advocates.
Ni katika kipindi cha 2000 na 2002 ambapo alikuwa mhadhiri wa somo la sheria katika Chuo Kikuu cha Moi.
Amekuwa mhadhiri pia katika taasisi za Kenya School of Professional Studies (KSPS) na Kenya School of Monetary Studies (KSMS).
Katika uchaguzi wa 2007, alichaguliwa kuwa mbunge wa Tigania Mashariki.
Aliteuliwa kuwa naibu waziri wa usalama wa ndani ya Oktoba 2006 na Desemba 2007.
Ni mtoto wa Mzee Jackson Munya M’Rukunga na Mama Grace Mwakithi na ambapo ni mume wa Phoebe Munya na baba wa Karauni na Nkio Munya.