Makala

Masaibu ya Ruto ni njama ya kumbadilisha na Raila serikalini?

July 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

KATIKA siasa yote yawezekana bora tu yawe yamepangwa vizuri.

Kuna wasiwasi mkuu kuwa Rais Uhuru Kenyatta amezindua njama kali ya kumshinikiza Naibu Rais William Ruto ang’atuke na badala yake, Raila Odinga ateuliwe katika wadhifa huo.

Mhadhiri wa somo la siasa, Gasper Odhiambo anasema uwezekano wa kuwepo njama hii unatokana na ushahidi wa kiusemi wa Rais mwenyewe.

“Rais Kenyatta amesikika hadharani akimsuta naibu wake kama aliye na mazoea ya kutangatanga. Amesikika si mara moja akisema kuwa mpango wake wa sasa kuhusu 2022 utashtua wandani wake ndani ya Jubilee licha ya kuahidi angehudumu kwa miaka 10 na kisha amkabidhi Ruto naye kwa awamu ya kwanza na amuunge pia ya pili. Hali ya kushtua inawezekana tu kwa kumpa Ruto talaka,” asema Odhiambo.

Pia, anasema kuwa ni hivi majuzi akiwa katika kongamano la Akorino ambapo alitangaza hakuna wa kumzuia kufuata ile barabara “nimejitengenezea ya kupeleka watu wetu (Jamii za Mlima Kenya) kwa manufaa halisi ya amani kwa miaka 50 ijayo.”

Odhiambo anasema hii ni ishara tosha kuwa Ruto hayuko katika hesabu ya Rais ifikapo mwaka 2022.

Aidha, hatua ya kiongozi wa nchi kutangaza ni yeye ndiye alijitafutia kiti na kuwasaidia baadhi ya wabunge kupata nyadhifa hizo ina maana kuwa DP Ruto alipata wadhifa huo kwa kuwa Rais alimkubali awe mgombea mwenza.

Matamshi ambayo Bw Odhiambo anashikilia ni msumari wa mwisho kwa jeneza la unaibu wa urais wa Ruto ni yale Rais alitoa: “Nimechoka na hii takataka mnayoita wanasiasa na nitawang’oa kutoka nyadhifa hizo mlizo nazo.”

“Rais hana uwezo wa kuwang’oa wanasiasa wengine ila tu naibu wake na ambapo Katiba imempa uwezo wa kuteua mwingine kwa usaidizi wa bunge kwa kipindi cha siku 30,” asema Odhiambo.

Masaibu ya Ruto yalianzia pale Rais Kenyatta alisalimiana na Odinga katika kile kinafahamika kama ‘handshake’.

Inadaiwa hatua hiyo imesababisha kila aina ya changamoto kwa DP Ruto na ndiyo sababu anapambana kufa kupona kujinusuru, kiasi cha kutangaza kuwa kuna njama ya kumuua.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema katika somo la siasa, uvumi huwa sio wa ukweli hadi wakati ule utakanushwa na walio ndani ya uvumi huo.

Katika hali hiyo, tayari waliotajwa kupanga kumuua Ruto wamekanusha. Hawa ni mawaziri Peter Munya, Sicily kariuki, Joe Mucheru na James Macharia.

Wadadisi wanasema inaweza kuwa sio mauti kwa Ruto yanapangwa bali ni mauti kwa unaibu wake wa urais.

Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro anasema kuna habari za kuaminika kuwa kuna njama ya kumng’atua DP Ruto kutoka unaibu wa urais lakini wanaopanga njama hizo wanalemewa kwa kuwa Katiba itazua utata na pia kutakuwa na athari mbaya za kisiasa kutoka kwa wafuasi wa Ruto.

“Mbinu inayotumiwa ni ya kumdunisha Ruto kama mfisadi, asiye wa kuaminika na ambaye hana uwezo wa kuongoza taifa ambalo linasaka umoja wa kijamii,” asema Nyoro.

Nyoro anasema njama hizo zote zimezinduliwa huku Ruto akizitibua kutokana na ueledi wake wa kisiasa na wa kuwa na mitandao ya kina ya kumkusanyia ujasusi wa yale yanayopangwa.

Mbunge wa Bahati Bw Kimani Ngunjiri anasema mwaka 2018 Odinga alikuwa amedokeza kuwa alikuwa na nia ya kumng’atua Ruto kutoka kwenye ushawishi wa kurithi Ikulu ifikapo mwaka 2022.

“Alianza kwa kusema Ruto hakuwa na uwezo wa kurithi Ikulu bila mchango wake (Odinga). Alionya kuwa alikuwa ameandaa mbinu ya kuingia katika hesabu ya urithi ndani ya serikali na ndipo salamu hizo za maridhiano zilishikishwa kasi na kuanzia wakati huo Rais akaonekana kujitenga na afisi ya naibu wake,” asema Bw Ngunjiri.

Anasema matunda ya handishake yamekuwa ni kupiga vita wote ambao walikuwa viungo muhimu katika ushindani wa kisiasa na kuishia kumuidhinisha Ruto kutwaa mamlaka ya uongozi.

Asema: “Tangu hizi salamu ziingie, Rais anaonekana waziwazi kuongoza njama kali za kumzima Ruto. Amekuwa akitangaza sera zinazoonyesha waziwazi kuwa zinamlenga Ruto. Inaonekana kuwa kuna mwanya unaosakwa kwa hila na njama wa aidha Ruto ahujumiwe hadi ajiuzulu au kuzuke msingi thabiti wa kumwandalia njama ya kumng’atua ama kupitia jopo maalumu au kufutwa kazi moja kwa moja.”

Bw Ngunjiri anasema shida kubwa ni kuwa ndani ya bunge kuna wingi wa ufuasi kwa Ruto na pia katika jumuia ya wapigakura, anabakia akiwa na ufuasi mkuu na ambao unatatiza njama hizo kutimizika.

Mchanganuzi wa masuala ya siasa Prof Macharia Munene anasema siasa ni mchezo sawa na wa kamari na ambapo kwa wengi, taswira maalumu huwa ni ya pata potea.

“Ingawa kwa sasa hakuna ule uhakika kuwa Rais Kenyatta anapanga kumtema Ruto, kuna ubashiri wa hadi asilimia 70 kuwa hawa wawili hawako pamoja kama walivyokuwa katika kipindi cha 2013 hadi 2017,” asema Prof Munene.

Anasema leo hii, kwa maongezi, mienendo na matendo, Rais yuko na imani kwa Odinga kwa asilimia kubwa kuliko ilivyo kwa Ruto.

Anasema madai haya ambayo yameanza kutandazwa hadharani kuwa kuna njama ya kumuua Ruto yatazidisha mwanya wa utengano kati ya Rais na naibu wake huku mikakati ya kunusuru amani ya taifa na uthabiti wa kiuchumi ikitegemea mshikamano wa Rais na Odinga.

“Hatari kuu katika hesabu hii iko dhidi ya Ruto. Rais akiungana na Odinga na wasukume mabadiliko ya kikatiba na sheria, Ruto atatemwa na Wakenya wakubaliane na hatua hiyo huku hata pengine kesi ikiandaliwa mahakamani kupinga kutemwa kwake iangushwe na umoja huo kwa msingi wa kunusuru taifa,” asema.

Katika hali hiyo, Ruto atajipata nje ya serikali ndipo akashirikishe siasa zake za 2022 bila mgongano na msimamo wa Kenyatta na Odinga.

Hilo likifanyika, Munene anasema Ruto atakuwa ametoa nafasi ya kuandaliwa kwa mpangilio wa umoja wa kitaifa kupata mrithi wa 2022 ambaye ataungwa mkono na jamii nyingi nchini na yeye (Ruto) ajipate amemalizwa kisiasa.